Wawekezaji kuna fursa kiwanda cha ‘helmeti’

03Dec 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe Jumapili
Wawekezaji kuna fursa kiwanda cha ‘helmeti’

WAKATI taifa linaweka msukumo mpya wa kuanzisha viwanda , ni muda wa kuangalia vitu ambavyo vinahitajika ili fursa za uwekezaji zilizoko zihimize kuanzisha viwanda ambavyo vina umuhimu  wa kipekee. 

Kofia ngumu kwa ajili ya abiria wa bodaboda ambao sasa wako Tanzania nzima ni moja ya maeneo ambayo yanahitaji kujengewe viwanda.

 

Tanzania inahitaji kiwanda cha helmeti kwa sababu  mamilioni ya watu wake  wanapanda bodaboda wakubwa kwa wadogo ambao kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 inazungumzia uvaaji wa kinga hiyo, japo inamlazimisha dereva wa pikipiki pekee  kuwa na kofia hiyo lakini si abiria.

 

Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji Majini na Nchikavu (Sumatra) imetoa kanuni inayolazimisha kila abiria wa pikipiki mdogo kwa mkubwa kuvaa kofia ili kujikinga na ajali inayoweza kuumiza kichwa.

 

Kinahitajika kiwanda kwa sababu kofia hizo sasa zinaonekana kuwa ni bidhaa muhimu inayohitajika nchini kwa ajili ya wakubwa kwa wadogo wanaopanda boda boda walio vijijini na mijini ili wajikinge na kuumia kichwa ajali inapotokea.

 

Hata hivyo, msukumo mwingine unahitajika kuwekwa kwenye viwanda hivyo kwa kuwa hakuna helmeti kwa ajili ya watoto wadogo licha ya kwamba kuna sheria inayokataza kuwapandisha kwenye bodaboda watoto wenye umri wa chini ya miaka tisa, hivyo ni wakati wa kuangalia uwekezaji kwenye kofia ngumu za  watoto  wenye zaidi ya miaka tisa ambao wanatakiwa pia kuvaa kinga hiyo wakipanda pikipiki.

 

Umuhimu wa kiwanda cha helmeti unaonekana nyakati hizi kwa kuwa hata abiria  ambao licha ya serikali  kutoa maagizo ya kuvaa  kofia hizo wanazikataa. Hazikubaliki kutokana  na uduni unaotokana na utunzaji mbovu.

 

Wanaziona ni chafu lakini pia hazina mikanda wala vishikizo vya kuzifunga na kuzibana shingoni ili zisianguke. Wapo abiria hasa wanawake wana nywele nyingi ama wamefunga vilemba kiasi cha kukwamisha uvaaji helmeti.

 

Ni vyema kuwa na msukumo wa kujenga kiwanda cha kofia hizo ambazo zitapatikana kwa ukubwa wa aina mbalimbali  , iwe kwa ajili ya watoto, wakubwa na wenye urembo wa nywele ambao unahitaji kofia maalumu .

 

Vyombo vya usalama  na Sumatra vinaweza kushuhudia jinsi uvaaji wa helmeti unavyofanyika kwa  geresha na kupotosha lengo la kujilinda na ajali barabarani.

 

Abiria wanaziegesha kofia kichwani hawazibani, hawazifungi shingoni na kuhakikisha kuwa ni timamu na hazidondoki. Kinachoendelea ni kuegesha kofia hizo na kuzishikilia ili zisianguke.

 

Abiria ana mkono kichwani muda wote wa safari akishikilia kofia ngumu.    

                     

Vyombo vya usalama na abiria wajihoji inawezekanaje kushikilia kofia isidondoke na pia kujishika ili mtu asianguke? Yote hayo hayawezekani, mshika mawili moja humponyoka.

 

Wasafiri huwa hawapendi kofia ngumu, nyingine zimechakaa na zinanuka .

 

Pengine kukiwa na kiwanda cha kuzalisha vifaa hivyo kanuni za Sumatra zitaagiza kila mtumia boda boda awe na kofia hiyo.

 

Ni wazi kuwa Tanzania siyo ya kwanza kuwa na usafiri wa pikipiki, zipo nchi zinazotumia usafiri huo kama Ujerumani , Japan na Sweden.

 

Taifa lijifunze jinsi wanavyotengeneza miundombinu ya pikipiki, baiskeli, magari na pia wanavyowakinga watoto na ajali za pikipiki.

 

Sumatra na Polisi zinafahamu fika kuwa piki piki zinawezesha wanafunzi kuwahi shuleni kwa hiyo zitoe maelekezo ya kuwapo kwa helmeti za watoto, mikanda na utaratibu wa kuzitumia. Si hivyo, pia wataalamu wa afya wanaweza kushauri jinsi ya kuziendesha ili kuzuia upepo na vumbi usiumize njia za hewa au vifua vya watoto hao wadogo.

 

Licha ya kujifunza na kuandaa mikakati ya kujenga viwanda vya helmeti nchini, serikali inapojenga na kupanua barabara kuu ikiwamo ya Morogoro, barabara za manispaa katika wilaya na mikoa mbalimbali ikumbuke kujenga miundombinu ya pikipiki na baiskeli  kwa kuwa ni usafiri mkongwe na wa siku nyingi ambao utaendelea kutumiwa kila wakati na vizazi vya sasa na vijavyo.

Habari Kubwa