Wawekezaji madini Ulanga walipoanza maisha kwa ofisi ya kijiji

14Feb 2020
Romana Mallya
Mahenge
Nipashe
Wawekezaji madini Ulanga walipoanza maisha kwa ofisi ya kijiji
  • Waziri shuhuda, adokeza ya fidia.
  • Yatajwa kila kitu vifaa elektroniki

FEBRUARI Mosi mwaka huu, imekuwa tarehe muhimu kihistoria kwa wanavijiji wa Mdindo, Kisewe na Nawenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, baada ya kukutana kwenye uwanja uliozungukwa na milima yenye uoto wa asili, kupokea majengo mapya matatu ya ofisi za vijiji vyao.

Waziri wa Madini, Doto Biteko, akikabidhi funguo za ofisi za Serikali ya Kijiji cha Mdindo, Kisewe na Nawenge wilayani Ulanga, baada ya kujengwa na kampuni ya uchimbaji madini Mahenge Resources. Kulia kwa Waziri ni Mwenyekiti wa kampuni hiyo, John de Vries. PICHA ZOTE: ROMANA MALLYA

Licha ya mvua kubwa kunyesha, baadhi ya barabara ndani ya vijiji zikipata changamoto kutopitika, mamia ya wanakijiji walijikusanya katika uwanja huo uliopo Mahenge, ambako makabidhiano ya ofisi hizo yalifanyika.

Hapo pameigharimu kampuni ya Mahenge Resources Sh. milioni 51 na iliyoko katika mchakato kujenga mgodi mkubwa wilayani humo, kwa ajili ya kuchimba madini ya kinywe (graphite).

Ni madini yanayotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile breki, kinga za mashine, betri za simu, kompyuta mpakato (laptop) na penseli.

Shughuli za makabidhiano kiofisi kwa upande wa serikali, alikuwapo Waziri wa Madini, Doto Biteko, aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya, mbunge wa jimbo hilo, Goodluck Mlinga na viongozi wengine sekta ya madini.

Kampuni ya Mahenge, alikuwapo Mwenyekiti, John De Vries, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Black Rock Mining kutoka Australia.

Kabla ya viongozi hao kuwasili eneo hilo, wingu lilifunga mawinguni na hatimaye mvua kubwa ilishuka huku burudani za ngoma za asili zikiendelea kuashiria kusherehekea yale yaliyohidiwa na mwekezaji, kabla ya ujenzi wa mgodi; kujenga ofisi na kulipa wananchi fidia.

Eneo ziliko ofisi hizo ni umbali wa kilomita 231 kutoka mjini Morogoro, ikiwa ni safari ya kuvuka miji midogo, vijiji vingi na barabara za lami na nyingine vumbi.

WAZIRI BITEKO

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri Biteko anaeleza namna alivyoguswa na mafanikio yaliyofanywa na kampuni hiyo, akisema: “Ningependa kutoa maoni yangu kwa nini mafanikio ya mradi huu ni muhimu Tanzania. Wachimbaji madini wana wajibu mkubwa kuendeleza rasilimali zilizopo chini ya ardhi na kuzifanya zilete tija kwa wadau.”

Kuhusu ofisi zilizozinduliwa, Waziri Biteko anasema ni ishara nzuri ya kampuni ya madini inayowajibika kwa umma.

“Ni kielelezo chema cha kampuni inayotimiza wajibu wake wa kurudisha manufaa ya mradi kwa wananchi yanayojulikana kama ‘Corporate Social Responsibility (CSR).”

Anadokeza kufahamishwa mradi wa Mahenge Resources utatumia reli ya Tazara kusafirisha bidhaa zao, kuanzia Ifakara hadi Bandari ya Dar es Salaam.

“Wananchi watapata ajira za kitaalamu na zisizo za kitaalamu, kupitia kufanya biashara na hivyo kupata fursa ya kuuza vitu mbalimbali katika mgodi huu,” anasema na kuendelea:

“Hii inamaanisha sehemu kubwa ya fedha zitokanazo na mgodi, zitabaki hapa hapa. Hili ndilo jambo la msingi zaidi kwenye sera yetu ya madini.”

Waziri Biteko anarejea tamko la tarehe 24 ya mwezi uliopita, Rais Dk. John Magufuli, aliposema: ““Tunahitaji mgawanyo sahihi wa mapato yatokanayo na uvunaji rasilimali zetu (win win situation)…Rais Magufuli ana maono kwamba sekta ya madini itakuwa inachangia asilimia 10 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2025.”

Kwa mujibu wa Biteko, kwamba ni jambo linalowezekana iwapo kutaendelezwa uanzishwaji migodi mipya mikubwa, ya kati na midogo na kufikia ndoto hiyo, ni budi sheria zilizopo zifuatwe.

Waziri Biteko anaeleza maono yake kwa mradi wa Mahenge Resources, kwamba utafungua njia kwa awamu hiyo mpya ya migodi mikubwa na kati nchini.

“Ninaamini kinywe au graphite itakuwa sehemu muhimu ya ujenzi huu wa mgodi mipya mikubwa. Hii itaifanya wilaya ya Ulanga na eneo hili la Mahenge litambulike kimataifa kama mzalishaji wa kinywe bora duniani.

Anasema hitaji la kinywe linaongezeka umuhimu na umaarufu wake, kwa sababu ya kutumika kutengenezaa betri na vifaa vingine vya kielektroniki.

“Simu zetu zote tulizo nazo zina graphite kwenye betri zake. Upatikanaji wake utazidi kuongezeka umuhimu kadri dunia inavyoendelea kuhamia kwenye teknolojia ya magari ya umeme, kwa lengo la kulinda mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo na moshi wa magari,” anaeleza, huku akifafanua nafasi ya sifa kurudi Mahenge.

Waziri anaeleza kuwa na taarifa za kampuni hiyo kuanza hatua za uthamini, fidia na uhamishaji makazi, akisema:“Nitoe rai kwa maofisa wa serikali wanaoshiriki mchakato huu kutoka katika ngazi zote, kuanzia taifa hadi ya kijiji, kushiriki kikamilifu.”

“Naiasa kampuni ya Mahenge Resources kuendelea kushirikiana na wananchi wa Mahenge katika kuwaletea maendeleo endelevu kutokana na kubarikiwa kuwa na madini haya,” anasema.

Kuhusu ofisi zilizozinduliwa, Waziri Biteko anasema: “Ni kielelezo chema cha kampuni inayotimiza wajibu wake wa kurudisha manufaa ya mradi kwa wananchi yanayojulikana kama ‘Corporate Social Responsibility (CSR)’ (uwajibikaji wa shirika kwea jamii).

KAMPUNI ILIKOANZIA

Anasema, kampuni hiyo kwa muda mrefu ilikuwa katika utafiti na kufikia hatua ya kuwekeza kwenye graphite ya Mahenge.

“Uwekezaji wao ni wa Dola za Marekani milioni 23 (Sh. bilioni 50.6) zitakazojenga mgodi huo wa Mahenge Resources. Changamoto waliyo nayo ni fidia kwa wananchi.

“Tayari tumeshawaelekeza waikamilishe haraka kabla ya uwekezaji, wameomba katika mchakato huu timu ya uthamini iwe na wawakilishi.

“Tayari nimemuelekeza Mkuu wa Wilaya wa hapa wawe na wawakilishi wa kijiji kwenye timu hiyo ili baadae kusitokee malalamiko.”

Waziri Biteko anasema kampuni imeshapewa sampuli mbalimbali za madini hayo ambazo walizipeleka katika maabara tofauti na wamejiridhisha, Kinywe ya Tanzania ni bora kuliko zinazopatikana maeneo mengine duniani.

MANENO YAO

Amina Juma mkazi wa Mahenge, anasema endapo kampuni zinazojishughulisha na shughuli ya uchimbaji wa madini zikifuata sheria za nchi, zitawawezesha wananchi kunufaika na miradi hiyo mikubwa.

“Tanzania tumebarikiwa madini ya aina mbalimbali, huku kwetu tuna madini ya Kinywe endapo wawekezaji hawa wanaokuja kuwekeza wakifuata sheria ninaamini sisi wananchi tutaondokana na umaskini,” anasema.

Joseph Peter anasema, mikataba ya madini iliyotiwa saini mbele ya Rais Dk. Magufuli kama wawekezaji wataitekeleza, itaongeza uchumi wa nchi wa wananchi nao hawatalia njaa.

Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Black Rock Mining, John de Vries, anasema imani yake ni kwamba, Tanzania itapata maendeleo makubwa katika sekta ya madini kupitia madini hayo ya Kinywe.

Aidha, anafafanua kuwa wajibu wao kama mwekezaji ni kuhakikisha wanarejesha manufaa kwa jamii.

“Tulipowauliza mlisema mnataka makazi bora zaidi, mlisema mnataka funguo, kuwapa funguo ndio dira yetu katika uthamini, hili ni deni letu na leo tumeanza kwa kutoa funguo za ofisi hizi,” anasema.

Anasema hadi sasa wamewaomba wanahisa wao na tayari wameshapata Dola za Marekani milioni 23 kwa ajili ya uwekezaji huo na kwamba wanahitaji kuwa na fedha nyingi zaidi kwa ajili ya fidia.

"Tupo katika hatua muhimu ya mchakato wa kujenga mgodi, tunawasiliana na benki zenye mitaji mikubwa ili tufanikishe hili na tuweze kukabidhi serikalini asilimia 16 kama mkataba wa madini unavyosema,” anasema.

Vries anasema kampuni hiyo imechukua tahadhari kubwa ili wasiahidi kitu ambacho baadaye washindwe kukitekeleza.

“Chochote tutakachoahidi tutakitekeleza, tunaamini hivi karibuni tutapata funguo kwa ajili ya mradi huu ikiwa ni pamoja na fidia zenu kwa wale watakaopisha uwekezaji huu,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya, anasema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii.

“Mwaka jana tulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 38, tulifanya harambee na kampuni hii ya Mahenge ilichangia Sh. Milioni 15, katika shughuli za Mwenge wa Uhuru walitoa sare za watoto wa alaiki zenye thamani ya Sh. Milioni 10 na leo wanatukabidhi ofisi za vijiji vitatu vinavyogusa maeneo yao ya uwekezaji,” anabainisha.

Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Goodluck Mlinga, alisema kampuni hiyo imetoa mchango mkubwa katika maeneo hayo na imekuwa ikishirikisha jamii.

Aidha, Mlinga aliwataka Tanesco kuhakikisha umeme unafika kwa wananchi ambao bado hawajapata nishati hiyo.

Kampuni ya Mahenge Resources itakapoanza uchimbaji inatarajia kuzalisha tani 80,000 kwa mwaka na uzalishaji huo baadae utafikia mpaka tani 250,000 kwa mwaka na utachangia Dola za Marekani milioni 100 (sawa na Sh. Bilioni 226).

Aprili 24, mwaka 2018, wananchi wa Mahenge, walishuhudia tani 500 zikisafirishwa kupitia usafiri wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara), katika stesheni iliyopo Ifakara, mzigo ukielekea Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuzisafirisha kwenda Canada.

Uzinduzi wa usafirishaji wa madini hayo ulifanywa na kampuni hiyo na ulifanyika viwanja vya stesheni ya Tazara, Ifakara ambao ulishuhudiwa na Ofisa Madini.

Uwepo wa Kinywe, unaifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa yanayozalisha kwa wingi madini hayo. Katika miradi hiyo mitatu mikubwa, ina uwezo wa kuzalisha jumla ya tani 240,000 kwa mwaka za madini hayo.

Mradi wa Namangale unaelezwa kuwa na uwezo wa kutoa tani 100,000 pamoja na Mahenge, ambayo ikikamilika na kuanza kufanya kazi, itaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa kuzalisha madini hayo duniani, ikitanguliwa na China inayozalisha zaidi ya tani 700,000 kwa mwaka.

Nchi ya India inashika nafasi ya tatu kwa kuzalisha tani 170,000 na Brazili nafasi ya nne ikizalisha tani 80,000, Canada, Korea Kusini na Uturuki wanazalisha tani 30,000. Zingine ni Russia inayozalisha tani 14,000, Mexico tani 8,000, Ukraine na Zimbabwe tani 6,000, Madagascar tani 5,000, Sri Lanka tani 4,000, Norway tani 2,000 na nchi nyingine zinazalisha tani 1,000.

Habari Kubwa