Wazazi, walezi wilayani Mbeya wanyooshewa kidole cha lawama

16Apr 2019
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Wazazi, walezi wilayani Mbeya wanyooshewa kidole cha lawama
  • Ni kwa kutowapatia wanafunzi wa kike mahitaji yao
  • Wakitaka wanafunzi hao wajinunulie wenyewe

WALIMU wa Shule ya Sekondari Nsongwe Juu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wamewalalamikia baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa Shule hiyo kwa kushindwa kuwapatia watoto wao wa kike mahitaji muhimu, zikiwamo nguo za ndani.

Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Shule ya Sekondari ya Nsongwe Juu Wilayani Mbeya, Elementia Mashazo (aliyesimama kushoto), akionyesha matumizi ya Pedi mbele kwa wanafunzi na Walimu.

Walimu hao wamedai kuwa asilimia 90 ya wanafunzi wa kike shuleni hapo hawavai nguo za ndani, jambo linalohatarisha afya zao, lakini pia linawafanya wasisome kwa utulivu pale wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi.

Mwalimu wa Afya shuleni hapo, Ramla Lui, anasema wazazi wengi wananunulia watoto wao mahitaji ya shule kwa maana ya darasani, lakini hawajali kuwanunulia mahitaji yao binafsi, hususan mavazi.

Anasema hali hiyo inaathiri mazingira ya watoto hao kusoma kwa utulivu na inawaweka katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya aina mbalimbali.

“Changamoto ya watoto wa kike kutovaa chupi tuliibaini baada ya binti wa kidato cha kwanza kuadhirika mbele ya darasa akiwa katika hedhi,” anasema na kuongeza:

“Sisi walimu wa kike tulifanya jitihada za kumsitiri lakini tukagundua hana utamaduni wa kuvaa chupi, na tulipomuuliza alisema mama yake alimshamwambia ajitegemee kwani ameshakua mtu mkubwa.”

WAANZA UKAGUZI

Mwalimu Ramla anasema walichukua uamuzi wa kuanzisha ukaguzi wa nguo za ndani kwa mabinti shuleni hapo baada ya tukio la binti huyo.

“Tulibaini wengi kutokuvaa chupi na hata kwa waliokuwa nazo baadhi hazikuwa katika hali ya ubora, tukatoa maagizo kwa wazazi kuhakikisha kila binti ananunuliwa nguo za ndani zisizopungua tano na taiti tano na pia wahakikishe wanaoga walau mara mbili kwa siku,” anasema na kuongeza:

“Wazazi wamekuwa mbali na watoto wao, hawawapatii elimu ya kujisitiri hasa pale wanapoanza kupata hedhi kutokana na kutokuwa na nguo za ndani na pedi.”

Anasema utaratibu wa kuwakagua watoto wa kike mara kwa mara umesaidia kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto hao, ikiwemo ya kubeba jukumu la kujitafutia mahitaji ya shule kwa kufanya vibarua.

“Tumeweka utaratibu wa kuwakagua watoto wa kike kila wiki… tumeona wengi wao hawavai chupi na badala
yake wanavaa kaptula ambazo ni kubwa,” anasema na kuongeza:

“Tulipobaini hali hii, tuliwaita wazazi ili kuwaeleza lakini mwitikio wake umekuwa mdogo, kwani wengi
hawajatekeleza maagizo tuliyowapa na badala yake wamewaachia watoto wajinunulie wenyewe nguo hizo,” anasema.

Mwalimu Ramla anabainisha kwamba baadhi ya wanafunzi wanasema kuwa wazazi wao hawana muda wa kuwa karibu nao kusikiliza au kujua mahitaji yao, badala yake wamejikita zaidi kwenye shughuli za uzalishaji kama vile kilimo.

WANAFUNZI WANENA

Elemetia Mashazo ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo.

Anasema wazazi wake hawajawahi kumnunulia nguo za ndani na badala yake hulazimika kufanya vibarau ili apate fedha za kujinunulia mahitaji yake hayo muhimu.

Anasema hulazimika kufanya vibarau kwasababu wazazi wake hawana utaratibu huo.

“Kwa mwaka huu tayari nimekwishajinunulia mwenyewe nguo za ndani, lakini hazitoshi…nitajitahidi kuongeza zingine ili kukidhi mahitaji kama walimu walivyoelekeza kuwa kila mwanafunzi wa kike awe na chupi tano na taiti tano,” anasema.

FAINES JACKSON

Kwa upande wake Faines Jackson ambaye ni Mwanafunzi wa Kidato cha tatu katika shule hiyo anasema wazazi wengi kwa sasa hawako karibu na watoto wao kwa sababu ya kujikita zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali na baadhi yao kuendekeza ukali.

Anasema upungufu huo upande wa wazazi husababisha binti kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na wanaume ili apate fedha za kukidhi mahitaji yake ikiwa ni pamoja na kununua nguo za ndani.

Aidha, Fainess ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Genda katika shule hiyo anazungumzia vilevile vitendo vya ukatili wa kingono vinavyowapata baadhi ya wanafunzi wa kike.

Anasema vitendo vya ukatili wa kingono bado ni changamoto kwa sababu vimesababisha baadhi ya wanafunzi wenzao kukatishwa masomo.

“Nina imani kupitia klabu hii tutaweza kupeana elimu vilevile ya masuala mbalimbali yakiwamo ya ukatili wa kijinsia, lakini pia kuungana pamoja kukemea vitendo hivi,” anasema.

OFISA ELIMU KATA

Ofisa Elimu Kata ya Ijombe, Ntabuli Mwakifuna, anasema utandawazi umesababisha wazazi kusahau wajibu wao wa kuwatimizia watoto wao wa kike mahitaji yao muhimu.

“Wanaamini kuwa kutokana na teknolojia binti akikua atajifunza mwenyewe namna ya kujihudumia na kujisitiri akiwa hedhi…matokeo yake ni kwa mabinti kushawishika na zawadi au fedha kutoka kwa wanaume ili waweze kupata fedha za kununulia nguo za ndani pamoja na pedi,” anasema na kuongeza:

“Naomba wadau na serikali tuendelee kuwaelimisha wazazi kuwatimizia mabinti mahitaji yao muhimu…hii itasaidia kupunguza majanga ya mimba za utotoni na ukatili wa kingono, hivyo kuwezesha watoto wetu kuzifikia ndoto zao.”

WAZAZI

Magreth Mwalizi ni Mkazi wa kijiji cha Nzongwe Mandaji.

Anakiri baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kuwanunulia mabinti zao nguo za ndani wakidai hawana fedha.

“Kwa upande wangu ninawajibika kumnunulia nguo cha ndani binti yangu lakini si kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na umaskini nilionao,” anasema.

Anabainisha kwamba anatambua umuhimu wa mtoto wa kike kununuliwa mahitaji yake lakini changamoto ni hali ya kipato hasa kwao wanaoishi maeneo ya vijijini.

Anachosema Magreth ndicho anachokibainisha Betina Anthony, Mkazi wa Kijiji cha Nzongwe Mandaji.

Anasema ni jukumu lake kama mama kumnunulia nguo za ndani mtoto wake, ila tu ukata wa fedha unaosababishwa na hali ya maisha umekuwa kikwazo cha kutimiza jukumu hilo licha ya kutamani kufanya hivyo.

KAMPENI YA ULINZI WA MTOTO

Kwenye siku ya Maadhimisho ya Wanawake Duniani, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), uliadhimisha siku hiyo kwa kutoa Elimu na kuzindua Kampeni ya Ulinzi wa Mtoto dhidi ya Ukatili wa kingono kwenye shule za Sekondari wilayani Mbeya.

Sababu ya kuzindua kampeni hiyo ni kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto, ambapo katika ripoti iliyotolewa Juni 2018 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonyesha kuwa wastani wa watoto 394 walibakwa kila mwezi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, anasema ripoti hiyo inaonyesha kuwa vitendo vya ulawiti kwa watoto vimeongezeka kutoka matukio 12 kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni 2017 hadi matukio 533 mwaka 2018 katika kipindi hicho.

Na mikoa inayoongoza kwa matukio hayo ni Dar es Salam na Iringa.

Lilian anasema kampeni hiyo inachangia jitihada za Serikali kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza vitendo hivyo kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kwa asilimia 50 ifikapo 2022.

Anasema jukumu la TGNP ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za ukatili wa kingono kwa watoto na umuhimu wa kuwalinda, kutathmini na kuibua mijadala katika jamii juu ya hali halisi ya vitendo hivyo.

“Kampeni hii imelenga kuwafikia watu wote kulingana na mazingira yao…jamii bado inawajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia… hii ni kwa mujibu wa sheria ya mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 na mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake,” anasema Lilian.

Anabainisha kuwa TGNP inaamini kila mtu atatimiza wajibu wake vizuri wa kumlinda mtoto na kwamba wanaitaka jamii kuchukua hatua za kumlinda mtoto popote alipo.

VITUO TAARIFA NA MAARIFA

Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilayani Mbeya, Flora Mlowezi, anasema vituo hivyo ambavyo vimejengewa uwezo na TGNP vimekuwa chachu kubwa ya kuleta mabadiliko katika jamii.

Anasema miongoni mwa mabadiliko wanayoendelea kuyafanya ni vita dhidi ya ukatili wa kingono kwa watoto hususani wa kike.

“Tumeamua kuanzisha kampeni hii ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya
vitendo vya ukatili,\’ anasema na kuongeza:

“Tuna imani itasaidia kuibua na kuripoti masuala hayo pindi yanapotokea na lengo letu ni kuhakikisha jamii inaguswa na tatizo la ukatili wa kingono dhidi ya watoto wakiwa ndani na nje ya shule.”

Habari Kubwa