Waziri atabasamu matumizi Sh. bilioni 9.2 Hospitali ya Wazazi Meta

22Jul 2021
Yasmine Protace
Mbeya
Nipashe
Waziri atabasamu matumizi Sh. bilioni 9.2 Hospitali ya Wazazi Meta
  • Hospitali Mkoa yaleyale; DC aishikia ‘bango’

MTU anapofika katika mikoa wa Mbeya, iwe katika zama za karibuni na simulizi ya zamani, kuna Hospitali kongwe ya wazazi ya Meta, jijini hapo.

Waziri Dorothy Gwajima. PICHA MTANDAO

Ina mengi imewatendea kinamama wa mkoa huo, kupitia huduma kwa kinamama, katika mwendelezo wa maboresho yake, hivi karibuni serikali imetoa  Sh. Bilioni 9.2 kukamilisha hitaji lililobakia, jengo la ghorofa sita mahsusi kumhudumia Mama na Mtoto.

Wakati jengo lililobakiza asilimia 85 na linatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amefanya ziara ya dharura kukagua maendeleo ya miradi ya afya inayoendelea mkoani humo.

Hospitalini Meta, Waziri Gwajima anakiri kufurahishwa na maendeleo hayo, akiamini upanuzi huo ni msaada kumhudumia mama na mtoto.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameshamalizia kutoa fedha zote na kufanya jumla ya Sh.bilioni 9.2 za ujenzi huu,” anasema na kuongeza: “Mradi utakapokamilika, idadi ya vitanda vitaongezeka kutoka 150 hadi 400.”

Dk. Gwajima anasema, ni jengo linalojitosheleza mahitaji likiwa na vitanda vya kujifungulia, vyumba vya upasuaji vinavyojitosheleza, matarajio ni kufunguliwa rasmi, Oktoba ijayo.

HOSPITALI MKOA

Pia, Waziri Gwajima, amekagua ujenzi wa wodi ya wahitaji wa upasuaji linalojengwa lenye vyumba sita, katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya.

“Jengo litakuwa na vitanda 82 vitakavyolaza watu waliofanyiwa upasuaji au wanaosubiri kufanyiwa upasuaji na hii ni hatua kubwa sana kuwa na vyumba vya upasuaji sita,” anasema Waziri Dk. Gwajima.

Anasema hadi sasa mamlaka ya mkoa yameshapewa Sh. bilioni tatu na wanakadiria kutumia Sh. bilioni 5.5 kumaliza ujenzi, hivyo anazitaka mamlaka mkoani kuharakisha hesabu wapatiwa fedha zilizobaki, lengo majengo yaanze kutumika mwaka huu.

“Nimefarijika kuona pia jengo la masuala yote yanayohusika na huduma za dharura kwa ufadhili wa Global Fund limekamilika." anaongeza.

HATUA ZINGINE

“Nimeona pia, mitambo ya oksijeni iliyounganishwa na mtambo wa kufua oksijeni ambayo imesimikwa kwenye hospitali saba za mikoa na bado tunasubiri hospitali nyingine 12.

“Huu ni ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wadau wake wakiwamo World Bank na Global Fund…Kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa ‘force account’ hata wakija wakiangalia watafurahi, wataleta zaidi ushirikiano wa misaada mbalimbali katika kuboresha huduma za sekta ya afya,” anapongeza.

BIMA AFYA

“Wateja wengi waje kisha muweze kunufaika na bima ya afya wanayotumia wengi kwa kuvutiwa na ubora wa huduma. Bima ya Afya sheria inakuja, Mungu akisaidia kuanzia mwakani hakutakuwapo mteja anayekuja wa msamaha.

“Kazi iliyobaki kwenu ni huduma nzuri kwa wateja na tabasamu, maana mtu mwenye hela yake anaweza kuamua kwenda zake asitumie huduma yako, iwapo haimridhishi hivyo utabaki huna wateja huku miundombinu unayo.

“Haya maslahi yetu tunayosema tunachelewa kulipwa tayari serikali imetuwekea mtaji wa miundombinu, vifaa na utaalamu tushindane kwa ubora wa huduma ‘marketing’ (masoko) ili tupate wateja wengi waliojiunga na bima za afya, hatimaye kusiwapo kuelemewa na misamaha.

“Wakija wengi kwa sababu wanapata huduma hapa, nanyi mtapata mapato mengi ya hospitali yatokanayo na mfuko wa bima na mkumbuke mna kamati zenu, bodi zenu, hivi atakayekuja kuwapangia ni nani, tabasamu lako hela yako, anzeni hizo sera.

DC CHUWA

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk.Chuwa Chuwa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, anamhakikishia Waziri Gwajima wanasimamia maelekezo yanayotolewa na mamlaka za juu kitaifa.

“Umeona na kukagua miradi ambayo ina karibu Sh. bilioni 14 ukijumlisha. Kwa kweli, ni miradi mikubwa tunaomba upeleke salamu kwa Mheshimiwa Rais, kazi yake aliyoifanya kwa Mkoa wa Mbeya ni kubwa sana na wana - Mbeya kiujumla wanaona namna anavyohangaikia afya zao.” anasema.

DK. Chuwa anasema, alishatoa maelekezo ya kufanyika kazi usiku na mchana alishaomba msimamizi kutoka Wakala wa Ujenzi nchini (TBA).

Habari Kubwa