Waziri azuru hifadhini Kilombero akimaliza msuguano na wananchi

15Jan 2021
Christina Haule
Kilombero
Nipashe
Waziri azuru hifadhini Kilombero akimaliza msuguano na wananchi
  • Asema wameshtukia hujumu hifadhini
  • Ruksa vijiji 41, ‘vigezo na masharti’ vyaja
  • Mbunge apiga debe uvuvi, nako akubaliwa

SERIKALI imeamua kumaliza mgogoro wa mipaka kwenye Bonde la Mto Kilombero uliodumu muda mrefu baina ya wananchi waliovamia Hifadhi na Mamlaka za Uhifadhi, huku mipaka hiyo ikiwa haina athari kwa wakazi wa vijiji 41 kati ya 42 vilivyopo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumaro, akiwa katika hadhara iliyowakusanya watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), anasema, wanavijiji 41 wataendelea kubaki kwenye bonde hilo, baada ya Rais John Magufuli kuwapa hisani hiyo.

Anasema, hivi karibuni kamati ya mawaziri wanane itawaita wakuu wa mikoa yote jirani kuwapa maelekezo ya mipaka ya vijiji hivyo 41 na wananchi watakaokuwapo, watatakiwa kuondoka kwa hiari kwenye bonde hilo, kwa maslahi ya taifa.

Dk. Ndumbaro amewaambia wanavijiji hao watakaobaki wafuate sheria za utunzaji vyanzo vya maji, ikiwamo kuacha kulima hadi watakapopatiwa mkataba wa mipaka mipya na miongozo ya kisera inayosisitiza maeneo ya kuendelea kuhifadhiwa.

Waziri Dk. Ndumbaro, anawataka wakazi kutambua mipaka ya bonde hilo iliyowekwa mwaka 1952 pori lilipoanzishwa na mabadiliko yake ya mwaka 1997 na mkataba mpya unaofanyiwa mchakato sasa.

“Mipaka hiyo ya zamani ipo na ilitolewa ikiwa na matangazo ya serikali, haijawahi kubadilishwa,” anasema.

Dk. Ndumbaro anasema, kinachoonekana kimatendo kwenye bonde hilo hadi kufikia uvamizi ni hujuma ya watu yenye athari kwa Mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere, zikiwamo kuwapa wanavijiji mbegu za mazao zinazonyonya maji mengi, jambo ambalo serikali imegundua na kuchukua hatua stahiki.

“Mtu yeyote anayehujumu mradi wa Mwalimu Nyerere kwa maneno na matendo atafikishwa mahakamani kupata anachostahili.

“Uhujumu uchumi ni kama mtu hutaki mradi wa umeme ufanikiwe wewe ni mhujumu uchumi, rushwa ni matendo ya watumishi na watendaji wa hifadhi kujipatia rushwa.

“Utakatishaji fedha ni kuzibadilisha fedha zinazopatikana kwenye mfumo usio rasmi, kuwa kwenye mfumo rasmi na ujangili ni vitendo vya rushwa na kufanya ‘sheshe’, viboko na tembo kuendelea kupungua kwenye bonde,” anasema Dk. Ndumbaro.

Anasema pori hilo tengefu linachangia asilimia 65 ya maji yote yanayoenda kwenye bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

KUPANDA CHEO

Ni katika tukio hilo, Waziri Dk. Ndumbaro, amempandisha cheo Ofisa Mhifadhi Daraja la Pili, Laurent Juma Okode, kuwa Ofisa Mhifadhi Daraja la I, kutokana na uaminifu wake, akitekeleza majukumu ya ya kazi akiwa Meneja wa Pori Tengefu la Kilombero.

Ni tukio lililoendana na kuwavua vyeo na kuwafuta kazi watumishi watatu, kutokana na madai na tuhuma za rushwa, kujihusisha na ujangili na utakatishaji fedha.

Anasema, mapato ya sekta utalii yanachangia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa, huku ikiingiza robo (asilimia 25) ya fedha za kigeni na lengo ya wizara ni kuongeza mapato yake maradufu.

Dk. Ndumbaro anasema, uvamizi katika pori la hifadhi kuchangiwa na uvamizi wa maeneo unaoendekezwa na viongozi wakuu kwenye wilaya husika, wanaotoa vibali vya vijiji, bila tathmini ya kina eneo hilo ni la mahitaji gani.

Anawataka wakuu wa wilaya hao kuwa makini kabla ya kuanzisha kijiji kipya katika maeneo yao, kwani inaweza kusababisha wananchi kuingia na kuishi kwenye maeneo ya muhimu na vyanzo vya maji na hifadhi za serikali.

Ni ufafanuzi unaoangukia mfano wa Bonde la Mto Kilombero, eneo linalotarajiwa kuingia kwenye mkataba wa kimataifa uitwao RAMPSA.

Rai ya waziri kwa wahifadhi nchini ni kwamba, walinde maeneo yao kisheria na wasiruhusu watu kuingia na kuharibu, ikiwa sehemu ya kuungana na jitihada za serikali zinazoendelea katika sekta hizo, akiitaja kuwa ni njia mojawapo ya kuitii sheria bila shuruti.

Dk. Ndumbaro anatambulisha sehemu ya adhabu kwa wakosaji kwamba kila ng’ombe atakayekutwa kwenye bonde hilo atalipa faini ya Sh. 300,000 na mmiliki atalazimika kulipa fidia ya uharibifu alioufanya mnyama baada ya tathmini kufanyika.

UVUVI RUKSA

Pia anawataka wanavijiji watakaobakia ndani ya bonde hilo, kuendeleza shughuli kama za uvuvi, wakifuata taratibu zitakazowekwa na TAWA, baada ya mipaka mipya kuwekwa.

Anasema kwa sasa TAWA wanajipanga kutengeneza soko la samaki kwenye maeneo hayo, ikiwa ni utekelezaji wa ombi la Mbunge wa Jimbo hilo, Abubakar Asenga, alilolitoa mbele ya waziri.

Wzairi Ndumbaro anasema, baada ya kuwekwa mpaka mipya, bonde hilo litakuwa na sehemu maalum ya kuegesha mitumbwi na wavuvi watapata nafasi ya eneo la kuvua na kwenda eneo la mauzo.

“Tatizo la wavuvi wengi wana tabia ya kuvua samaki, kulima na kujenga kandokando ya mto bila kujali uhai wa mto huo. Hayo hayaruhusiwi tena,” anasema Dk. Ndumbaro.

NAIBU WAZIRI & DC

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, anasema bonde hilo limo katika orodha ya maeneo yenye hadhi kimataifa, kuwa na ardhi oevu yenye kilomita za mraba 6,500 na linalohitaji kutunzwa sana, pasipo uharibifu wa aina yoyote.

Anawataka wananchi kuona umuhimu wa kuzingatia sheria zilizopo, kwa kuacha kuvamia na kuishi kwenye maeneo ya mapito ya wanyama (shoroba), hali inayobabisha matukio ya vifo na vitisho kwao, kutoka kwa wanyama wakali, hali inayoongezeka kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Ismail Mlawa, anaiomba wizara kutoa msimamo utakaozisaidia wilaya tatu za Ulanga, Kilombero na Malinyi, ukaoutumia kama dira ya kuendelea kusimamia bonde hilo.

Mlawa anasema, wamekuwa wakipigania kuhakikisha watu hawaingii ovyo kwenye bonde hilo na utatuzi wa migogoro hiyo ya muda mrefu, utakaosaidia kuzifanya wilaya hizo kuishi kwa amani.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzukwi, anawasisitizia wahifadhi waendelee kuzingatia kazi waliopewa kwa niaba ya Mungu.

Habari Kubwa