Waziri Elimu ajaye aanze na:

21Nov 2020
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Elimu ajaye aanze na:
  • *Kuwezesha walioelimika kujiajiri
  • *Vyuo vikuu kuwa vituo vya weledi

MOJA ya maeneo muhimu kufanyiwa kazi wakati wa muhula wa pili wa awamu ya tano ni kuondoa changamoto iliyopo leo kwa taasisi hasa vyuo   vikuu na vya kati kufunza wasomi ili waweze kujitegemea  na kulitegemeza taifa.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, akisalimiana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji Damian Lubuva, kabla ya kuwatunuku wahitimu vyeti vya shahada na stashahada.

Ni kwa sababu inavyooneka vinazalisha wahitumu tegemezi pengine wasio na hatma ili kumudu maisha yao.

Jukumu la Waziri wa Elimu ajaye ni kukabiliana na  uwezo mdogo wa  wanafunzi wa vyuo vikuu ambao  licha ya kuelimika wanashindwa  kujianzishia ajira zenye  tija kumudu maisha yao , badala yake wanategemea kuajiriwa.

 Baadhi wakizungukia maofisini kila leo kuulizia ajira wakiwa wamebeba vyeti kwenye bahasha za khaki ambazo zimechanika na kuchakaa ikiashiria kukata tamaa.

Wakati hayo yakitokea vyuo vikuu vinatamba kuwa vinaandaa wasomi wanaoweza kujiajiri, vikitamba na kutaja mipango na mikakati iliyopo lakini ukweli ni kwamba havijaweza kutimiza azma hiyo.

Waziri wa Elimu mtarajiwa na wataalamu wa masuala ya kazi wanachotakiwa sasa ni kufanyakazi na kuwezesha mipango na mikakati ya kuandaa wasomi kujiajiri na kuifanya hali hiyo iakisi ukweli kuwa Tanzania ni nchi ya uchumi wa kati kwa matendo.

Licha ya kuwapo maelezo kuwa vyuo vikuu vinawafundisha wanafunzi hao kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa ajira, hakujawa na jitihada za kutosha kufanikisha azma hiyo, hivyo Waziri wa Elimu ajaye, akumbuke hilo.

MIKAKATI MADHUBUTI

Pengine   kukosekana mikakati ya wanafunzi kujianzishia ajira binafsi, pia uhaba wa  kazi  na  taasisi za elimu ya juu kushindwa kutatua tatizo hilo  ni  ‘jipu’ linalovimba na kuongeza maumivu kila siku.

Kwa hiyo ni  wakati wa kuwa na mipango na mikakati ya kubadili sera na taratibu za kufundisha ili kuwaandalia wahitimu hatma na kuondokana na wimbi la kuzurura kusaka kazi kila uchao.

Ni nini kifanyike sasa? Ndilo swali la kila mmoja, hivyo wasomi, watunga sera, wataalamu wa ajira walijibu kwa kuanza na kupunguza  kubadilisha utaratibu wa kufundisha ili uangalie jinsi ya kuwaandaa  vijana kumudu maisha yao badala ya  kuangalia alama za kufaulu kama A na B au ‘sifuri.’

Utaratibu uende mbali kwa kuchambua uwezo wa mwanafunzi   kuchangia maendeleo yake ya  taifa kwa kuwafundisha ujasiriamali na kujitegemea kunakotokana na rasilimali zinazopatikana kupitia kozi wanazozisoma madarasani.

Iwapo mtazamo huo ukibadilika pengine utawezesha kuviingiza vipaumbele vya maendeleo kwenye  taaluma ambapo wanafunzi watafunzwa jinsi ya kutumia elimu walizopata kujiendeleza na kutatua matatizo ya jamii zao.

Pia rasilimali nyingi zilizoko nchini zitumike kupunguza tatizo la ajira kwa mfano kwenye migodi ya vito na dhahabu, mistu, wanyamapori , ardhi na maji.

Pia vyuo vikuu na vya kati viwe  mfano wa maeneo ya kuelimisha na kufunza vijana kujiajiri mfano   Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kinachotoa mafunzo ya kilimo  na ufugaji, sayansi na teknolojia vitafsiri elimu inayotolewa kwa matendo ili ibadilishe maisha  ya wahitimu wake, majirani wanaowazunguka chuo na hata Mkoa wa  Morogoro.

SUA inaweza kulenga kwenye kuwa na mashamba darasa na kituo cha umahiri wa masuala yanayoendana na   kilimo, uvuvi, ufugaji, uundaji wa zana za kilimo  na teknolojia za kilimo.

Ni wakati wa vyuo kuonyesha kwa vitendo na umahiri elimu inayotolewa inavyobadili maisha na kutengeneza ajira.  Ndiyo masuala ya shamba darasa liwe la mazao, teknolojia, ufugaji, kuchimba madini, uzalishaji viwandani na  miradi inayotumia matokeo ya utafiti unaofanywa na vyuo ili watu na wanafunzi kujifunza.

Vyuo kama Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU) kinaweza kuwa mfano na kioo cha kuitazama jamii na kuibadilisha kiuwekezaji kwa kuiwezesha kuigiza mifano ya miradi ya uwekezaji, ujasiriamali ubunifu wa biashara kwa kuona mifano inayosimamiwa na chuo hicho ili wanafunzi na jamii ijifunze.

KUJIFUNZA UKWELI

Awamu ya lala salama ya muhula wa pili wa awamu ya tano, ni wakati wa kuhakikisha kuwa ufundishaji unatoka nje ya vitabu, elimu za kinadharia, kukariri na mihadhara ambayo haiakisi uhalisia wa mambo.

Lakini pia  kujali alama za kufaulu  kwa kuangalia A, B+ mambo hayo yawekwe kando,

ufundishaji uende mbele  kutafsiri elimu zinazotolewa kwa kuzihusisha na rasilimali zilizopo na kuwafundisha wanafunzi ubunifu wa kuchanganya taaluma na mazingira yanayozunguka na rasilimali zilizopo ili waanzishe miradi na kumudu maisha yao.

Elimu ya juu isaidie wanafunzi kuona jinsi watakavyoweza kujiajiri wakitumia  rasilimali kwa mfano bahari, ardhi, madini, mifugo, mazao  kama viungo, maua na vivutia watalii kutengeneza kazi nyingi hata kuanzisha viwanda ili kubadili maisha yao.

KUSHIRIKISHA WADAU/UTAFITI

Si kila kinachosemwa na serikali  kuhusu elimu ya juu kiko sahihi. Wakuu wa vyuo, serikali  na wadau wengine wa taaluma, wajiri, masuala ya kazi na watafiti washirikiane kuibua  upungufu uliko vyuoni.

Vigogo wa vyuo waelezwe wanapokosea, iwe ni  kwenye kuandaa wasomi wa elimu ya juu ili waweze kuwapika wajitegemee na kutumikia taifa kwa kuajiri na kujiajiri.

Vyuo vya kati na  vikuu vinahitaji maoni ya wadau kwenye kutatua tatizo la ajira na kuinua  elimu hivyo kila mwaka wawe wakiandaa kongamano la wadau kupeana mikakati ya kuboresha taasisi za elimu hasa vyuo vya kati na vya elimu ya juu.

Serikali, vyuo na vyuo vikuu katika mazingira ya leo ya kusaka kazi ni kwamba havizalishi ajira vinapika wasomi na wataalamu ambao watachukuliwa na wanaotengeneza kazi  ambao ni `waajiri’ hivyo, wanapokutana wanapata fursa kueleza wanachofanya ili taasisi za elimu zijifunze.

Sekta binafsi na wawekezaji wanaeleza aina ya kazi walizonazo, mambo wanayotaka yazingatiwe kuboresha mahitaji yao kwenye kufundisha vyuoni,  serikali inataja mipango yake, wanafunzi na kila mmoja anabainisha atakavyosaidia mchakato akitaja fursa na ushauri utakaozingatiwa.

Ni mambo yanayotakiwa kufanyika kila mwaka ili kupunguza makali ya kukosekana ajira rasmi lakini pia wanafunzi kushindwa kujiajili na kuandaa mikakati ya ubunifu ya kuwawezesha zaidi kwenye elimu ya juu yenye manufaa.

UWEKEZAJI ELIMU   

Mafanikio ya uchumi yanayoleta maendeleo yanaanzia kwenye elimu ya juu hivyo, kufanikiwa elimu hiyo kutaboresha elimu ya msingi, afya, kilimo, siasa hivyo awamu ya tano iwekeze zaidi.

Habari Kubwa