Waziri Ummy na Mtafiti Repoa: Hivi ndivyo wasichana wanavyomalizwa

16Mar 2017
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Ummy na Mtafiti Repoa: Hivi ndivyo wasichana wanavyomalizwa
  • ‘Ndoa za utotoni ni kuweka afya mabiniti rehani’

LICHA ya sheria za kitaifa na kimataifa kukataza ndoa za utotoni, zimethibitisha kuwa tatizo sugu nchini linaloegemea katika utamaduni, mila na desturi za nchini.

Hali kadhalika, umasikini na ubaguzi vimeelezwa kuwa vyanzo vinavyoendelea kuchochea kitendo hicho ambacho kinaharibu maisha ya wasichana na kuzuia mafanikio ya jamii na nchi yao.

Mtafiti wa Taasisi ya Repoa, Dk. Lucas Katera, anasema utafiti aliofanya ni kuhusu ukubwa wa ndoa za utotoni, kuenea kwake, vichocheo na athari ambao ulifanyika nchini.

Utafiti huo ulifanywa mwaka jana na Sera ya Utafiti kwa Maendeleo, Repoa, kwa kushirikiana na taasisi za Children’s Dignity Forum (CDF), Foundation for Women Health Research and Development (FORWARD), Plan International na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA), pamoja na Plan International.

Dk. Katera anasema ndoa za utotoni ni suala la kuthamini haki ya wasichana na utafiti unaonyesha kwamba haki hizo kwa kawaida zinapuuzwa, matokeo yanayowaumiza wasichana zaidi waliko katika malezi.

“Ndoa za utotoni zinaathiri afya zao, elimu yao na fursa za ajira na mara nyingi kuwanyima kuzungumza chochote katika uendeshaji wa maisha yao wenyewe,” anasema.

Mtaaluma huyo anasema, ndoa za utotoni zina madhara makubwa kwa vizazi na jamii zilizoko katika mzunguko wa umaskini na vigumu kujinasua.

“Tunawaomba wote wenye mamlaka katika ngazi zote za jamii, kuanzia familia hadi serikalini, kutekeleza mapendekezo yaliyotokana na utafiti huu na kusaidia kukomesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao ni ndoa za utotoni,” anasisitiza.

Utafiti huo ambao umezingatia viashiria vilizokusanywa katika mikoa 10 yenye viwango vya juu, kati na viwango vya chini vya ndoa za utotoni.

Pia ilijumuisha viashiria kutoka kaya zenye washiriki wa utafiti 3,299, waliohojiwa umuhimu wa kina wa watoa taarifa wengine 199.

Hali kadhalika, inaelezwa taarifa zilichukuliwa kutoka kwenye mijadala 190.

“Kwa kuzingatia matokeo kutokana na uchunguzi wa utafiti asili, muhtasari wa ripoti unawasilisha sababu kuu za ndoa za utotoni, unachanganua ni wasichana wapi wanaathirika zaidi na ueneaji wake katika mikoa mbalimbali ya Tanzania,” anasema.

Matokeo ya utafiti

Dk. Katera anasema takwimu zitokanazo na Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) mwaka jana, zinaonyesha asilimia 36 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 20 na 24 waliolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Anasema kuwa ndoa za utotoni ni za kawaida vijijini, ingawa pia zinatokea mijini, kukiwa na tofauti kubwa baina ya mkoa mmoja na mwingine.

Ni taarifa zinazooonyesha kuwa mwaka 2010, mikoa iliyoongoza kwa mimba za utotoni ni Shinyanga ikiwa na asilimia 59; Tabora (58); Mara (55); na Dodoma asilimia 51.

Mkoa wa Iringa na Dar es Salaam zilikuwa na kati ya asilimia nane na 17.

Pigo la umaskini

Umaskini ulitajwa kuwa kichocheo kikuu cha ndoa za utotoni nchini, ambacho kina sura nyingi na zinatofautiana kati ya mikoa na makundi ya makabila.

Anasema kiuchumi, familia zenye maisha magumu mara nyingi zinapambana kutafuta chakula na mavazi kwa ajili ya watoto wao, mbali na dai la ada au gharama nyingine zinazohusiana na kuhakikisha watoto wanaendelea vyema na masomo.

“Matokeo yake, wengi wanaishia kuwaoza mabinti zao kama njia ya ‘kuwalinda’ kiuchumi na kijamii. Familia zinakuwa hazijapunguza mtu mmoja tu wa kumlisha, bali katika ndoa yake ‘mahari’ inalipwa kwa familia ya msichana na mara nyingi ng’ombe au fedha taslimu na mifugo,” anasema.

Mila na desturi

Katika baadhi ya maeneo, desturi na mila za utamaduni wa jamii na taratibu maalumu kwa makundi mahususi ya makabila, zilionekana kuchangia kushamiri ndoa za utotoni.

Dk. Katera anasema mila hizo zinajumuisha sherehe za matambiko, ngoma za kimila na ukeketaji wa wanawake.

“Shughuli hizo ambazo mara nyingi huwa na madhara, taratibu za kimila huwaingiza wasichana, wakati mwingine wakiwa wadogo wenye miaka tisa kuwa wanawake,” anasema.

Anafafanua zaidi akisema: “Wanakusudia kuhakikisha kwamba wasichana wako tayari kuolewa na kukubalika kama wake, mara taratibu hizo zinapokuwa zimefanyika. Mara nyingi haraka na kimya kimya hufuatiwa na ndoa,” anasema.

Anataja mikoa ya Mara, Manyara na Dodoma ina viwango vikubwa vya ukeketaji wa wanawake na ndoa za utotoni na maeneo mengine vitu hivyo viwili havitokei kwa wakati mmoja.

Ubaguzi wa kijinsia

Ubaguzi wa kijinsia ni kutokuwa sawa kijinsia na kutokuwa na uwiano wa madaraka unaowabagua wanawake na wasichana majumbani, kwenye taasisi na sheria inayowahusu na huishia katika ndoa za utotoni.

Anasema wasichana wanalelewa katika namna ambayo inawafundisha kuwa walezi, wakifanya shughuli za nyumbani zisizo na malipo.

“Matokeo yake wasichana hawana thamani ya kiuchumi inayotambulika kwenye kaya, zaidi ya mahari na elimu haichukuliwi kama kipaumbele kwao,” anasema.

Anafafanua kuwa wavulana kwa upande mwingine wanachukuliwa ni wawekezaji wa kiuchumi ambao baadaye wataisaidia familia kiuchumi.

Nafasi ya heshima

Dk. Katera anasema familia zina wasiwasi kwamba, sifa yao inaweza kuharibiwa, pia familia kuathirika kuhusiana na mimba za vijana balehe.

Anasema wazazi wana uwezo wa kuamua kuwaoza mabinti zao katika umri mdogo kwa sababu wanaweza kuona tabia ya mtoto wao sio nzuri.

“Kwa hiyo, wanaamini ni bora kumuoza ili angalau wapate ng’ombe, kuliko kusubiri apate mimba wakati akiwa nyumbani.,” anasema.

Madhara ya ndoa

Dk. Katera anasema ndoa za utotoni kwa wasichana mara nyingi wanaozwa kwa wanaume wenye umri wa utu uzima na katika mikoa yote nchini, zaidi ya asilimia 50 ya ndoa za utotoni inahusisha wanaume ambao ni wakubwa kwa umri wa kati ya miaka mitano 5 hadi 14.

“Ni muhimu kutambua kwamba ndoa za utotoni haziwaathiri tu wasichana wenyewe, pia zina madhara kwa familia, jamii na nchi kwa ujumla,” anasema.

“Wasichana wasio na elimu au ujuzi wa kitaalamu, nao wana uwezekano wa kubakia maskini na kuendeleza mzunguko wa umasikini, ambao unathiri maendeleo na mafanikio ya taifa kwa ujumla, sasa na baadaye,” anasisitiza.

Anataja lingine ni hatari za kiafya zinaongezeka kwa wasichana na familia zao, kwa kuwa upatikanaji huduma za afya na taarifa zinazohusiana nazo, chanzo chake si elimu ndogo, bali hadhi yao kijamii.

Dk. Katera anasema athari za ndoa za utotoni zinafika mbali kwa kupoteza fursa za maendeleo na kuongezeka kwa matatizo ya kiafya.

Waziri Ummy

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye ndiye mwenye dhamana na watoto, anasema ili kukabiliana na tatizo hilo nchini, serikali inanuia kufanyia marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ambayo inachangia ndoa na mimba za utotoni.

Ummy anasema utafiti unabaini kuwa, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ni miongoni mwa vigezo vya kushamiri ndoa za utotoni.

“Mimi nimeamua kujilipua. Nnasema wazi na siyo kama nakinzana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nasimamia sera ya maendeleo ya watoto, kwa hiyo nakiri hadharani na nitaendelea kukiri hadharani kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni kichocheo cha ndoa za utotoni,” anasema Waziri Ummy.

“Nitashirikiana na wenzangu wa serikali, ili kuhakikisha tunaifanyia marekebisho, ingekuwa ipo chini ya wizara yangu pekee, ningekuwa nimeshawasilisha mapendekezo ya marekebisho bali ipo pia chini ya Wizara ya Katiba na Sheria,” anafafanua.

Waziri Ummy anasema jukumu la serikali ni kuelimisha jamii kuwa mali na mahari za kuwaoza watoto hazitoshi kumaliza umasikini na kwamba ukeketaji na unyago unahamasisha ndoa na mimba za utotoni.

Rai yake kwa mashirika yanayoshughulika na watoto kwenda vijijini, ambako ndoa za utotoni zimeshamiri, ili kutoa elimu, badala ya kubaki mijini ambako hakuna matukio hayo.

Ummy anabainisha kuwa, ni wastani wa watoto 14 kati ya 100, wameanza ngono kabla ya miaka 18, hali ambayo inachochea ndoa za utotoni.

Pia, kuna watoto 36 kati ya 100, wanaoolewa chini ya umri wa miaka 18 kila mwaka.

Habari Kubwa