Waziri Ummy: Naumia kila siku kupoteza wanawake 24

01Sep 2016
Elizaberth Zaya
Dar es salaam
Nipashe
Waziri Ummy: Naumia kila siku kupoteza wanawake 24

PAMOJA na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kupigania kupunguza tatizo la vifo vinavyotokana na uzazi kwa wakina mama, bado hali hiyo inaendelea kuwatesa kinamama.

waziri wa afya, ummy mwalimu.

Tanzania ilianzisha Mpango Mkakati kwamba ifikapo mwaka 2025, huduma za uzazi salama utapatikana kwa kiwango kuridhisha, kuhakikisha kunapnguzwa vifo vya kinamama na watoto wachanga na wadogo, ambavyo vimekuwa vikitokea kila mara.

Hiyo ni mojawapo ya vipaumbele vya kusaidia kupunguza tatizo hilo, ikiwa na mtazamo wao kulimaliza kabisa.

Katika mkakati huo miongoni mwa vitu vilivyoanishwa ni kwa serikali kutoa kipaumbele, kuongeza na kuilinda bajeti ya Huduma Kamili za Dharura za Uzazi Salama(CEmONC), ili kuokoa maisha ya mama mjamzito na watoto wachanga.

Wakati uchumi wa Tanzania unatarajiwa kupanda kila mwaka hadi kufikia katika ufanikishaji malengo hayo, afya ya wananchi wake na nguvu kazi kutoka makundi mbalimbali inategemea zaidi kasi ya kukua uchumi.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mkakati wa Sekta ya Afya Awamu ya Tatu, kati ya mwaka na 2009 2015, Tanzania bado haijapiga hatua kubwa katika kuokoa vifo vya kinamama na watoto, kati ya mwaka 1990 na 2013.

Pamoja na kupungua kwa kasi ya vifo hivyo kufikia asilimia 47 ya kinamama na watoto wachanga wa miaka hiyo wanaojifungua, Tanzania haijapiga hatua za kutosha kufikia malengo ya Millennia Namba Tano.

Ni lengo linaloangaza katika ku punguza asilimia 5.5 kwa mwaka ya vifo vya kinamama na watoto kktaifa.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kutoka mwaka 1990 hadi 2013, Tanzania vifo vya kinamama viko katika wastani wa asilimia 3.5.

MTAZAMO WA UTEPE MWEUPE
Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe na Uzazi Salama, Rose Mlay, ambao ni miongoni mwa wadau muhimu katika mkakati huo, wa kukoa maisha ya kinamama na watoto, anasema takriban kila siku wanawake 24 hufariki kutokana na vifo hivyo.

Anasema takriban wanawake 8,000 hufariki kila mwaka kwa sababu ya matatizo yanatokanayo na mimba na uzazi.

Pia watoto wachanga 40,000 hufariki katika kipindi cha mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa na watoto 50,000 hufia tumboni mwa mama zao.

Katika idadi hiyo ya wanaofia tumboni, nusu hufa kabla ya kuzaliwa.

KWANINI VIFO?

Rose anataja sababu zinazochangia zaidi ya asilimia 70 ya vifo vya kinamama ni pamoja na kuvuja damu kwa wingi, kifafa cha mimba, maambukizi baada ya kujifungua, kutoa mimba na uchungu pingamizi.

Anasema mwaka 2012, matatizo ya kujifungua yalichangiwa kwa asilimia 63 ya vifo vya kinamama nchini.

Mratibu huyo wa Utepe Mweuoe anaasema kuwa, sababu hizo zote ni matatzo yanayozuilika, iwapo wahusika wangepatiwa huduma za dharura za uzazi salama za afya mahali waliko.

Anasema ukosefu wa huduma hizo, kunachangia kwa kiwango kikubwa vifo na kwamba utoaji wa huduma hizo kamili katika vituo, ikiwamo damu salama na upasuaji wa mjamzito wakati wa kujifungua hupatikana kwa asilimia 73 za hospitali nchini.

Pia, asilimia tisa za vituo vya afya, zina huduma za upasuasaji. Lengo halisi lilikuwa, ni asilimia 100 kwa hospitali zilizopo na asilimia 50 ya vituo vya afya vyote nchini.

Rose anasema vifo vya kinamama vinaweza kuathiri kipato cha nchi kwa sababu asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na takriban asilimia 98 ya wanawake vijijini, ndiyo wakulima wa mazao ya chakula na biashara.

Anasema kundi hilo la jamii ndilo liko katika tatizo la kutopata huduma bora za uzazi salama na ndiyo wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua.

“Iwapo wanawake wataendelea kufa, kutakuwa na pengo kubwa la wafanyakazi na nguvu kazi ya taifa. Hivyo, hata wazalishaji wa kiuchumi watapungua,”anasema Rose na kuongeza:

“Mama ana jukumu jukumu kubwa kama mlezi wa familia na jamii, anapofariki nafasi ya kiuchumi inaweza kupungua au kutoweka kabisa.

“Vifo vya kinamama vina athari kubwa katika familia, jamii na taifa kwa ujumla, kwa sababu ndiyo wanaowahudumia watoto, mume na wakati mwingine wazee.

“Wana nafasi kubwa katika makuzi, malezi, elimu ya watoto, hivyo anapofariki (mama), maana yake mwalimu anatoweka na wakati mwingine wanapofariki familia husambaratika.”

Rose anasema uzoefu wa Utepe Mweupe kupitia mkoa wa Rukwa, unaonyesha uwezekano wa serikali kutekeleza ahadi zake za kuhakikisha nusu ya vituo vya afya vinatoa huduma kamili za uzazi, iwapo kutatengwa bajeti ya kutosha kuhdumia hitaji hilo.

Anarejea mwaka 2013, wakati Utepe Mweupe ulianza kampeni ya masuala ya uzazi salama, hakukuwapo kituo cha afya hata kimoja kilichokuwa kinatoa huduma kamili za uzazi kati ya 10 vilivyokuwapo, huko Rukwa.

Rose anasema baada ya juhudi za ziada kufanywa na serikali za mitaa, wanasiasa, watoa huduma za afya na jamii kupiga kelele katika mkoa huo, vituo vitano kati ya hivyo vilianza kutoa huduma mwaka jana.

BAJETI NA UZAZI SALAMA

Mratibu wa Mradi wa Huduma Kamili za Dharura za Uzazi (CEmONC), ulio chini ya Muungano wa Utepe Mweupe, Sizarina Hamisi, anasema hadi sasa bajeti imekuwa ikitengwa na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni jumuishi.

Anasema kutengwa bajeti kuwa jumuishi, kunachangia ugumu wa kutatua tatizo la vifo vinavyotokana na uzazi.

Anaongeza:“Vituo vingi vya afya havina vifaa vingi muhimu vya uzazi, dawa na hata miundombinu yake siyo rafiki.

“Kwa hiyo, mwanamke anapohitaji kujifungua, baadhi yao wanafia njiani, kutokana na kucheleshwa kufika hospitalini kwa sababu ya ubovu wa miundombinu.

“Hata pale wanapofanikiwa kuwafikisha wanakuta vifaa vingine havipo, kwa maana hiyo uwezekano wa kujifungua salama unakuwa mdogo.”

Sizarina anashauri bajeti zijazo serikali, ziliangalie hilo kwa kuhakikisha kunatengwa fungu la kushughulikia masuala ya uzazi pekee.

Mratibu huyo anasema wamepanga kuonana na viongozi wa serikali kuu na serikali za mitaa, kujadili bajeti za afya, ili kuwekewe uzito katika maboresho ya huduma za uzazi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anakiri kwamba tatizo la vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi bado ni tatizo na kwamba serikali inafanya jitihada za kuhakikisha vinapungua kwa kuboresha huduma za uzazi salama.

Anaeleza masikitiko yake ya vifo vya wanawake 24 kila siku, kwamba si jambo jema na binafsi katika hadhi yake kama mwanamke, imekuwa ikimuumiza sana.

“Nikiri kwamba pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kupunguza vifo hivyo, bado hatujafanikiwa kufikia lengo.

“Idadi ya wanawake 24 wanafariki kila siku kwa sababu ya uzazi ni kubwa na mimi kama waziri na mwanamke, inaniumiza na niahidi kwamba lazima tulitafutie ufumbuzi,” anasema.

Waziri Ummy anatoa agizo kwamba, kwa vituo vyote vya afya nchini kuhakikisha kwamba, mwanamke mjamzito asitozwe gharama za vipimo na kumuona daktari wakati wowote.

Habari Kubwa