Waziri Wang Yi Afrika

13Jan 2021
Ani Jozen
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Wang Yi Afrika
  • *Ni kutanguliza agenda kabla Marekani kuzinduka
  • *Tanzania ya kwanza, ilianza 2013 na Rais Jinping

WAKATI Marekani inapata taabu kungoja Rais Donald Trump, amalize muda wake Jumatano ijayo, ili kuapishwa mteule Joseph Biden, tayari China imetanguliza agenda za kuafikiana na Afrika kabla utawala mpya wa haujaingia ikulu.

Tanzania inakuwa ya kwanza kupokea ujumbe huo wa China baada ya Waziri wa Mambo ya Nje, Wang Yi, wiki iliyopita kuanzia kazi Chato alipokutana na Rais John Magufuli, ukiwa ni mwanzo wa safari ya siku tano.

Wang Yi amekaa nchini siku mbili ikionyesha kuwa, alikuwa na upana zaidi wa mazungumzo na Rais John Magufuli kuliko taifa jingine.

Kwa miaka mingi inaeleweka kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza kwa uhusiano na China, ikiendana pengine na Zimbabwe.

Hata mwaka 2013 Rais wa China Xi Jinping, alizuru Tanzania likiwa ni taifa la kwanza tangu alipoapishwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

Rais John Magufuli, akizungumza kwenye mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, aliomba China iisamehe Tanzania madeni ya dola takribani dola milioni 167.7zilizokopwa kujenga reli ya TAZARA, kiwanda cha nguo cha Urafiki na nyumba za wanajeshi. 

Ni suala ambalo China haikulitolea maelezo, lakini Waziri Yi, alilipokea.

Aidha, China imekubali kusaidia ukamilishaji wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR ulioafikiwa kwa kujenga kipande kinachoanzia Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga chenye urefu wa kilomita 341.

Baada ya Tanzania Waziri Yi aliendelea na safari kuelekea Seashells, Nigeria, Botswana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

AJENDA YA CHINA

Itachukua miezi kadhaa kwa serikali mpya Washington kujipanga na kuanzisha sera zinazoeleweka, ingawa sasa kuna picha kuwa Biden atakuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyotazamiwa hapo awali. 

Ni baada ya Chama cha Democratic cha Biden kushinda uchaguzi wa viti vya Senate Jimbo la Georgia ambako wakati wa uchaguzi mkuu wa Novemba hakuna aliyefikia asilimia 50, kati yake na Donald Trump.

Yako maeneo ambayo China inaweza kuhitaji kufahamu, kwa mfano kuanza kutumika kwa Mkataba wa Soko Huria Afrika (CAFTA) ambao umeanza rasmi kutumika Januari mosi baada ya nchi 33 kuupitisha bungeni.

Tanzania ilitia saini, lakini bado ulikuwa haujaingia katika sheria, ila unaweza kuwa wa manufaa kwa China katika uendelezaji wa ule mkakati wa ‘belt and road,’ (ukanda na barabara) yaani kwa uwekezaji na uuzaji wa bidhaa zake.

Kwa upande wa China mkwamo wa kisiasa Marekani kuna faidi kwani sura ya Marekani nchi za nje imekuwa na mkanganyiko wa Rais Trump kuwahamisha wafuasi wake kushambulia bunge na kuua polisi.

Rais mteule wa Marekani alisema katika hotuba kuhusu tukio hilo kuwa ingekuwa ni maandamano ya ‘Black Lives Matter,’ yamefikia hatua ya kuvuruga kinachoendelea bungeni, kujaribu kuzuia kumthibitisha rais mteule kuwa ameshinda uchaguzi mkuu, ‘wangepata taabu sana.’

Lakini kwa vile ilikuwa ni kundi kubwa la weupe (Wazungu) wanaoapa kwa jina la Trump polisi hawakufanya linalotakiwa, walikuwa wachache na mmoja akapoteza maisha.

Ni jambo ambalo limevuruga sura ya Marekani mbele ya dunia na itachukua muda kiasi kwa serikali mpya kuingia madarakani na kila kitu kionekane kinaenda sawa dunia ianze kuisikiliza Marekani.

Ni kawaida katika uhusiano wa nchi za nje kuwa kiwango cha umoja ndani ya nchi kina athari kubwa katika uwezo wa kuendesha siasa au uhusiano na nchi za nje.

Pale ambako kuna mianya ya wazi katika utii kwa utawala uliopo madarakani, nchi kama hiyo haiwezi kuendesha uhusiano wa nje kwa urahisi, kwani nchi nyingine (serikali zao) hazitaamini au kutilia maanani serikali hiyo iliyoko mashakani inachoongea.

Kwa mfano Ijumaa iliyopita, asubuhi kwa saa za Marekani, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi, aliongeza na mkuu wa majeshi wa Marekani, kuhofia Trump,’ akatoa amri ya kushambulia mahali fulani, hata kutumia bomu la nuklia.
Taarifa zilisema Spika hakujibiwa.

ZIARA YA WANG YI

Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China haikufuatana na mkasa huo jijini Washington, lakini ni wazi ungechangia hoja za Wang Yi kwa nchi za Afrika kuwa China ni nchi thabiti yenye sera zinazoeleweka inayoweza kufanya mikataba ya muda mrefu na Afrika kuliko taifa jingine.

Marekani, kwa upande wa pili, hivi sasa imegubikwa na sintofahamu ya kuwa na pande mbili za kisiasa zinazohasimiana, na hivyo kujiweka njia panda ikingoja lini utawala uliopo madarakani utaisha, uingie mwingine, tofauti na uliotangulia.

Wakati Rais Barack Obama alitaka ‘mabadiliko,’ Trump aliingia kama kinyume cha Obama na sasa Biden kama kinyume cha Trump.

Pia kuna uhusiano kwa kiasi fulani kati ya mahitaji ya China kwa nchi za Afrika hivi sasa na historia ya uhusiano ya pande hizi mbili, kuwa Afrika ilikuwa ndiyo kundi kubwa zaidi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutaka China ichukue nafasi ya Taiwan, kisiwa kinachojitawala, lakini kwa jadi ni sehemu ya China.

KUIPINGA CHINA

Utawala wa Trump umejitahidi kuitenga China katika maeneo tofauti ya kibiashara na hasa matumizi ya teknolojia au vifaa vya kisasa vya mawasiliano kutoka China (5G) vya kampuni ya Huawei, ukisema kampuni hiyo ina uhusiano wa karibu na Jeshi la China na inaweza kuitumia kijasusi.

Ni eneo ambalo Trump alishindwa kuwaridhisha kihoja hata washirika wake wa karibu zaidi, nchi za Ulaya.

Maeneo ya ushindani kati ya Marekani na China kibiashara barani Afrika yanapungua au labda hayapo kwani ni kampuni chache za Marekani zinafanya biashara kubwa na hata kwingineko Afrika siyo kampuni nyingi. 

Ila Marekani ni kitovu cha biashara ya fedha duniani na kila nchi, hata China inategemea soko la hisa na fedha la Marekani iinue mikopo kutumia katika ustawishaji wa viwanda au teknolojia.

Inatazamiwa kuwa kampuni za China zilizoondolewa katika soko la mitaji New York zinaweza kurudishwa kama sehemu ya kupangua sera za Trump.

Habari Kubwa