Wazo la NCCR-Mageuzi laweza kumaliza mvutano huu

13Nov 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wazo la NCCR-Mageuzi laweza kumaliza mvutano huu
  • *Ni wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa

CHAMA cha upinzani cha NCCR-Mageuzi, kimejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kufuatia majina ya wagombea wake kukatwa.

Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, James Mbatia.PICHA: MTANDAO

Pamoja na kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho, mwenyekiti wa chama taifa, James Mbatia, anaviomba vyama vya upinzani nchini kutafuta njia ya maridhiano na serikali ili kuendelea kuilinda amani ya nchi.

Ndivyo kiongozi huyo alivyokaririwa na vyombo vya habari jijini Dodoma akisema hayo wakati akitangaza chama chake kujiondoa, kwamba katika majina 35,567 waliyopitishwa na chama hicho, yaliyorejeshwa ni 149.

“Jambo hilo halikubaliki, hivyo tumeamua kujitoa katika kinyang'anyiro hicho. Baada ya kufanya kikao cha Kamati Kuu tumeagiza wagombea wetu wajitoe na wadhamini, waliowadhamini ambayo ni matawi, tumeagiza waondoe udhamini au wagombea wajiondoe wenyewe, anasema Mbatia.

Mwenyekiti huyo anaongeza kusema: “Sisi hatushiriki uchaguzi huu wanatakiwa kufuata kanuni, hatuwezi tukaliacha Taifa linapelekwa ovyo, hii ni hatari sana,” anasema.

Ingawa kiongozi huyo anasema mengi, lakini kubwa ambalo naamini ni muhimu lizingatiwe na wanasiasa wote ni kutafuta njia ya maridhiano na serikali ili kuendelea kulinda amani ya nchi.

Hii inatokana na ukweli kwamba jamii tulivu na yenye amani ni muhimu katika kufanikisha shughuli za maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, hivyo amani haina budi kulindwa na watu wote.

Mvutano ambao umejitokeza baada ya serikali kuamuru wagombea wa upinzani waliokatwa majina warudishwe kwenye kinyang'anyiro ni wazi kwamba kuna haja ya kutafuta njia ya maridhiano.

Kinachoendelea sasa hakiwezi kulifikisha taifa pazuri, bali ni kukaa meza moja ya mazungumzo ili kila upande utoe dukuduku na hatimaye kufikia muafaka na kisha kuendelea na mchakato wa uchaguzi.

MAAGIZO YA TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, anawaagiza wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wagombea wote walioteuliwa na kudhaminiwa na kufanikiwa kurejesha fomu zao za uteuzi kwa wasimamizi wasaidizi wanaoshiriki katika uchaguzi huo.

“Hapa hakuna mtu kukimbia kwenye ‘cage’ (ulingo), hakuna mtu kuweka mpira kwapani, wote waliochukua fomu na kurejesha fomu wataenda kushiriki uchaguzi Novemba 24, mwaka huu, kama wamezoea kukimbia safari hii hakuna kukimbia,” anasema Jafo.

Anasema, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za serikali za mitaa, Tangazo la Serikali namba 371 na kanuni ya 49, wagombea wote walioteuliwa na kudhaminiwa na vyama vyao na kufanikiwa kurejesha fomu zao za uteuzi kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika kipindi kilichokuwa kimepangwa cha kuchukua na kurejesha fomu, wanapewa sifa ya kupigiwa kura na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Lakini pia anawataja wagombea, ambao hawatashiriki katika uchaguzi huo ni wale waliobainika kuwa na makosa yakiwamo ya kutokuwa raia wa Tanzania, kujidhamini wenyewe, kujiandikisha mara mbili, wasiodhaminiwa na vyama vyao vya siasa na kurejesha fomu watu zaidi ya mmoja kutoka chama kimoja.

"Vyama vya siasa ndiyo vilivyojitoa katika uchaguzi huo na siyo wagombea," anasema bila kutoa ufafanuzi kutokana na sheria ya sasa nchini kutoruhusu wagombea binafsi na inaelekeza wagombea wote wa nafasi za uongozi wa kisiasa kupitia vyama vya siasa.

MSIMAMO WA BAADHI YA VYAMA

Maagizo ya Jafo yanapingwa na vyama vya upinzani huku vingine vikiweka masharti ndipo vishiriki katika uchaguzi huo, vinginevyo vitaendelea kukaa pembeni vikishuhudia kinachoendelea.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinasema, wasimamizi wa uchaguzi huo wameshapoteza uhalali wa kusimamia uchaguzi huo kwa kuwaengua wagombea bila sababu za msingi.

Kinataka uchaguzi usimamiwe na watu huru ili mchakato uwe huru, kwamba takwimu za CCM kupita bila kupingwa siyo halali na kudai kuwa kama waziri Jafo angekuwa na nia njema asingetangaza kuwa CCM imepita bila kupingwa wakati anajua kuna waliozuiliwa bila sababu.

Ndivyo alivyokaririwa na vyombo vya habari akisema, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika na kupiga marufuku nembo ya chama hicho kutumika katika uchaguzi huo.

Wakati Chadema ikisema hayo, Chama cha ACT-Wazalendo nacho kimesema hakiwezi kuhalalisha uharamu kwa kuwa mchakato wote, katika hatua zote za kuchukua na kurejesha fomu ziliathiriwa na ofisi za wasimamizi kufungwa wiki nzima.

Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, anakaririwa na vyombo vya habari akisema:

“Hatuwezi kuingia kwenye mtego aliotuwekea, mchakato uanze upya, iundwe kamati huru yenye uwakilishi wa vyama vyote, mchakato wa kuchukua kurejesha uanze upya ili uchaguzi ufanyike katika mazingira ya kuaminiana, amani na uhakika,” anasema Zitto.

Zitto anasema, uhalisia ni kuwa wagombea watashiriki uchaguzi, lakini wasimamizi watawatangaza watu waliowaacha kwenye mchakato wa awali, hivyo hataki chama chake kishiriki uchaguzi huo.

“Kama waliweza kufuta watu bila sababu za msingi, basi hawashindwi kuwatangaza waliowaacha awali kama washindi. Walisema wagombea wa upinzani wameshindwa kujaza fomu, sasa fomu walizonazo zimerekebishwa saa ngapi?” Anahoji.

Kimsingi kila chama kina haki ya kuelezea msimamo wake, lakini jambo la muhimu hapa ni kuweka mbele maslahi ya taifa, siyo ya vyama vya siasa kwa ajili ya kulinda amani.

Suala la kukaa pamoja ili kumaliza mvutano huo limesemwa na Mbatia wakati akitangaza chama chake kujitoa, akiviomba vyama vya upinzani nchini kutafuta njia ya maridhiano na serikali, ili kuendelea kuilinda amani ya nchi.

Vilevile ni muhimu kutambua kuwa nyumba inayojengwa ni moja, ambayo ni Tanzania, hivyo hakuna haja ya kugombea fito, badala yake ni kukaa meza moja kwa ajili ya maridhiano, kwani penye wengi hapaharibiki neno.

Habari Kubwa