Wenye ulemavu Shinyanga kumekucha mkopo wa Manispaa wawapaisha

04May 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wenye ulemavu Shinyanga kumekucha mkopo wa Manispaa wawapaisha

SERA ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, inauelezea ulemavu kuwa ni changamoto aliyonayo mtu kwenye viungo au kiakili. Anaweza kuzaliwa nayo, kuipata kwa kuugua au kutokana na ajali, kwa hiyo mtu yeyote ni mlemavu mtarajiwa.

Mmoja wa wanachama wa kiwanda cha kutengeneza viatu akiwa kazini. PICHA: MARCO MADUH.

Hata hivyo, ulemavu si kushindwa maisha kwa vile tiba yake ni kupata vifaa visaidizi na kuwezeshwa iwe kimtaji, teknolojia, elimu au kimiundombinu hatua inayowawezesha wanaoishi na ulemavu kujikwamua na kumudu maisha yao.

Ndivyo wanavyothibitisha wana kikundi cha Mapambano na Ufundi cha wanaoishi na ulemavu cha Manispaa ya Shinyanga, wanaojihusisha na kutengeneza viatu.

Hawa ni miongoni wa wanufaika na mikopo ya halmashauri ambao wanapata asilimia mbili, wakati kinamama na vijana wanapata asilimia nne kila kundi.

Wana Mapambano mwaka jana walinufaika na mkopo wa Shilingi milioni 10.2 na kufungua kiwanda kidogo cha kutengeneza viatu vya ngozi.

Mweka hazina wa kikundi hicho John Samweli, akizungumza na Nipashe kwa niaba ya mwenyekiti wake, anasema awali kabla ya kupata mkopo huo, maisha yao yalikuwa magumu na walikuwa wakiishi kwa kushona viatu vilivyochanika na kupata pesa kidogo isiyokidhi mahitaji yao.

Anasema baada ya kusikia kuna pesa za mikopo asilimia mbili kwenye halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ndipo wakajiunga kwenye kikundi cha watu watano na kuanzisha mradi wa kutengeneza viatu.

Walinufaika na mkopo huo wa halmashauri na wamefungua kiwanda hicho cha viatu vya ngozi.

Anasema: “Tunaishukuru serikali kwa kututambua wenye ulemavu na kuanza kutupatia mikopo sababu tutakuwa tumesahaulika na kuonekana ni watu wa kupewa misaada wakati tuna uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kujipatia mapato. Kikubwa kinachopaswa ni kuwekewa miundombinu rafiki na kuwezeshwa.”

“Ukiangalia sisi maisha yetu yamebadilika na siyo tegemezi wala watu wa kuomba msaada, bali tuna uwezo wa kiuchumi na tunahudumia familia zetu, hivyo tunaiomba serikali iendelee kuwajali zaidi wanaoishi na ulemavu na kuwapatia mikopo ili tujikwamue kiuchumi,” anaongeza Samweli.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu mkoani Shinyanga (SHIVYAWATA) Richard Mpongo, anasema fedha za mikopo za halmashauri zimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake na kuwainua kiuchumi.

Anasema baadhi ya watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, lakini kilichokuwa kikiwakwamisha ni ukosefu wa mitaji pamoja na elimu ya ujasiriamali, na baada ya kuanza kupatiwa vitu hivyo wengi wanajishughulisha na biashara mbalimbali na kujipatia kipato.

“Tunaishukuru serikali kwa mpango wake wa kutoa fedha za mikopo kwa wenye ulemavu, ambazo zimetukomboa kiuchumi, mfano Halmashauri ya Ushetu imetoa fedha kwa vikundi vitatu, Msalala vitatu, Kahama Manispaa 12, Shinyanga Manispaa Sita, Kishapu na Shinyanga Vijiji kikundi kimoja kimoja,” anasema Mpongo.

Anawaomba maofisa maendeleo wa halmashauri waendelee kutoa elimu hiyo ya mikopo na ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu, kwa sababu wengi hawana uelewa ili kuwasaidia kujua namna ya kujikwamua kiuchumi na kuendesha maisha yao bila ya kutegemea misaada, anaongeza Mpongo.

Joseph Masota, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, anasema watu wenye ulemavu baadhi yao wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, lakini kutokana mitazamo potofu iliyojengeka ndani ya jamii kuwa wao ni tegemezi na hawana uwezo wa kufanyakazi, wamekoseshwa fursa na kuishi maisha magumu.

Anaitaka jamii kuelimika na kubadilika kuwa watu wenye ulemavu ni kama binadamu wengine, hivyo wapewe fursa mbalimbali ambazo zitawafaya kujiongizia kipato na kuacha kuwa tegemezi au kuomba misaada, sababu wengine wana uwezo mkubwa.

“Tumeshuhudia baadhi ya watu wenye ulemavu ambao wamewezeshwa, namna wanavyofanya kazi ya kujiingizia kipato, na hili jambo lingeanza toka zamani la utoaji mikopo, wange kuwa mbali sana na wala tusingeweza kuona omba omba mitaani,” anaongeza Masota.

Ofisa Vijana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Charles Ruchagula, anasema fedha za mikopo za halmashauri asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu, walianza rasmi kuzitoa mwaka 2019 baada ya serikali kutoa mwongozo.

Ilielekeza kuwa asilimia 10 za vijana na wanawake zigawanywe pia kwa walemavu kwa kupewa asilimia mbili.

Anasema tangu mwaka huo 2019 mpaka mwaka jana, wameshatoa fedha za mikopo kwa watu wenye ulemavu kwa vikundi sita na kutoa jumla ya Sh. milioni 21.1 na wamekuwa wakiwatembelea ili kuona maendeleo yao, na wanafanya vizuri na kubainisha kuwa mwaka huu watatoa tena fedha hizo za mikopo.

Anawataka wenye ulemavu, kujitokeza kwa wingi kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, pamoja na kubuni mawazo bora ya kibiashara ambayo yatavutia mikopo na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuacha kuishi maisha magumu.

Habari Kubwa