WHO: Uchafuzi mazingira unaua robo milioni ya watoto duniani

14Sep 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
WHO: Uchafuzi mazingira unaua robo milioni ya watoto duniani

MOJA ya mada za motomoto katika uga wa kimataifa kwa sasa ni ile ya mabadiliko ya tabianchi.

Mada hii imepewa kipaumbele katika ngazi zote za kiutawala miongoni mwa mataifa yaliyoendelea, na yanayoendelea kuwa ni mojawapo ya suala lenye uzito stahiki kwenye mikono ya Umoja wa Mataifa (UN).

Hii ni kwa sababu, madhara yake yameanza kujitokeza katika sura mbalimbali kuanzia kwenye mafuriko, ukame, matetemeko ya nchi, maporomoko ya udongo na kupungua au kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, na hivyo kusababisha matatizo makubwa kwa binadamu.

Pengine katika kulieleza hili ili liweze kufahamika vyema, matatizo ya njaa na mafuriko yaliyokumba baadhi ya maeneo nchini, kimsingi yanaelezewa kutokana na janga hilo la mabadiliko ya tabianchi.

Mojawapo ya sababu kubwa za mabadiliko ya tabianchi ni shughuli za kibinadamu kama vile ukataji wa miti unaoendelea kwa kasi kubwa, uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwanda na magari, uchafuzi wa mazingira na mengi mengineo.

Hayo yote kimsingi yana madhara yake na miongoni mwake ni magonjwa mbalimbali yanayokumba afya za watu.

Matokeo ya Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), umebainisha kuwa, hewa yenye sumu, maji yasiyo salama na mazingira duni ndiyo chanzo cha vifo vya watoto milioni 1.7, wenye umri chini ya miaka mitano, kila mwaka duniani.

WHO imesema kwamba, uchafuzi wa mazingira unasababisha kifo kimoja kati ya vifo vinne vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kila mwaka, huku hewa yenye sumu, maji yasiyo salama na mazingira duni ya makazi kwa watu yakitajwa kuwa sababu kubwa ya vifo hivyo.

Hata hivyo, ripoti ya shirika hilo inaonyesha kuwa, pamoja na mazingira yaliyochafuliwa kusababisha idadi hiyo ya vifo kila mwaka, lakini vifo vingi kati yake vinaweza kuzuiwa ikiwa hatua zilizothibitishwa kuwa na matokeo mazuri zitatumika.

Mfano wa hatua hizo ni ile ya kutumia majiko yasiyosababisha uchafuzi wa mazingira.

“Mazingira yaliyochafuliwa ni hatari sana, hasa kwa watoto,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Margaret Chan na kuongeza

“Hiyo inatokana na ukweli kwamba, ukuaji wa viungo vya watoto na mifumo ya kinga pamoja na miili yao midogo, ikiwa na njia zao za hewa zinawaweka katika hali ya kuathiriwa zaidi na hewa chafu na maji.”

WHO inasema, balaa dhidi ya hewa chafu linaweza kuanza toka wakati wa ujauzito, kwa sababu linaongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti.

Dk. Chan anasema, baada ya mtoto kuzaliwa, hewa chafu tunayoivuta huongeza hatari kwa mtoto kushambuliwa na ugonjwa wa Nimonia (Pneumonia), ambao ndio chanzo kikuu cha vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Anasema, hata kwa watoto waliovuka umri wa miaka mitano, hewa chafu husababisha magonjwa ya muda mrefu na hasa yanayoshambulia mapafu, kama vile pumu.

Aidha Dk. Chana anasema, hali hiyo inaweza vilevile kumuweka mtu katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya moyo, kiharusi na saratani katika siku za uzee wake.

UPANA WAKE
Ripoti hiyo imewasilisha kwa mapana, mapitio ya madhara ya kiafya yatokanayo na mazingira duni.

Inafafanua kwamba, watoto 570,000 chini ya umri wa miaka mitano duniani wanakufa kila mwaka kutokana na magonjwa ya maambukizi kwenye mfumo wa hewa kama vile nimonia.

Aidha inafafanua, watoto wengine 361,000 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kuharisha, sababu kuu ikiwa ni maji machafu na mazingira duni.

WHO inakadiria kwamba, asilimia 11 hadi 14 ya watoto wenye umri wa miaka mitano na zaidi kwa sasa wamekuwa wakiripoti kukumbwa na dalili za ugonjwa wa pumu, huku nusu ya dalili hizo zikihusishwa na uchafuzi wa hewa.

Ripoti hiyo inapendekeza kwamba, viwango vya joto kali na hewa ukaa vinavyohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi, vinaweza kuongeza viwango vya chavua na kuufanya ugonjwa wa pumu kuwa mbaya zaidi.

“Kuwekeza katika miradi ya kuondoa hatari za kimazingira kutakuwa na manufaa makubwa,” anasema Dk. Maria Neira, Mkurugenzi wa Mazingira na Vigezo vya Afya ya Kijamii, kutoka WHO.

Anatoa mfano wa hatua kama za kushughulikia taka za umeme, kutapunguza hatari ya kuwaweka watoto kwenye madhara ya sumu hizo ambazo husababisha uwezo mdogo kiakili na ugonjwa wa saratani.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef), lilikuja na makadirio yanayowakabili watoto wanapowekwa katika mazingira yenye hewa chafu na kukuta kwamba, karibu asilimia 90, kwa maana ya watoto bilioni mbili wanaishi kwenye maeneo ambayo uchafu wa hewa unazidi kiwango cha mwisho kilichowekwa na WHO.

Unicef ilibaini kuwa, watoto milioni 300 kati ya hao bilioni mbili wanaishi katika mazingira yaliyo na kiwango kikubwa cha uchafuzi wa hewa, ambako mvuke wa sumu unaoingia hewani ni zaidi ya mara sita ya maelekezo ya kiafya.

WHO ilitangaza mwezi Mei, mwaka jana kuwa, uchafuzi wa hewa duniani unaongezeka katika kiwango cha kutisha, huku karibu majiji yote katika mataifa yanayoendelea yanakumbwa na tatizo hilo, kama ilivyo kwa nusu ya majiji katika nchi tajiri.

Utafiti uliofanyika mwaka 2015 ulibanisha kwamba, zaidi ya watu milioni tatu hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa, idadi ikiwa ni zaidi vya vifo vinavyosababishwa na Malaria na Ukimwi, kwa pamoja.

Dk. Chana anahitimisha kwamba uchafuzi wa hewa ni moja ya vitisho hatari vinavyoikabili afya ya binadamu kwa sasa, na uko katika viwango vilivyo vya hatari kubwa zaidi kuliko magonjwa ya Ukimwi na Ebola.

Habari Kubwa