WHO yaitangaza rasmi China haina malaria

22Jul 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
WHO yaitangaza rasmi China haina malaria
  • Uthibitisho wa miaka 4 duniani ziko 40

KWA mara ya kwanza baada ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa miongo saba, China imetangazwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa taifa huru katika ugonjwa huo.

Mtaalamu wa China akionyesha uthibitisho, kipimo bila malaria. PICHA: WHO.

Huku ikiwa ndio mwasisi kwa mara ya kwanza malaria kuonekana nchini China na WHO inakuwa nchi ya 40 kutokomeza malaria kwa miaka ya karibuni ikiwamo Argentina, Algeria na Uzbekistan.

Unapozungumzia malaria, kwa nchi zinazoendelea utabaini kati ya vikwazo vikuu na vinasababishi vya kurudisha maendeleo nyuma, kuongeza umaskini na kupunguza nguvu kazi.

Malaria huathiri zaidi mataifa ya Kusini mwa Jangwa Sahara na katika baadhi ya mataifa ya Asia na Amerika ya Kusini, mbali na ukweli kwamba ugonjwa huu, una tiba, unaepukika umeendelea kusababisha vifo vingi duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema mtoto mmoja kila baada ya dakika mbili hufariki dunia, huku visa vipya zaidi ya milioni 200 vikiripotiwa kila mwaka.

Malaria ni kati ya ugonjwa unaohatarisha maisha unaosababishwa na mbu wanaombukiza baada ya kumng’ata mtu aliyeathiriwa nakisha mwingine, huku dalili za ugonjwa zikianza kwa homa, kuumwa kichwa na tiba isiyo ya mapema inachangia vifo.

Jukumu la kukabiliana na ugonjwa huo wakati zikiendelea kutafutwa na wataalamu wa afya duniani kote, WHO wiki kadhaa zilizopita imeitangaza rasmi China nchi kutoka bara la Asia, kwamba imefanikiwa kuiondoa malaria.
WHO

Mbinu mbalimbali hutumika hasa kwa nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania katika kujikinga na malaria kwa kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa (ITN), kupuliza dawa ndani na nje ya nyumba (IRS). Uzoefu wa mafanikio ya China katika kupambana na ugonjwa huo, umezua udadisi na nchi kadhaa kutaka kujifunza kufikia hatua hiyo.

WHO inasema, China baada ya miaka 70 imefanikiwa kuiondoa malaria, huku ikiwa kati ya nchi iliyowahi kukumbwa na hali mbaya sana, katika miaka ya 1940, walikuwa na mikasa milioni 30 ya malaria na tangu kipindi hicho, harakati zilianza kutafuta jibu la kukabiliana ugonjwa huo.

Shirika linasema, lilishuhudia nchi hiyo ikitumia mbinu mbalimbali katika kupambana na malaria, ikiwamo kuondoa mzunguko wa mazalia ya mbu.

WHO katika ripoti hiyo kuhusu mafanikio ya China dhidi ya malaria, limebaini kwa miaka minne sasa China haijarekodi kisa chochote cha malaria na kutangazwa rasmi, imefanikiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, anasema mafanikio ya China hayakuwa rahisi kwa miongo kadhaa, hadi kufikia mafanikio ya sasa.

CHINA YAFURAHIA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje China, Wang Wenbin, anasema kuiondoa malaria kunatokana nan chi hiyo kujali afya na haki za binadamu, huku wakijiandaa na kuandaa Sherehe ya Miaka 100 ya Chama cha China Kikomunisti (CCP), wakijivunia kutambuliwa na WHO kufikia hatua hiyo.

"CCP na serikali ya China, kila mara imeweka kipaumbele katika kulinda afya za watu wake,” anasema Wenbin.
Serikali ya China ilifanikiwa kushusha kiwango cha maambukizi ya malaria kwa kutumia dawa za kujikinga za kupulizia kwenye mazalia ya mbu, sambamba na kugawa vyandarua vilivyotiwa dawa.

MIKASA YA MALARIA

WHO inasema, pamoja na kuwapo kinga, tiba inatolewa mara tu ugonjwa anapogundulika, inakadiriwa mwaka 2019. Matukio ya malaria duniani yalifikia milioni 229 yakiwa na vifo 409,000, (chini ya asilimia moja), huku takribani asilimia 94 ya vifo vikitokea barani Afrika.

WHO inasema, nchi inaweza kuomba kuthibitishwa kama haina malaria iwapo itaripoti miaka minne mfululizo bila ya tukio lolote la ugonjwa huo na kuwasilisha ushahidi wa kuonyesha uwezo wao katika kuzuia mikasa katika siku zijazo.

Mapema mwaka huo, chanjo iliyotayarishwa na Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza na kufanyiwa majaribio kwa asilimia 77, ikiwamo nchi ya Burkina Faso na kwamba yatazifikia nchi nne za Afrika.

DAWA ASILI

Wanasayansi wa China, pia walitumia dawa za asili kutibu malaria miaka ya 1970 na kwamba aina ya Artemisinin, iligunduliwa kutoka kwenye mitishamba tangu karne nne.

Mtaalamu Prof. Lang Linfu, anasema ni kati ya wataalamu waliohusika kwenye utafiti na wanasayansi hao, wakibaini dawa hiyo inatibu malaria ikiwa na tatizo dogo linalotokana na athari za dawa yoyote na imeokoa mamilioni ya watu duniani.

Habari Kubwa