Wiki ya Sheria, elimu yake iwafikie wanafunzi shuleni

15Feb 2020
Reubeni Lumbagala
Dodoma
Nipashe
Wiki ya Sheria, elimu yake iwafikie wanafunzi shuleni

KILA mwaka nchini, kunakuwepo Siku ya Sheria, ambayo shughuli mbalimbali zinafanyika, ikiwamo utoaji elimu kwa umma kuhusu masuala ya kisheria na kimahakama.

Siku ya Sheria kwa Mwaka 2020 inachagizwa na kaulimbinu isemayo “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.”

Kabla ya kufikia kilele cha Siku ya Sheria, kunatanguliwa na Wiki ya Sheria, ambayo pamoja na mengine, kuna maonesho mbalimbali ya wadau wa sheria, kwa ajili ya kuwapa wananchi uelewa wa sheria zinazotumika mahakamani.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alikuwa mgeni rasmi wa matembezi maalum ya Wiki ya Sheria, yalioanzia Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma na kuishia viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.

Katika hotuba yake, Spika Ndugai alisema: “Bunge litashirikiana na serikali kuhakikisha mahakama inapata rasilimali za kutosha, ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati.” Ni kauli hii inayonesha namna ambavyo mihimili inavyoshirikiana katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, alisema:“Katika Wiki ya Sheria kutakuwa na maonyesho ya utoaji elimu ya mahakama yatakayofanyika rasmi kuanzia Januari 31, 2020 hadi Februari 5, 2020 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma na Mahakama mbalimbali nchini.”

Wadau ambao wameshirikiana na mahakama katika maonesho hayo kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ni pamoja na; Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, majeshi ya Magereza na, Polisi, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Tume ya Haki za Binadamu.

Wadau hawa wamefanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ambao wamepata fursa ya kufika katika maonyesho hayo ili kujifunza masuala mbalimbali ya sheria na namna mahakama zinavyofanya kazi katika utoaji wa haki kwa wananchi wake.

Sheria ni nyanja muhimu ambayo wananchi wanapaswa kuifahamu japo kwa sehemu hasa katika kutambua haki zao na kuzidai pale zinapokiukwa. Kwahiyo, ni muhimu elimu ya sheria iwafikie wananchi wake katika kujenga jamii inayojitambua ili kupunguza kitendo vya uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Katika mafanikio ya utoaji wa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kimaendeleo kama suala la elimu ya sheria kwa umma, ni vyema elimu hiyo ikaanzia ngazi ya chini yaani kuwaelimisha watoto kujitambua, ili watakapokuwa wakubwa wawe ni watu wanaojitambua na wanaoweza kudai haki zao kwa ujasiri mkubwa katika mamlaka husika.

Kalamu ya Mwalimu inashauri, wanafunzi walioko katika shule za msingi na sekondari nchini wafikiwe na elimu ya sheria ili waweze kufahamu mambo ya msingi kuhusu sheria na haki za binadamu.

Wiki ya sheria imemalizika Februari 05 na kilele chake kimehitimishwa Februari 6, 2020. Pamoja na kumalizika kwake, wadau wamefanya kazi nzuri ya kuwaelimisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Pengine, mhimili wa mahakama unaweza kuangalia uwezekano wa kuongeza siku kadhaa mbele ili elimu hiyo muhimu iwafikie wanafunzi walioko shuleni, ambao hawakuweza kufika katika viwanja vya maonesho kupata elimu hiyo muhimu.

Wanafunzi wanapaswa kuelimishwa vya kutosha kuhusu haki za watoto na haki za binadamu kwa ujumla. Watoto wakiandaliwa vyema katika kutambua haki zao, Taifa letu litafanikiwa sana katika juhudi za maendeleo.

Zipo changamoto za ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi, hivyo wanafunzi wakipewa elimu ya sheria itawajengea uwezo wa kujua namna wanavyoweza kuripoti matukio hayo kwa usalama na maendeleo yao.

Wanafunzi shuleni ni wadau wakubwa wa kufanikisha azma ya kufikia maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati kupitia kupata elimu bora. Elimu ya sheria itawasaidia wanafunzi kufahamu namna mahakama na utungaji wa sheria bora unavyoweza kuwa chachu ya kufanikisha maendeleo ya biashara na uwekezaji kwa kutenda haki kwa wananchi na kutafsiri vyema sheria za biashara na uwekezaji.

Kwahiyo, wadau wa wiki ya sheria waangalie namna wanavyoweza kufanya ili kuwafikia wanafunzi mashuleni ili kuwapa elimu ya sheria kwani wengi wao hawakupata fursa ya kufika katika viwanja vya maonesho kupata elimu hiyo adhimu.

Mahakama ione umuhimu wa kuwafikia wanafunzi katika kuwaelimisha ili wajitambue na waweze kudai haki zao. Elimu ianze kutolewa kwa wanafunzi shuleni halafu elimu hiyo isambae kwa wananchi wengine. Tafakari.

•Reubeni Lumbagala ni walimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Anapatikana kwa simu namba: (+255) 765 409249.

Habari Kubwa