Wilaya inavyoibuka kimikakati kwenye sayansi, yaandaa wasomi

24Aug 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wilaya inavyoibuka kimikakati kwenye sayansi, yaandaa wasomi

YANAPOTAJWA masomo ya sayansi, juhudi mbalimbali zinafanyika ikiwa ni pamoja na kujenga sekondari maalumu za kila mkoa za wasichana, ili taifa liwe na hazina ya akiba ya wanawake wanasayansi, shule hizo zinaanza kuandaliwa mwaka huu.

Baadhi ya wanafunzi wa Mugango Sekondari wakijifunza masomo ya sayansi kwa vitendo, katika moja ya maabara ya shule hiyo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Masomo hayo yanapigiwa chapuo na wadau wa elimu, ili kuwahamasisha wanafunzi wayapende na taifa kuwa na wataalamu wengi wa baadaye wa fani hiyo watakaoshughulikia mahitaji na changamoto mbalimbali za nchi.

Katika harakati za kuhakikisha lengo hilo linatimia, Wilaya ya Musoma mkoani Mara, imeanza mkakati wa kuzigeuza baadhi ya sekondari zake kuwa za kidato cha tano na sita zitakazofundisha masomo ya sayansi. utekelezaji wa mkakati huo, ukianza mwakani, kama Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya, Majidu Karugendo, anavyoieleza Nipashe hivi karibuni.

Anazitaja sekondari hizo kuwa ni ya Rusoli, Kiriba, Mugango na Bugwema ambazo anafafanua kuwa zina maabara za masomo yote matatu ya sayansi ambayo ni kemia, fizikia na baiolojia.

"Wilaya ya Musoma ina sekondari 21 na nyingine zinaendelea kujengwa, lakini tutaanza na nne, ili nasi tutoe wataalamu wa fani mbalimbali watakaowezesha taifa kusonga mbele " anasema Karugendo.

Anaeleza kuwa kinachoendelea katika sekondari hizo ni walimu kuwahamasisha wanafunzi, ili kupenda masomo ya sayansi pia kuwafundisha kwa vitendo kwa kutumia maabara zilizopo shuleni.

"Ni muhimu kuandaa vijana wetu wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye mabadiliko ya viwanda, nasi tunataka wataalam wa fani mbalimbali watokee huku kwetu, siyo maeneo mengine tu," anasema.

Ofisa Elimu Karugendo anawaomba wadau wa maendeleo ya elimu kuendelea na moyo wa kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya sekondari, ili kuhakikisha shule zote zinakuwa na maabara tatu na maktaba.

Anatolea mfano Mugango Sekondari, kwamba ina maabara zote tatu zinafanya kazi, lakini inakabiliwa na uhaba wa baadhi ya miundombinu mengine ambayo anaona ni muhimu kushirikisha wadau kuiboresha.

Akizungumzia maboresho ya miundombinu hiyo, Mkuu wa shule hiyo, Chacha Ragita, anaelezea uhaba huo na kusema ni wa madarasa 20 wakati yaliyoko ni 16 pekee wakati idadi ya wanafunzi ni 800.

Shule ina uhaba wa nyumba za walimu ziko nne, wakati zinazohitajika ni 18 na kuongeza kuwa kuna walimu 18, lakini mahitaji halisi ni 25.

“Tunaamini serikali itaongeza wengine kadri inavyowezekana, pia kwenye vyoo, kuna matundu 24, yanayohitajika ni 34, hivyo tunawaomba wadau wasichoke kusaidia kuboresha mindombinu ya shule hii," anasema Ragita.

Aidha, anasema, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilishatoa vifaa vya maabara zote tatu na pia kuchangia Shilingi milioni 75, kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike ambao mkuu huyo wa shule anafafanua kuwa tayari umeanza.

"Pia mbunge wa jimbo, Profesa Muhongo ametoa mifuko 130 ya saruji na vitabu mbalimbali vikiwamo vya masomo ya sayansi zaidi ya 2,000, kwa ajili ya maktaba ya shule yetu ni sehemu ya fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo," anasema.

Anaongeza kuwa shirika la Water Aids Tanzania nalo limetoa matangi mawili ya   maji yenye ukubwa wa lita 5,000 kila moja kwa ajili ya matumizi ya shule na kwenye maabara.

Aidha, Ragita, anazungumzia ufaulu, akisema kwa upande wa ufaulu wa mitihani kidato cha nne mwaka 2020 , watahiniwa walikuwa 83, huku waliofaulu daraja la kwanza wakiwa wanne, daraja la pili watano, daraja la tatu 14, daraja la nne 39 na daraja la sifuri 21.

"Kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili, watahiniwa walikuwa 175, ambapo daraja la kwanza walikuwa nane, daraja la pili 11, daraja la tatu19, daraja la nne 121 na daraja la sifuri 16," anasema.

UHAMASISHAJI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma, anasema madiwani na viongozi wengine akiwamo mbunge, wanashiriki kukamilifu kuhamasisha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo ya elimu.

Magoma anasema, uhamasishaji huo umeingia kuifanya halmashauri hiyo kuwa na sekondari 21 ambazo wananchi wameshiriki kwa hali na mali kuzijenga ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu.

"Wananchi wamekuwa wakitoa nguvukazi ya kusomba, maji, mawe, mchanga na kokoto na wakati mwingine kuchangia fedha, ili kuunga mkono serikali katika ujenzi wa sekondari katika maeneo yao," anasema Magoma.

Mwenyekiti huyo anasema, hatua inayofuata sasa ni kuhakikisha halmashauri hiyo inakuwa na shule japo nne za kidato cha tano hadi cha sita za masomo ya sayansi, ili kuwa na wataalum wengi wa baadaye.

"Tunatamani wanafunzi wa mchepuo wa sayansi wanaofaulu kidato cha nne katika mikoa mingine waje waendelee na masomo yao katika sekondari zetu, ili nasi tutoe wataalam," anasema.

Halikadhalika, anasema wanaunga mkono juhudi za kuleta mapinduzi ya kiuchumi, ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

"Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ambao sasa unaingia awamu ya tatu unatarajiwa kufanikishwa na uwapo wa rasilimali watu wakiwamo wataalamu wa sayansi na teknolojia," anasema.

Anasema dira hiyo inalenga kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi, ili kulifanya taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025 ambayo ni miaka minne kuanzia sasa.