Wilaya yaibua kaulimbui 'Elimu Kwanza' *Majibu 2021,

24Nov 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wilaya yaibua kaulimbui 'Elimu Kwanza' *Majibu 2021,

BAADA ya awamu ya tano kuanza kugharamia elimu kuanzia darasa la awali hadi sekondari ni hatua inayoendana na ongezeko kubwa la wanafunzi kuanzia usajili shule ya msingi hadi kuingia vyuo vikuu.

Maeneo mengi yamekumbana na ongezeko hilo na mojawapo ni Wilaya ya Musoma mkoani Mara ambayo sasa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa shule tano za sekondari, ambazo zinatarajia kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka ujao.

Shule hizo zinatajwa kuwa ni Bukwaya, Kigera, Nyasaungu, Ifulifu na Seka, ambazo kwa mujibu wa Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya, Majidu Karugendo, ujenzi uko hatua za mwisho, ili kupokea wanafunzi hao.

Katika mazungumzo na gazeti hili wiki iliyopita, Karugendo anasema, wilaya inaendelea na mkakati wa kuboresha elimu kwa kuongeza shule za sekondari za kata, ikitumia kaulimbiu 'Elimu Kwanza'.

"Lengo la kaulimbiu hii ni kuhimiza wananchi kutambua umuhimu wa elimu, wachangie ujenzi wa shule ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bila kutembea umbali mrefu," anasema Karugendo.

Anaongeza kuwa Idara ya Elimu Sekondari pia ina jukumu kuhakikisha shule zake zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ili kuiwezesha wilaya hiyo kuendelea kuwa juu kitaaluma.

"Wilaya inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali hasa ya ujenzi wa madarasa kwa kushirikisha wananchi, ili kupanua wigo wa elimu kwa shule za sekondari ili pia wanafunzi wawe katika mazingira bora ya kujifunzwa na kujifunzia," anasema.

SHULE TANO TENA

Karugendo anawahakikishia wananchi kuwa mbali na shule hizo tano kufunguliwa Januari mwaka ujao, zitajengwa nyingine tano kuanzia mwaka 2021 lengo likiwa ni kuendelea kuboresha elimu.

Anazitaja sekondari hizo wanazotarajia kujenga kuwa ni Etaro, Makojo, Ugango, Suguti na Tegeruka, ikiwa ni mwendelezo wa kuboresha elimu wilayani mwao, kuwapunguzia wanafunzi vikwazo vya njiani.

"Vilevile, miaka mitano ijayo, tunatarajia kuongoza shule za kidato cha sita kutoka mbili zilizopo sasa hadi kufikia sita na hilo litawezekana kwani tumedhamiria kuboresha elimu," anasema.

Anaongeza kuwa wananchi wamehamasika na sasa nguvukazi yao inatumika, ikiwamo kusomba maji, mchanga, mawe, kokoto na hata watu kuanzia miaka 18 hadi 59 kutoa fedha taslimu.

Karugendo anafafanua kuwa, wilaya hiyo ina vijiji 68, kata 21 na shule sekondari 20 za kata na mbili za binafsi na kwamba wananchi wanaendelea kushirikiana na serikali katika jitihada za kuongeza sekondari mpya.

"Ninajua penye mafanikio hapakosi matatizo, hivyo hata katika mafanikio haya, yapo matatizo machache, ambayo ni baadhi ya wananchi kutoshiriki kikamilifu ujenzi wa sekondari, lakini tunaendelea kuelimisha," anasema.

SEKONDARI ZA VIJIJI

Karugendo anasema, baadhi ya wanafunzi hutembea umbali mrefu kufuata elimu na kujikuta wakichelewa kufika shule ama kurudi nyumbani na wakati mwingine wanafunzi wa kike wanakutana na vikwazo vingi njiani.

Kutokana na hali hiyo, anasema baadhi ya vijiji vimejenga sekondari za vijiji vyao, ili kuwaondolea watoto kero hiyo, ambayo kwa nyakati tofauti inasababisha usumbufu kwa wanafunzi.

Anatolea mfano vijiji vya Kigera Etuma, Kakisheri na Nyasaungu kwamba wakazi wake wameshirikiana na serikali kujenga sekondari za vijiji hivyo, ambazo ni miongoni mwa zile tano zitakazofunguliwa mwaka ujao na vyote vipo kata ya Nyakatende.

Wananchi wamejenga sekondari ya pili, hivyo watoto wao watasoma huko badala ya kwenda Nyakatende Sekondari, anasema.

Anafafanua kuwa kata ya Ifulifu, inaendelea na ujenzi wa sekondari ya kata hiyo, lakini wakazi wa kiijiji cha Nyasaungu kilichopo kata hiyo, wamejenga sekondari ya kijiji hicho na kwamba itafunguliwa Januari mwakani.

"Wanafunzi wa kijiji hicho kwa sasa wanasoma Nyakatende Sekondari ambako ni mbali. Yaani wanafuata elimu kata nyingine, lakini wazazi wao wanaona hakuna sababu na kwa pamoja wamejitolea kujenga sekondari ya kijiji," anasema.

MCHANGO WA WADAU

Naye Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, anasema, ni miongoni mwa wadau wakuu wa elimu ambaye amekuwa akihamasisha uboreshaji wa elimu na pia kutoa michango mbalimbali kuleta mabadiliko ya kielimu vijijini jimboni hapo.

"Kwa mfano kupitia fedha za mifuko ya jimbo tumetoa mifuko 100 ya sementi mabati 108, na huo ni mchango uliokwenda Sekondari ya Kigere, lakini nimeshiriki kuchangia sekondari zote," Prof. Muhongo anasema.

Anafafanua kuwa kama mbunge anashirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali kuhimiza wananchi kuchangia maendeleo ya elimu, kwa vile elimu ina mchango mkubwa katika maendeleo.

Anasema, ingawa wapo baadhi ambao bado ni wazito, lakini anaamini kwamba, wananchi wataelewa na kushiriki kikamilifu pamoja na wadau wengine katika uboreshaji wa elimu hasa kwa kuchangia ujenzi wa shule na kuwa na za kutosha.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyakatende, Marere John, anasema, kwa kushirikiana na wadau wengine ametengeneza madawati 120 kwa ajili ya wanafunzi watakaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza katika Sekondari ya Kigera, mwaka ujao.

"Tuko hatua za mwisho za ujenzi wa Sekondari ya Kigera kwa kusaidiana pia na wazaliwa wa vijiji vya Kigera Etuma na Kakisheri wanaoishi mikoa mbalimbali, wanawalipa mafundi na kununua vifaa vya ujenzi," anasema John.

Habari Kubwa