Wiki ya maji Dar, Waliokosa maji miaka mingi waanza kufaidika

23Mar 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Wiki ya maji Dar, Waliokosa maji miaka mingi waanza kufaidika

KWA miongo miwili sasa Tanzania, inaadhimisha Wiki ya Maji, mwaka huu, maadhimisho yalianza Jumamosi iliyopita Machi 16 na kuhitimishwa jana kitaifa mkoani Dodoma.

MAJI 2-Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto, akimtua mama ndoo kichwani baada ya kuzindua mradi wa maji mtaa wa Majengo Vingunguti Jijini Dar es Salaam, utakaohudumia wananchi 1,440 ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani.

Ikumbukwe kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Usimwache mtu nyuma katika kupata huduma ya maji.’ Ikimaanisha kuwa Watanzania wanaoishi mijini wanafikiwa na huduma hiyo kwa asilimia 95 wakati wa vijijini ni kwa asilimia 85.

 

Katika wiki hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Cyprian Luhemeja, anazungumza na Nipashe na kueleza kuwa mamlaka hiyo imetekeleza miradi iliyofikisha maji kwa wananchi ambao awali walikuwa hawana huduma hiyo.

“Mfano ni eneo la Salasala na Kinzudi ambalo halikuwa na maji, lakini sasa wananchi wanapata huduma baada ya mradi kukamilika.

 

Hii ilihusu ulazaji wa bomba kwa umbali wa kilometa 48 na ujenzi wa tangi kubwa la ujazo wa lita 6,000,000 katika eneo hilo, pamoja na kituo cha kusukuma maji,” anaeleza Luhemeja.

Kadhalika, anataja kuwa katika mradi huo zaidi ya wateja 5,400 wa maeneo hayo wameunganishwa kwenye mtandao wa huduma hiyo, huku akitoa wito kwa wananchi ambao wanahitaji kuunganishwa ili kupata maji wajitokeze.

Akizungumzia mradi mwingine ambao sasa wananchi wanapata maji, Luhemeja, anasema ni ule wa eneo la Kiembeni Bagamoyo mkoani Pwani ambalo halikuwa na maji kabla ya mradi huo.

“Baada ya kukamilika, wananchi zaidi ya 2,000 wameunganishwa na kuanza kupata huduma ya maji safi na salama,” anaongeza na kufafanua kuwa mradi mwingine ni wa 2D uliofikisha maji Kiluvya, Kibamba, Hondogo, Mloganzila na Kwembe wilayani Ubungo.

“Mradi huu nao umekamilika na wananchi wa maeneo haya wataanza kunufaika na huduma ya maji kwa awamu, kadiri maunganisho yanavyoendelea kufanyika, ambapo hadi sasa takribani wateja 6,500 wanafurahi huduma hii,” anaongeza Mtendaji Mkuu wa Dawasco.

Anasema katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa Kiwalani Bombom na vitongoji vingine, Dawasa imekamilisha mradi wa maji sehemu hiyo. 

KUONANA NA WATEJA

Mwaka huu maadhimisho yalishuhudia kuonana na wateja. Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam, ilifungua dawati maalum kwa ajili ya kuhudumia wateja katika viwanja vya Mnazi Mmoja lililolenga kuwasikiliza na kumaliza kero zao, anaeleza Neli Msuya.

Akizungumza katika viwanja hivyo, wakati wa uzinduzi, Msuya, Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Dawasa, anasema mwaka huu maadhimisho yamekwenda pamoja na kuhakikisha kuwa kila idara ya shirika hilo inasikiliza kero na changamoto za wateja na kuzitatua kwa wakati.

“Dawasa imefungua dawati maalum kwa wateja ambalo ni la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema), Miradi ya Maji na dawati la manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hivyo, tunawahamasisha wananchi kujitokeza ili tuwahudumie,” anasema Msuya.

Anaongeza kuwa katika maadhimisho hayo, ambayo kitaifa yalihitimishwa jana mkoani Dodoma, kama kauli mbiu inavyoeleza , hakuna atakayeachwa katika kuongeza, kasi ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika dunia inayobadilika kitabia nchi, juhudi nyingi zimefanyikiwa.

Anaeleza, kuwa wananchi watakaofika katika viwanja vya Mnazi Mmoja watapata fursa ya kupata maelezo ya mipango inayoendelea kutekelezwa ili kuboresha sekta na huduma ya maji Dar es Salaam na miji jirani ya mkoa wa Pwani. 

MIRADI IJIONGEZEAkizindua mradi wa maji Mtaa wa Majengo ulioko Vingunguti utakaohudumia wateja 1,440 kwa siku, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilamoto, anapongeza juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Mhandisi wa Maji Manispaa ya Ilala uliofanikisha kumalizika kwa kazi ya kuwapa wananchi maji kwa wakati.

Anaeleza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huu ambao ulikuwa unasubiriwa na wananchi kwa muda mrefu, jumuiya ya watumia maji ijiongeze ili kusimamia mradi huu kwa weledi ujiendesha na uweze kuzalisha miradi mingine.“Tunajua kunakuwa na changamoto hususani kwenye jumuiya za maji kwa kushindwa kusimamia miradi iliyopo kwenye mitaa ila napenda kuwaambia kuwa jumuiya wahusika mjiongeze kwa kusimamia miradi ili ijiendeshe yenyewe na kuzalisha mingine kwa kuwa visima vya watu binafsi vimekuwa na maendeleo kuliko vya serikali,” ni kwa sababu ya usimamizi anasema Kumbilamoto.

Aidha, anaziagiza Manispaa kuangalia bei za maji na kuweka utofauti kati ya gharama zinazotozwa na visima vya watu binafsi na vya serikali ili wananchi wengi wapate maji safi na salama.

“Wananchi watunze miundo mbinu ya maji ili iweze kudumu na wapate maji safi na salama kwa kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano kama inavyoainishwa na makamu wa Rais Samia Suluhu ni kumtua mama ndoo kichwani,”anasisitiza Kumbilamoto.Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Upendo Lugongo, akizungumzia gharama za mradi huo anasema, kuanzia eneo lililojengwa mradi huo, kuchimba kisima, kujenga vizimba vya kuchotea maji na tangi lenye uwezo wa kuzalisha lita 4,800 kwa siku kwa ajili ya wananchi wa mtaa wa Majengo gharama ya Sh milioni 28, imetumika.

 

Lugongo aliwaomba wananchi kuendelea kulinda miundombinu pamoja na kutumia maji hayo kwa uangalifu na kwa manufaa ya wote.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Majengo, Chande Msoke, ameishukuru serikali pamoja na kamati ya utendaji ya mtaa kwa kupitisha bajeti iliyofanikisha kumalizika kwa mradi huo ndani ya wakati na kuwa kwa sasa kero ya maji kwenye mtaa wake umemalizika.Katika kusherehekea Wiki ya Maji iliyoanza Machi 16 na kumalizika Machi 22, miradi mbalimbali ya maji ilizinduliwa ikiwa mikakati ya kuhakikisha kuwa ikifika mwaka 2020 asilimia 95 ya wakazi wa mijini wawe wanapata maji safi na salama na asilimia 85 kwa upande wa vijijini.

Habari Kubwa