Wingi makada CCM kuwania uspika Unapohusishwa na kuchangamkia fursa

19Jan 2022
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wingi makada CCM kuwania uspika Unapohusishwa na kuchangamkia fursa
  • * Idadi ndogo ya wanawake yatetewa

WATANZANIA hujengewa fikra na imani kuwa ili ‘utoke kimaisha’ ni lazima kupitia barabara ya siasa, kunatajwa kuwa chanzo cha msukumo mkubwa na ari ya wana CCM 70 kuchukua fomu ya kuziba nafasi ya uspika, iliyoachwa wazi na Job Ndugai, aliyejiuzulu hivi karibuni, kutokana na kauli yake kuhusu ..

Mbunge wa Nyasa, Stella Manyanya, ni miongoni mwa wana CCM waliochukua fomu kuwania uspika. PICHA: MTANDAO

mikopo mipya na kuongezeka kwa deni la taifa.

Kwa sasa fomu za wagombea 70 zimeshapokelewa na mchakato unaendelea ndani ya chama hicho ukiwa ni wa kuchuja waliojitokeza, ili hatimaye wapatikane wale ambao watachuana katika kinyang'anyiro kwa ajili ya kumpata atakayeziba nafasi hiyo kwa kupigiwa kura bungeni mwanzoni mwa mwezi ujao.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakizungumzia kwa nini watu wengi wamejitokeza kiasi hicho kuwania nafasi hiyo,akiwamo Godwin Gonde ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, anasema, Watanzania wamejengewa mfumo ambao wanaamini kuwa njia pekee ya kutoka na kufanikiwa kimaisha ni kupitia siasa.

"Wanaamini kuwa kila mmoja ana haki  kuwaania nafasi yoyote ndani ya chama na hata serikalini, na wanachukulia kama jukwaa la kutaka kujulikana ili kupimwa na hatimaye kuchaguliwa," anasema Gonde.

Anasema, mazingira hayo ndiyo yanawafanya wajitokeze kwa wingi, na hata wakati mwingine bila kujipima kama wana uwezo wa kuongoza mhimili huo na kwamba wanaangalia kile wanachotarajia kukipata baada ya kuchaguliwa.

"Wengine wanaangalia uchaguzi wa ndani ya chama utakaofanyika mwaka huu, wanataka kujitangaza kupitia njia hiyo ya kuwania uspika ili iwe rahisi kujulikana kwa wana CCM na Watanzania kwa ujumla," anasema.

       KUCHANGAMKIA FURSA

Mjumbe wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda, anasema, siku hizi wanasiasa wamekuwa ni wepesi wa kuchangamkia fursa kwa lengo la kujinufaisha wao na familia zao kiuchumi na kimapato.

"Ni haki yao kuwania nafasi hiyo, lakini binafsi ninaamini kuwa kinachosumbua wengi ni fursa kwa ajili ya kupata maslahi manono zikiwamo fedha na heshima kwenye jamii pamoja na familia zao, lakini pia wanataka wawe kwenye rekodi," anasema Mwakagenda.

Kuhusu rekodi hiyo anafafanua kuwa, wakikosa nafasi ya uspika, majina yao yatakuwa yamejulikana, na kwamba yawezekana mamlaka za uteuzi zikawaona na kuwateua katika nafasi nyingine za uongozi wa nchi.

"Hivyo huo ni mkakati wa kisiasa wa kujitangaza, ili kwamba hata kama watakosa, inawezekana siku moja mamlaka zikaulizia CV zao kwa lengo la kuteua miongoni mwao katika nafasi mbalimbali. Kwa hiyo ninaona wingi wao unatokana na kuchukulia kama fursa," anasema.

Anaeleza kuwa hata ikitangazwa nafasi ya katibu kata, wanaweza kujitokeza wengi kwa madai kwamba, siasa imekuwa ni ajira kwa ajili ya kutengeneza maisha bora badala ya kuzingatia weledi na vigezo na sifa za uongozi.

   WANAWAKE NI MAKINI

Katika idadi ya makada hao wa CCM waliojitokeza kuwania uspika, wengi wao ni wanaume, huku wanawake waliochukua fomu wakiwa wachache, ambapo inaelezwa kuwa hatua hiyo inatokana na umakini wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, anasema, kwa kawaida wanawake huwa si watu wa kukurupuka, bali wanapima jambo kwanza kabla ya kulifanya.

"Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa, uongozi siyo rahisi, ni kutumikia wananchi, jipime, jihoji kwanza, lakini pia ujue maana ya uongozi, na ndivyo wanawake wanafanya," anasema Liundi.

Mkurugenzi huyo anasema, uchache wa wanawake katika kinyang'anyiro hicho, unaonyesha jinsi ambavyo si wepesi wa kukurupikia jambo, badala yake wanakaa na kutafakari kwanza kabla ya kuchukua hatua.

"Kwa uchache wao huo, ninaweza kusema kuwa wanawake si watu wa kurukia vitu, wanapeleleza kwanza ndipo wanaamua. Kwa hiyo huo ndiyo mtazamo wangu kuhusu uchache wao," anasema.

Liundi anasema, hatua hiyo ya kutojitokeza kwa wingi, pia imeonyesha ni jinsi gani wasivyo na tamaa ya madaraka, bali lengo lao ni kutumikia wananchi na siyo kutafuta maslahi binafsi. Kinamama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Dk. Tulia Ackson, Stella Manyanya, Sophia Simba.

Msururu mrefu wa wanaume miongoni mwao yumo, Andrew Chenge, Stephen Masele, Mussa Azan Zungu na Dk. Thomas Kashilillah, Goodluck Mlinga, Athumani Mfutakamba, Norman Sigalla na Andrew Kevella, ambao wamejitosa kutaka kumrithi Job Ndugai aliyejiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni baada ya kutoa madai yaliyopinga na na mipango ya serikali ya kukopa fedha za maendeleo.

Ndugai alichukua hatua hiyo mwanzoni mwa mwezi huu, baada ya kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa viongozi mbalimbali ndani ya chama cha CCM kumtaka kujiuzulu kutokana na majibizano kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu serikali kuchukua mikopo ya maendeleo.

Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima ni miongoni mwa waliomshauri kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kwamba hataweza kuliongoza bunge kwa madai kwamba, wabunge wote wasingekuwa upande wake.

Naye mbunge wa Mtera mkoani Dodoma (CCM), Livingstone Lusinde, alimtaka Ndugai kuchukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kwa kupitia video nzima ya hotuba ya Spika Ndugai aliyoitoa katika moja ya mikutano yake na wazee uliofanyika mkoani Dodoma.

Habari Kubwa