Yajue maradhi tata kwa mwanaume,yanavyompotezea sifa za uanaume

10Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Yajue maradhi tata kwa mwanaume,yanavyompotezea sifa za uanaume
  • Aeleza ucheleweshaji ulivyobeba janga
  • Pombe kali, janga lingine kwa kinababa

“…Kwa zaidi ya saa nne bila ya kuwa na hisia ya tendo la ndoa, huu ni ugonjwa na inatakiwa mhusika kufika hospitali mapema, kwani anapochelewa anasababishia uume wake kushindwa kusimama katika maisha yake,” ni maneno ya daktari bingwa wa upasuaji mfumo wa mkojo, Ryuba Nyamsongola.

Madaktari wakimhudima mgonjwa wa maradhi tajwa katika makala.PICHA MTANDAO.

Dk. Nyamsongola anayasema alipohojiwa na Nipashe akisema, kitaalamu ugonjwa huo unaitwa Priapism. Ni tatizo linalotokea pale uume unaposimama kwa muda mrefu zaidi ya saa nne bila ya kuwepo hisia ya tendo la ndoa.

Anasema sababu ya kutokea hilo, ni kuwepo kwa hitilafu katika kushindwa kutoka kwa damu kwenda eneo jingine na kusababisha uume kuendelea kusimama kwa muda mrefu.

“Kwa kawaida, kusimama kwa uume ni kwamba damu inashuka chini, inakwenda kwenye kiungo na kiungo kinajaa, lakini kinatakiwa kijae kwa muda pale unapokuwa na hisia na baada ya ama hisia au tendo kwisha, ile damu inatakiwa itoke na kurudi katika sehemu niyingine za mwili. Damu ndio inasababisha uume kujaa,” anasema

ATHARI ZIKOJE?

Dk. Nyamsongola anasema, kuna aina mbili ya ‘Priapism’ ya kwanza ni damu kushindwa kwenda kwenye uume. Hii natokea mara kwa mara, yaani mirija imeziba na damu inashindwa kutoka kwenda sehemu nyingine.

Anasema, aina ya pili inasababishwa na ajali katika maeneo ya siri na kuwepo kwa muungano wa mishipa inayosababisha damu kwenda kwenye uume, inakuwa ni nyingi kuliko inayotoka.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa kwa aina hizo mbili, ya kwanza inahitajika kwa dharura kwani kama damu haiendi kwenye uume, mara nyingi unavimba na nyama zake zinakufa.

“Kwa huu ugonjwa ndani ya saa 24, mgonjwa anatakiwa kufika hospitali na kuhudumiwa akichelewa inakuwa ni shida … wengi wetu wanakuja hata saa 72 na nyama za uume zinakuwa zimekufa . Sasa zikifa huu uume unaweza usifanye kazi tena katika maisha yake yaliyobaki,” anasema mtaalamu huyo.

Anaeleza kuwa moja ya tatizo hasa kwa Tanzania, ni kuwepo magonjwa ya damu anayotaja kama vile: Seli muundo, Lukemia ambayo ni saratani ya damu na saratani. Nyinginezo.

“Kwa ugonjwa kama wa Seli Muundo, unasababisha mirija ya kutoa damu kwenye uume, ili usinyae inaziba kutokana na seli zake, hivyo inapoziba ina maana damu itakuwa inaingia tu bila kutoka,” anasema

Dk. Nyamsongola anasema, mbali na Seli Muundo na Saratani nyingine za damu, ‘Priapism’ inaweza kusababishwa na ajali kwenye maeneo ya siri.

Anafafanua kuwa ajali hizo husababisha kuwepo na muunganiko wa mishipa ya damu; mshipa wa kuingiza damu na kutoa damu zinaungana na kusababisha kutoweka mfumo wa kutoa damu.

Anataja sababu nyingine ya kutokea ‘Priapism’ ni baadhi ya dawa zinazoweza kusababisha mgonjwa akapata tatizo hilo.

“Baadhi ya dawa zinazotibu shinikizo la damu , baadhi ya dawa zinazotibu afya ya akili, kuna sindano za chakula yaani zile za dripu zinaweza kusababisha kupata hilo tatizo,” anasema

Anaongezea kuwa: “Zaidi ya hapo kuna sindano zinazochomwa … wapo baadhi ya watu wana matatizo ya kusimamisha, hivyo huwa wanachoma sindano katika uume wao ili wasimamishe, vilevile zinaweza kumsababishia kupata tatizo la Priapism,” anasema daktari huyo.

Anasema, kuchoma sindano hizo kila mara kwa baadhi ya watu zinaweza kumleetea hayo madhara ya uume kusimama muda mrefu, pasipo msukumo wa kihisia.

Dk. Nyamsongola anasema ulevi uliopitiliza matumizi ya baadhi ya vilevi, kama dawa za kulevya, nazo zinaweza kusababisha kutokea maradhi hayo ya ‘Priapism.’

“Unaweza kusimamisha kwa muda mrefu, ndio maana utawasikia walevi wanaotumia ….(kinywaji kikali) wanapata hiyo hisia, lakini hawawezi kufikia hii ya zaidi ya saa nne, yaani hali ya hisia inakuwa haipo,” anaeleza.

Dk.Nayamsongola anafafanua zaidi, akisema: “Wengine wanakunywa… na hisia anaipata, lakini kuna wakati ukinywa pombe sana, unaweza kutokewa na hiyo hali,”

Mtaalamu huyo aliyeshawahi kutumika kama daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema utafiti walioufanya, kwa asilimia 50 ya wagonjwa chanzo kikuu bado hakijulikani ni nini.

“Utafiti tulioufanya tukagundua sababu zinazochangia ni hizo na hii asilimia 50 tukashindwa kugundua ni nini kinachochangia hii, mtu kupata ‘Priapism.’

“Sio kila mmoja anayekuja na ‘Priapism’ tunagundua sababu wanaweza wakaja wagonjwa 10, watano wakajulikana sababu na watano sababu zisijulikane,” anasema

Huku akisema wagonjwa wake wako zaidi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Nyamsongola anafafanua kuwa:

“Kwa mwaka juzi na mwaka jana ndani ya miezi mitatu unaweza kupata wagonjwa watatu ama wawili na baadhi yao wengi wao wanakuwa na tatizo la seli muundo.”

DALILI ZAKE

Dk. Nyamsongola anasema, dalili ya ugonjwa huo ni uume kusimama muda mrefu, inayoendana na muamivu makali kwa mgonjwa.

Anasema, namna ya kuchunguza tatizo hilo huwa wanapima damu na kwenye damu wanaweza kuangalia chanzo cha ugonjwa, kama ni chembehai au saratani ya damu.

Pia, anasema wanaweza kupima mkojo kujua kama mgonjwa ametumia aina ya kilevi au dawa za kulevya na huwa wanafanya vipimo vya aina ya ‘Utra Sound’ kuangalia muunganiko wa mishipa ya damu, hasa kwa wamliopata ajali.

TIBA YAKE

Dk. Nyamsongola anasema, matibabu ya ugonjwa huo yanatagemea aina ya mgonjwa na kama ni ya kwanza, ambayo damu inashindwa kwenda kwenye uume, inabidi tiba yake iwe ya dharura.

Anasema lengo ni kuondoa damu iliyoganda ndani ya uume na kubadilisha mwelekeo wa damu (Shanting).

“Damu inakuwa imeganda kama mabonge hii inabidi iondoke na kubadili mwelekeo. Wakati mwingine tunachukua sindano na kuanza kuiondoa hiyo iliyoganda.

“Damu ilikuwa inakuja sehemu ya kutokea inakuwa imezuilika na kubakia hapo ndani ya uume sasa hapa unapoiondoa unabadili mwelekeo na kufanya ile inayokuja iweze kutoka,” anafafanua.

Anataja tiba nyingine, ni kukabili visababishi husika, yaani kama mgonjwa amekuja na ‘chembe hai muundo’ anapatiwa tiba.

KUPONA UGONJWA

Anasema kwa mgonjwa ambaye anafika ndani ya saa 24 kwenye matibabu, ana nafasi ya kupona na kurejea katika hali yake na kwa wale ambao wamechelewa, wanapata tiba kurudia hali ya zamani inakuwa vigumu.

“Ikipita saa 48 (sikumbili) au 72 (Siku tatu ) mara nyingi, uume unaweza usifanye kazi na watu wa aina hiyo kwa vile, wengi wanakuwa ni vijana kama atataka kufanya tendo la ndoa, inabidi atafutiwe njia nyingine ya kusaidia ambayo huwekewa vifaa maalum ili aweze kusimamisha,” anasema

Anasema, matibabu hayo kwa nchini Tanzania bado hayajaanza na kuna baadhi ya wagonjwa walishawahi kuwekewa vifaa hivyo nchini India.

USHAURI

Dk. Nyamsongola ambaye kwa sasa anafanya kazi katika hospitali ya Doctors Plaza Clinic, anasema inapotekea mtu amepata tatizo hilo la uume kusimama zaidi ya saa nne, anatakiwa kuwahi hospitali akapatiwe tiba, badala ya kuingiza imani potofu kutafuta tiba kwa waganga.

Dk. Nyamsongola anasema: “Watu wanatakiwa kuelewa huu ni ugonjwa na upo siku nyingi na kwenye jamii yetu upo jambo la msingi unapoona dalili zimetokea, ni kuwahi hospitali kwa ajili ya kupata tiba sahihi, linatibika akichelewa tiba yake inakuwa ngumu na huwezi kupona.”

Anahitimisha kwamba, mtu anapotibiwa ugonjwa huo, mara nyingine ina tabia ya kujirudia kwa sababu tatizo la msingi bado lipo kwa mfano kwa yule mwenye ‘seli muundo.’

Habari Kubwa