Yalivyo maisha mapya kwa ngariba mstaafu ‘ngangari’

06Dec 2019
Sabato Kasika
Serengeti
Nipashe
Yalivyo maisha mapya kwa ngariba mstaafu ‘ngangari’
  • Ya leo; vitisho, marufuku kilimo, kutengwa
  • Asimamia uamuzi, mkufunzi wa waliokataa

SEHEMU ya kwanza jana, ilikuwa na simulizi ya ngaruba aliyeaacha, alichofanya huko na mkasa uliomuondoa katika kazi hiyo ya ukatili wa kijinsia na haki za binadamu. Endelea kujua anachokifanya sasa, katika ajira mpya.

Muhabe Marwa akionyesha baadhi ya kazi zake za ujasiriamali. PICHA: SABATO KASIKA.

MUHABE Marwa, alistaafu kazi ya ungariba mwaka 2016 akiwa amekeketa mara moja tu, lakini alipopata elimu dhidi ya vitendo vya ukeketaji, aliamua kuweka zana zake chini na kuhamia ajira kinzani.

Haukua mtihani rahisi kuacha kazi hiyo. kijijini alitengwa, wakamzuia kulima katika mashamba ya familia na vitisho lukuki. Kamwe hakubadilika, badala yake akatoka ‘kivingine’anashika chaki kuelimisha vita dhidi ya mila huyo potofu.

Katika mazungumzo yake na Nipashe, elimu iliyombadilisha inatoka kwa Rhobi Samwelly, Mkurugenzi wa taasisi ya Hope for Girls and Women Tanzania, iliyopo mjini Mugumu, Serengeti mkoani Mara.

Ngariba huyo mstaafu, sasa amepewa jukumu la kuwa ‘mhadhiri’ anayetoa elimu kuhusu mila na desturi za kabila la jamii yao waachane nambo yaliyopitwa na wakati, zikiwamo za ukeketaji.

Muhabe mwenye umri wa miaka 47, anasema ingawa uamuzi wake huo umesababisha akumbane na matatizo mengi, ikiwamo vitisho, msimano wake hatarajii kurudia kazi hiyo.

"Mimi kwa sasa ninaishi mjini Mugumu. Mara tu baada ya kuachana kazi ya ukeketaji, niliifanya kwa msimu mmoja wakati huo nikiishi katika kijiji cha Matare, wilayani Serengeti," anasema Muhabe.

Mama huyo anasema amelazimika kwenda kuishi mjini Mugumu katika nyumba za kupanga, kwa vile hakuona sababu ya kuendelea kuishi kijijini, wakati hakuwa na sehemu ya kulima, baada ya kunyang'anywa mashamba na ndugu zake.

"Kwa kweli hali bado haijawa nzuri, hasa baada ya kukosa sehemu ya kulima. Ila ninamshukuru Dada Rhobi Samwelly, ambaye amenileta hapa nyumba salama ya Hope for Girls and Women Tanzania," anasema.

Anasema jukumu lake katika nyumba hiyo, ni kufundisha mila na desturi za kabila lake na anapewa posho kidogo, inayomuwezesha aendelee kuishi mjini, wakati akitafuta njia za ziada.

"Pamoja na matatizo yote ninayokumbana nayo baada kuacha ukeketaji, siwezi kurudia kazi hiyo. Badala yake ninayageuza matatizo hayo kuwa fursa ya kupiga hatua kwenda mbele," anasema.

Muhabe anaanza kusimulia kwamba, amezaliwa katika familia ya watoto 14, yeye akiwa wa tatu. Pia, wapo wengine 10 waliozaliwa na mke wa pili wa baba yao.

Anasema, alisoma Shule ya Msingi Kibeyo na kuhitimu mwaka 1987. Mwaka uliofuata alikeketwa na kisha mwaka 1990 akaolewa na kubahatika kupata watoto saba wote wa kiume, lakini walio hai sasa ni watatu.

"Lakini nilishaachika baada ya kukumbana na manyanyaso katika ndoa yangu.Kwa sasa ninaishi mwenyewe nikiendesha maisha yangu, ingawa kama nilivyosema yana changamoto nyingi," anasema.

Aidha, anasema jina la Muhabe alilopewa ni la bibi yake mzaa baba, ambaye alikuwa anafanya kazi ya ukeketaji, hivyo naye alipewa jukumu hilo, ambalo alilifanya mara moja tu na kuliacha kabisa.

ALIANZAJE UNGARIBA?

Muhabe anasema, alianza kazi ya kukeketa mwaka 2016 na kisha akaacha kazi hiyo na kukumbana na vitisho kutoka kwa familia na wazee wa mila, vikiwamo kwamba atakutwa na mambo mabaya kwa kukiuka mila ya kikurya.

Ngariba huyo mstaafu anasema, aliamua kuziba masikio na kumtegemea Mungu na ameweza kuvuka vikwazo hivyo ingawa kinachomsumbua sasa kukosa sehemu ya kulima ili aendeshe maisha yake kwa uhakika.

"Dada Rhobi wa Hope for Girls and Women Tanzania ananisaidia, lakini pia ni muhimu kuwa na kitu changu mwenyewe cha kuniwezesha kuendesha maisha yangu ya kila siku," anasema.

Ngariba hiyo anasema, vitisho haviko kwake tu bali hata wale wanaotoa elimu ya kupinga ukeketaji nao wanakumbana navyo, kwa vile wanagusa maslahi ya wanaofaidika na ukatili huo.

OMBI LAKE

Anasema, jambo la kwanza ni kuwataka ngariba wengine wanaoendelea kazi hiyo waache mara moja na kuungana nayo katika vita ya kupinga ukeketaji kwa ajili ya kunusuru maisha ya watoto wa kike.

"Ninasema hivyo kwa sababu uhai wa binadamu ni muhimu kuliko fedha, na pia wazee wa kimila waache kutisha watu wanaokataa kukeketa au kukeketwa kwamba kuna madhara watapata, huo ni uongo," anasema.

Mubabe anawaomba wadau wote wanaojishughulisha na kupinga vitendo vya ukeketaji, wawasaidie ngariba wote walioachana na ukeketaji kwa hali na mali, ili waweze kujikimu kimaisha.

"Binafsi ningesaidiwa kupata mtaji ili niweze kufanya biashara ndogo hapa mjini Mugumu, huku nikiendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara ya mila potofu zikiwamo za ukeketaji," anasema.

Anasema, anamhurumia Rhobi Samwelly, ambaye amekuwa akimpa posho inayomsaidia kuendesha maisha, lakini akipata msaada zaidi kutoka kwa wadau wengine, atakuwa na uhakika kumudu gharama za maisha.

"Ninasikia kuna mashirika huwa yanawasaidia fedha za biashara, ngariba wanaoacha kazi hii, niwaombe kama wapo wanione hata mimi ambaye niko hapa nyumba salama ya Hope for Girls and Women Tanzania," anasema.

Muhabe anasema, ameamua kutokuwa miongoni mwa watu wanaosababisha madhara kwa watoto wa kike, kwa vile ameshaelimishwa na kutambua kile ambacho kinawakuta watoto wanaokeketwa.

"Bahati nzuri mimi nilipokeketa, hakuna binti aliyepoteza maisha kwa kutokwa na damu nyingine bali wote walisalimika, hivyo ninashukuru nimeacha kazi hiyo mikono yangu ikiwa salama," anasema.

"Ninajua kuna vitisho ambavyo umekuwa ukikutana navyo, katika vita hii, wewe endelea usikate tamaa, serikali inaunga mkono juhudi zako na inataka vitendo vya ukeketaji vikomeshwe kwenye jamii," anasema.

Habari Kubwa