Yanga isivyo na bahati mbele ya Waarabu

27Jun 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga isivyo na bahati mbele ya Waarabu

WAKATI kesho ikitarajia kupambana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DR, Yanga ilichapwa bao 1-0 na Mo Bejaia ya Algeria ikiwa ugenini.

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga haijawahi kuitoa kwenye mashindano ya klabu Afrika timu yoyote kutoka Uarabuni.

1. Yanga 1-6 Al Ahly-1982
Mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilikung’utwa 5-0 nchini Misri, kabla ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 6-1 mwaka 1982.

2. Yanga 0-4 Al Ahly-1988
Mwaka 1988, Yanga ilicheza mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa mara nyingine na Al Ahly na katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, timu hizo hazikufungana, kabla ya Yanga kulala 4-0 ugenini.

3. Yanga 1-2 Ismailia-1992
Yanga ilicheza tena Ligi ya Mabingwa ikiwa ni raundi ya kwanza dhidi ya Ismailia ya Misri mwaka 1992.
Mechi ya Dar es Salaam Ismailia ilishinda 2-0 na mechi ya marudiano Yanga ilikomaa na kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.

4. Yanga 3-9 Raja Casablanca-1998
Mwaka 1998 Yanga ilifanikiwa kuingia kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi B sambamba na Raja Casablanca ya Morocco. Katika mechi ya kwanza ugenini, Yanga ilichapwa 6-0, kisha sare ya 3-3 Dar es Salaam.

5. Yanga 1-5 Zamalek-2000
Yanga ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Zamalek mwaka 2000 Kombe la Shirikisho Afrika Dar es Salaam, kabla ya kufungwa 4-0 nchini Misri.

6. Yanga 0-3 Esperance-2007
Ilifungwa 3-0 ugenini na Esperance ya Tunisia raundi ya pili Kombe la Shirikisho, kabla ya kulazimisha sare ya bila bila Dar es Salaam.

7. Yanga 1-2 Al-Akhdar-2008
Yanga ilikutana na Al-Akhdar kutoka nchini Libya mwaka 2008 raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).
Mechi ya kwanza ilichezwa nchini Libya na kufungwa bao 1-0, kabla ya sare ya 1-1 mechi ya marudiano.

8. Yanga 0-4 Al Ahly-2009
Mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2009, Yanga ilipokutana tena na Al Ahly ikafungwa 3-0, kabla ya kufungwa bao 1-0 katika mechi ya marudiano.

9. Yanga 1-3 Al Ahly-2011
Mwaka 2011,Yanga ilikutana na Al Ahly ya Misri. Katika mchezo wa kwanza ugenini Cairo, Yanga ililala 3-0, kisha ikalazimisha sare ya 1-1 nyumbani.

10. Yanga 1-2 Zamalek-2012
Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho 2012 na kukutana na Zamalek, iliyotoka nayo sare ya 1-1 Dar, kabla ya kufungwa 1-0 ugenini.

11. Yanga 3-4 Al Ahly-2014
Ligi ya Mabingwa 2014, Yanga ilicheza tena dhidi ya Al Ahly na kuifunga 1-0 nyumbani, kisha kupoteza kwa idadi kama hiyo ugenini. Hata hivyo iliyolewa kwa mikwaju ya penalty 4-2.

12. Yanga 1-2 Etoile du Sahel-2015
Mwaka jana, 2015, Yanga ilikwaana na Etoile du Sahel katika hatua ya 16 bora na ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1. Ililazimisha sare ya 1-1 nyumbani na kupoteza ugenini 1-0

13. Yanga 2-3 Al Ahly-2016
Ilikuwa ni mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Yanga ilipotoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri na kuchapwa mabao 2-1 ugenini.

14. Yanga 0-1 Mo Bejaia-2016
Mechi hii ilichezwa usiku wa kuamkia Jumatatu Juni 20 nchini Algeria, Yanga ilipopokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mo Bejaia kwenye mechi ya kwanza ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa