YISHUN-SINGAPORE:Mji uliojaa paka kila kona,anayewadhuru anaishia jela

16Jun 2016
Peter Orwa
Nipashe
YISHUN-SINGAPORE:Mji uliojaa paka kila kona,anayewadhuru anaishia jela

KILA jiji linaelezwa kuwa na tofauti ya aina yake. Katika katika jiji la Yishun nchini Singapore, taifa lenye uchumi wa kati na linaloundwa na visiwa 63, kunaelezwa kuwapo utitiri wa paka wanaofika 600.

Paka hao wana tofauti zao, kwamba licha ya kuwa ‘paka pori,’ wamekuwa marafiki wa wakazi wengi wakiwapatia mahitaji muhimu ya chakula kama wanavyofanya kwa ombaomba.

Lakini paka hao katika sura ya pili, nao wamejenga urafiki mkubwa na wanadamau wanaokutana nao mitaani.

Hata hivyo, kuna matukio yasiyoridhisha kwamba kuna wahalifu ambao hutumia mwanya kuua paka hao, jambo linaloonekana kuikera sana serikali na wanaharakati wa jinsia.

Paka hao wamebatizwa majina “paka wa jamii.” Mara nyingi wakazi wa jiji hilo hutumia huwapelekea vyakula na maji paka hao wa mitaani na imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, baadhi wakiwaita ‘mjomba’ na ‘shangazi.’

Hicho ndicho kinachofanywa mara nyingi na wafanyakazi nyakati za kutoka na kuingia kazini.

“Paka hawa ni wa kipekee sana,” anatamka mmoja wa wakazi wa Yishun na anaeleza tabia yao akisema: ”ananifahamisha alipo na ninapoondoka ananifuata kunisindikiza.”

“Ni kweli rahisi kuwa na paka anayeitwa ‘Chungwa’ hutukimbilia tunapotembea usiku.”

Anaongeza:”Kama unaweza kumtunza paka mmoja kila usiku, inatosha."

MAUAJI YA PAKA

Pamoja na kuwapo urafiki huo baina ya wakazi wa Singapore na ‘paka wa jamii’ kuna mambo ambayo ni kinyume na ustawi wao.

Kuna watu wanaoendesha ukatili wa kuwaua wanyama hao saa za usiku, kitendo kinachodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana na ndio habari zilozotawala kila mahali kwa wiki kadhaa, ikiwamo kwenye vyombo vya habari.

Ingawaje hakuna takwimu kamili za kisanyansi, hadi sasa kuna paka 39 wanaodaiwa kuuawa kinyama na watu wasiojulikana.

Wanaowapenda paka hao wamekuwa wakieleza kusikitishwa na vitendo hivyo wakivitafsiri ni vya kinyama.

Mamlaka ya Vyakula na Wanyama (AVA) ya nchini Singapore, inaunga mkono hoja hiyo kwa kueleza kwamba mauaji hayo ya paka wa Yishun yanafanyika kwa makusudi.

Taarifa ya AVA inasema katika idadi hiyo ya vifo vya paka 39, kati yao 13 ambao ni asilimia 33, inatokana ajali za barabarani na waliobaki vifo vyao vinatokana na mazingira tata.

Hivi sasa mamlaka za dola nchini humo zimeigia kazini kuwasaka wahalifu wanaosababisha vifo hivyo vya paka.

Mbunge wa jimbo la Yishun ambako paka wanauawa sana, Louis Ng, anasema mtihani mkubwa uliopo na unawakwamisha ni kukosekana ushahidi kuhusiana na mauaji hayo.

"Huwezi kupata alama za vidole kwa paka. Pia humjui mrithi wake na kuna watu wachache unaweza kuwahoji,” anasema mbunge huyo ambaye yuko mstari wa mbele katika kuwasaka wahalifu husika.

Hadi sasa kuna watu wawili wanaoshikiliwa kutokana na mauaji hayo ya paka, mmoja shauri lake liko kizimbani na mwingine alishahukumiwa kifungo cha miezi 18.

Mhusika alikiri kosa kwamba alimrusha paka huyo kutoka ghorofa la 13.

DORIA YA KULINDA PAKA

Ni saikolojia ya ajabu lakini ndio ukweli ulikosimamia. Mkazi mmoja wa jiji hilo anasema amekuwa akifanya doria kila siku baada ya kufanya kazi ya mchana kutwa, kukagua kama kuna paka yeyote katika ya anaowajua ametoweka.

Anasema amekuwa akifanya hivyo bila ya hata kufahamisha familia yake na watu wengine anawajua, kwamba itakuwa vigumu kwao kumuelewa.

“Si kwamba kila mtu atanielewa,” anasema na kuongeza: “lakini inatokana na utashi wangu kwa paka hao.”

Anasema ana mtandao wake wa watu wanaowalinda paka na iwapo anagundua kuna paka aliyetoweka, huwataarifu haraka kuanzisha msako.

Kila paka anayemjua amempa jina, kwa mfano Bushy, ambaye amepewa jin a hilo kutokana na kuwa na mkia mrefu na baadhi ya paka wamekuwa marafiki wake wa karibu, kila wanapomuona wanamsogelea kulala karibu na kumcgezea miguuni.

KESI YA MAUAJI YA PAKA

Inaelezwa kwamba, kulikuwapo kasi kubwa ya mauji ya paka tangu Desemba mwaka jana na ndani ya miezi mitatu tangu kipindi hicho, takwimu rasmi zinaonyesha paka 17 walishauawa, idadi inayoelezwa ni kubwa sana.

Mbali na hao waliouawa, kuna wengine 17 wanaoelezwa kujeruhiwa vibaya sana

Mtuhumiwa Lee Wai aliyehukumiwa kifungo cha miezi 18, alifikishwa mahakamani akituhumiwa kufanya ukatili dhidi ya wanyama, kupitia sheria inayokataza ukatili kwa wanyama na ndege.

Katika shitaka hilo ambalo Lee alikiri kulitenda na kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo na mahakama, mamlaka hiyo iliagiza akapiwe akili katika Taasisi ya Afya ya Akili (IMH), ili kujiridhisha kama yuko sawa kiakili.

Miongoni mwa walioshabikia na kufuatilia kwa karibu kesi hiyo, ni wanaharakati wa Kundi la Ustawi Paka wa mjini Yishun, wanaoamini itakuwa nafuu kwao kwa wanayemuamini mmoja wa wauaji maarufu wa paka, kuhukumiwa.

Katika kipindi hicho ambacho kasi ya mauaji ya paka imechachamaa, wanaharakati waliunda kikosi kazi cha kujitolea, kilichoamua kufanya doria usiku kulinda usalama wa paka wao vipenzi na kuwaska kwa hali na mali.

Miongoni mwa wadau muhimu katika doria hiyo ni mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Waokoaji Wanyama, ni miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele katika doria.

Huko nyuma mwezi Desemba, alitoa wito kutaka mamlaka husika, kufanya kila kinachowezekana kuwatia mbaroni wauaji hao wa paka.

“Tumedhamiria kuhakikisha haki inatendeka,” alitamka mbunge huyo katika tukio moja la mwishoni mwa mwaka jana, walipomkuta paka amekufa na akielea katika dimbwi la maji bondeni.

Wanaharakati hao wanaishangaa Mamlaka ya Kilimo na Mifugo katika kushindwa kulitatua suala hilo kama inavyo stahili.

Katika mkutano wa waandishi wa habari kati ya mbunge, Chama cha Ustawi wa Wanyama (CWS), na wanaharakati wa kunusuru paka walitaka kuwapo ushahidi unaojitosheleza kufanikisha mashitaka.

Hata hivyo, wanalalamika ukosefu wa ushahidi kuwa walakini unaowakabili katika kufanikisha mashitaka mahakamani dhidi ya wakosaji.

“Kunahitajika ushahidi wa kutosha kutoka kwa Polisi, kuliko ushahidi wa video,” anasema mjumbe mmoja wa mkutano huo.

“Pia kila mmoja kutoka juu anapaswa kukusanya ushahidi kwa kiasi kingi,wanyama waliokufa wanapoondolewa na wafagiaji na makandarasi na kuna mashuhuda wa uhalifu husika,” anasema.

Katika matukio mengi ya mauaji ya paka, kwa kiasi kikubwa walitupwa kutoka sehemu za juu na kuathirika vibaya kupata majeraha ya kichwani, machoni, mguuni, kwenye tumbo na mgongoni.

“Hii ni kwa mara ya kwanza kumekuwapo utashi wa hali ya juu, kwamba mbunge, Polisi na AVA wanashirikiana na rasilimali zao. Huu ni ushirikiano mpya,” anatamka mjumbe wa mkutano huo.

Anaongeza:“Naamini kwamba hii itakuwa itifaki ya pamoja katika muda mmoja. Ni katika hatua ya kipekee kwamba Polisi na AVA wanachangia rasilimali, utaalamu, na ufahamu wa masuala yanayohusu ujangili wa wanyama.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyama na Ndege, mtu anayeenda kinyume na sheria hiyo, ama anatiwa kifungoni kwa miezi isiyozidi 18 au faini ya Dola za Marekani 15,000 (Zaidi ya Sh. milioni 32) au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Habari Kubwa