Ziara ya Rais Magufuli ilivyoacha neema Pwani Wananchi vicheko vitupu

28Jun 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es salaam
Nipashe
Ziara ya Rais Magufuli ilivyoacha neema Pwani Wananchi vicheko vitupu

ZIARA ya siku tatu ya Rais John Magufuli katika Mkoa wa Pwani, imeacha neema kwa wananchi wa maeneo mbalimbali katika mkoa huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (wa kwanza Kushoto), kuhusu matumizi ya gesi katika Kiwanda cha Vigae cha Good Will wakati waziara yake mkoani humo. PICHA: MTANDAO.

Ziara hiyo iliyoanza Juni 20 hadi Juni 22, mwaka huu ilikuwa ni ya neema kwa wananchi wa mkoa wa Pwani kutokana na pale alipokuwa anapita aliwaacha wakazi wa eneo husika wakifurahi.

Baadhi ya neema hizo ni pamoja na kuwapatia wananchi wa mizani wilayani Bagamoyo eneo la ekari 65 baada ya wananchi hao, kujitokeza mbele yake wakiwa na mabango yanayolalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa na Magereza ikiwa ni pamoja na kufukuzwa katika eneo hilo.

Neema nyingine ni kumwagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa, na wilaya, kuhakikisha kuwa wanachukua hatua dhidi ya watu wote ambao walishiriki kuiba fedha za pembejeo na kuwaacha wananchi wanyonge wakihangaika.

Pia, aliwaahidi wakazi wa Pwani kuwajengea bandari kavu eneo la Ruvu ambayo itakuwa ikipitisha mizigo ya nchi jirani.

Rais Magufuli hakuishia hapo tu katika ziara hiyo, bali alizundua viwanda vikubwa vitatu pamoja na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam.

Akiwa ziarani mkoani humo, Rais Magufuli pia aliweza kununua dawa za kuzuia malaria kwa gharama ya Sh. bilioni 1.3 akiwa kwenye kiwanda cha viuatilifu ambavyo ni maalumu kwa ajili ya kuzuia mazalio ya mbu na kuwaagiza wakurugenzi wote wa wilaya kuhakikisha wanakwenda kuchukua dawa hizo kwa ajili ya kuulia mazalia ya mbu.

Hizo ni baadhi tu  ya neema ambazo Rais Magufuli amewaachia wananchi wa mkoa wa Pwani alipofanya ziara ya siku tatu, lakini mbali na neema hizo pia aliwashukia wananchi wanaounga mkono wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari wanaopata mimba kwa kusema kuwa katika utawala wake hakuna mwanafunzi wa kike atakayepata mimba kisha aendelee na masomo.

Awapa wananchi eneo la Magereza:

Rais Magufuli akiwa mjini Bagamoyo wakati wa uzinduzi wa barabara ya Msata-Bagamoyo yenye urefu wa kilomita 64, alitangaza kuwapa wananchi eneo la Magereza la ekari 65  baada ya wananchi wa eneo hilo kujitokeza na mabango wakimuomba  kuwatatulia mgogoro kati yao na Jeshi la Magereza.

Baada ya kujitokeza kwa mabango, Rais Magufuli alitoa ruhusa ya mama mmoja kuzungumza kwa niaba ya wenzake na ndipo mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Asma Msigale akatoa kilio chao.

Mama huyo alisema “Sisi tumekaa hapa kwa miaka mingi, lakini sasa tunafukuzwa na Magereza wanasema ni eneo lao, tunakuomba sana Rais utuonee huruma, sisi baadhi ni wajane tunatumia eneo hii kwa ajili ya kilimo na kusomeshea watoto wetu, tunaomba watuachie tuendelee kulima,” alisema mwanamke huyo.

Baada ya ombi hilo, Rais Magufuli alimwita Mkuu wa Magereza na kumuuliza wanaukubwa wa eneo gani; Mkuu huyo wa Magereza akajibu wana ukubwa wa ekari 6,186.25 “Mkuu lile eneo lilikua na ukubwa wa ekari 75, tumetoa ekari 15 tukawapa halmashauri kwa ajili ya machinjio na zimebaki ekari 65”.

Kutokana na majibu hayo, Rais Magufuli alisema “Sasa  nyie mna eneo kubwa hata hamlimi lote, naagiza hizo ekari 65 ni kidogo sana, waachieni hawa wananchi wazimiliki, na kuanzia leo zitakua za kwako.”
Uzinduzi wa viwanda vitatu:

Kadhalika, Rais Magufuli akiwa mkoani humo aliweza kuzindua viwanda vikubwa vitatu ambavyo ni kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Tanzania Ltd kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 kwa siku kwa ajili ya kuhifadhia mazao.

Pia, Rais Magufuli alizindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400 aina ya Ursus ambao utagharimu Sh. bilioni 55 na matrekta hayo yatasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo, mradi ambao unamilikiwa na serikali kwa asilimia mia.

Rais Magufuli alizindua kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group kilichopo Mlandizi ambacho kwa awamu ya kwanza kinauwezo wa kuzalisha tani 500,000 za nondo kwa mwaka wa pili  na awamu ya pili kitaongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni 1.2 kwa mwaka.
Ufisadi wa Pembejeo:

Rais Magufuli alisema kwa sasa anajiandaa kuchukua hatua kwa mafisadi ambao walitumia vibaya fedha za pembejeo wa kuandikisha watu ambao tayari walishakufa ili mradi waibe fedha hizo.

Alisema anajua miongoni mwa watu waliofanya ufisadi huo ambao ni viongozi wa wilaya na mikoa.

“Mtu anaandikisha maiti, sijui walikuwa wanatoka kaburini kuja kuchukua pembejeo alafu wanarudi kaburini,” alisema Rais Magufuli.
Dawa za Malaria:

Kwenye ziara hiyo akiwa kwenye kiwanda cha viuatilifu ambavyo ni maalum kwa kuzuia mazalia ya mbu, Rais Magufuli alisema dawa hizo zimejaa kiwandani hapo, lakini watendaji wa Wizara ya Afya wamejikita kwenda kununua dawa za kutibu malaria Ulaya, wanaacha kununua dawa za kuzuia malaria ambayo lita moja inauzwa kwa Sh. 13,000 tu.

Alisema iwapo Wizara ya Afya ingetumia dawa hizo kuangamiza mazalia ya mbu, ndani ya miaka mitano ugonjwa wa malaria ungetokomea.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alinunua dawa hizo kwa Sh. bilioni 1.3 na kuwataka wakurugenzi wote wa wilaya kuhakikisha wanakwenda kuchukua dawa hizo kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Uzinduzi wa barabara na mradi wa maji:

Rais Magufuli akiwa ziarani mkoani humo, aliweza kuzindua barabara ya Bagamoyo-Makofia-Msata yenye urefu wa kilomita 64 iliyojengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 169.

Barabara hiyo inauwezo wa kudumu kwa miaka 20 iwapo magari yatakayoitumia hayatazidisha uzito wa tani 56.

Rais Magufuli alisema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inapita maeneo ambako itajengwa bandari mpya ya Bagamoyo, alisema barabara hiyo itafungua fursa nyingi za kiuchumi kutoka maeneo ya Pwani kwenda maeneo ya Kaskazini na maeneo mengine ya nchi.

Kadhalika,Rais Magufuli akiwa Mlandizi mkoani Pwani alizindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu ambao utaongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha, Mlandizi na Bagamoyo.

Habari Kubwa