Zidane anavyojua kujitengenezea masika yake Real

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Zidane anavyojua kujitengenezea masika yake Real

MOJA ya kosa kubwa ambalo wengi huwa tunalifanya ni pale tunapojisahau na kuamini kuwa furaha zetu hutegemea kitu au mtu.

Yaani bila mtu au kitu fulani ni ngumu kwetu sisi kupata furaha. Hapo ndipo hatua ya kwanza ya maumivu inapoanzia.

Hapo ndipo palipo na chimbuko la maumivu ndani yake. Maisha ni furaha, hiki ndicho tunachotakiwa kukijua.

Tunatakiwa kuishi maisha yenye furaha ndani yetu. Na furaha siku zote hutengenezwa na mtu mwenyewe. Hakuna furaha ambayo mwanadamu yeyote hutengeneza kwa ajili ya mwanadamu mwingine.

Na kama ipo hiyo itakuwa furaha ya muda mfupi na siyo furaha ya muda mrefu. Kipi unakitafuta katika maisha yako? Furaha inayoyeyuka au furaha inayosimama kama mwamba?

Hili ni swali muhimu sana. Swali ambalo huja na mwongozo sahihi wa kupata furaha. Furaha ya dhati hupatikana kwenye mikono ya mhusika mwenyewe.

Ndiyo maana tunashauriwa sana kujifunza kutafuta furaha. Hapa ndipo ambapo tunapokuja kuona namna ambavyo Zinedine Zidane alivyo na uwezo mkubwa wa kujitafutia furaha.

Anapenda kuishi kwenye furaha, anapenda kuishi kwenye sehemu ambayo kuna masika. Masika ambayo yanaweza kumsaidia kwenye kilimo chake.

Anajua kabisa jinsi ya kujitengenezea mazingira ya masika, anajua kabisa kujitengenezea mazingira ya kumpa furaha.

Yaani kwa kifupi anajua kutengeneza furaha kwa mikono yake mwenyewe. Wakati anachaguliwa kuwa kocha wa Real Madrid alifanikiwa sana na timu hii.

Alibeba Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mara tatu mfululizo. Alikuwa na kikosi imara sana. Kikosi ambacho kilikuwa na Cristiano Ronaldo.

Mwanadamu ambaye alikuwa anafunga mabao kuanzia 50 ndani ya msimu mmoja. Kwa hiyo wakati yupo Real Madrid alikuwa na uhakika wa timu yake kupata mabao 50 kupitia mtu mmoja tu!

Alikuwa na wapishi mahiri wa mabao, Toni Kroos alikuwa mpishi bora sana. Luka Modric alikuwa mhimili mkubwa sana ndani ya kikosi cha Real Madrid.

Akamtengeneza Casemiro kuwa kiungo bora wa eneo la kuzuia. Sergio Ramos alikuwa beki imara.

Beki ambaye alikuwa anauwezo mkubwa wa kuyalinda mabao na alikuwa na uwezo wa kuyafunga pia hayo.

Unamkumbuka Marcelo? Beki ambaye alikuwa na sifa nyingi sana za kuwa mshambuliaji?

Huyu alikuwapo kwenye kikosi chake na akamfanya kuwa beki ambaye alikuwa anatengeneza nafasi nyingi za mabao yeye pamoja na Dani Carvajal.

Lakini taratibu hali ya dalili ya kiangazi ilianza kuonekana katika klabu ya Real Madrid, Ronaldo aliondoka.

Toni Kroos na Luka Modric wakawa wameshuka kiwango. Vivyo hivyo kwa Dani Carvajal na Marcelo.

Dalili za kupata Real Madrid ambayo ni dhaifu zilianza kuonekana. Ndipo hapo Zinedine Zidane alipoamua kujitoa taratibu na kupumzika kwa muda.

Akaiacha Real Madrid dhaifu, Real Madrid ambayo kwa hivi karibuni imefungwa mechi tano mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani zikiwamo mechi mbili dhidi ya Barcelona.

Real Madrid ambayo imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na Ajax kwa kufungwa katika uwanja wao nyumbani.

Ni Real Madrid ambayo iko nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) ikiwa nyuma kwa alama 12 kutoka timu inayoongoza ligi hiyo.

Msimu umekaribia kuisha, Zidane anarudi tena Real Madrid. Anarudi kipindi ambacho watu wengi hawatamhukumu kwa matokeo haya ya mwishoni.

Kitu kizuri kuwa tunaenda kuingia katika dirisha kubwa la usajili, dirisha ambalo litampa nafasi yeye kusajili wachezaji nyota ambao atatembea nao.

Tayari amekuja kipindi ambacho anauwezo wa kujitengenezea masika yake. Kipindi ambacho anauwezo wa kujitengenezea furaha yake mwenyewe.

Kipindi ambacho ana uhakika wa kuingia sokoni kumchukua Mbappe, Neymar, Hazard kwa ajili ya kuendelea kutengeneza Ufalme wake pale Santiago Berbaeu, hebu tusubiri tuone!

Habari Kubwa