Zimbabwe wasusia ‘send-off’ kueleka Afcon 2017

09Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
HARARE, Zimbabwe
Nipashe
Zimbabwe wasusia ‘send-off’ kueleka Afcon 2017

SHEREHE ya kuiaga timu ya Taifa ya Zimbabwe, imeingia ‘kirusi’ baada ya wachezaji kuisusia wakitaka kwanza walipwe chao mapema.

Willard Katsande.

Timu hiyo ilikuwa iagwe Jumamosi usiku tayari kwa safari ya kuelekea Cameroon kucheza mechi ya kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika [Afcon 2017] itakayoanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki Gabon.

Wachezaji hao wa ‘The Warriors’ Ijumaa waligoma kuhudhuria chakula cha usiku kwa ajili ya kuagwaa ‘send-off dinner’ na Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Nyota hao walitaka kwanza kulipwa fedha zao walizoahidiwa endapo watafuzu michuano hiyo, pamoja na kila mmoja kulipwa Dola za Marekani 5,000 kwa kila mechi watakayocheza katika fainali hizo huko Gabon.

Lakini Chama cha Soka Zimbabwe (Zifa) kimeripotiwa kuwa tayari kutoa ofa ya pauni 2,500 kwa kila mechi.
Nahodha wa Warriors hao, Willard Katsande aliiambia Star FM Zimbabwe kuwa, licha kuwapo kwa mgogoro huo, timu hiyo haitasusia michuano hiyo.

"Ni wazi tutakwenda kucheza, lakini ni kuhusu suala la kujadili, ukichukulia tunastahili mazuri," alisema.

"Hatujaomba kiasi kikubwa, tunajua tunachokihitaji kama timu, tumewasilisha mapendekezo yetu, lakini hakuna aliyeyajali."

Hata hivyo, Zifa imeomba msamaha kwa kilichotokea "kwa washikadau wote wa soka Zimbabwe na zaidi Makamu wa Rais," na kuongeza kuwa "hali hiyo iliyojitokeza kwa timu ni aibu kwa taifa zima."

Habari Kubwa