Zingatia haya unaponunua mapambo mitandaoni

13Aug 2016
Vivian Machange
Nipashe
Zingatia haya unaponunua mapambo mitandaoni

ZAMA hizi za dijitali zinaibua mengi mojawapo ni hili, kwa wengi walioko mijini kununua bidhaa mitandaoni kunaibuka kwa kasi.

Biashara mtandaoni au ‘e-commerce’ imewarahisishia wanunuzi wengi wasio kuwa na muda au uvumilivu wa kuzunguka kwenye maduka mitaani kusaka na kununua bidhaa mbalimbali , kama mapambo ya nyumbani, ambayo nataka kuyazungumzia.

Uwepo wa mitandao kama instagram, facebook, whatsapp pamoja na tovuti website umechangania kurahisisha manunuzi mitandaoni ambao unahusisha kununua na kuletewa ulipo.

Hata hivyo, kila kitu kina changamoto zake na hapa nimekuandalia mambo saba muhimu ambayo unatakiwa kuyazingatia unapoamua kununua mapambo ya nyumbani mitandaoni.

La muhimu ni kulinganisha bei kwa wauzaji zaidi ya mmoja. Unapokuwa unalinganisha bei ya bidhaa hiyo hiyo kwa wauzaji zaidi ya mmoja kuna uwezekano mkubwa wa kuikuta ikiwa ya chini kwa muuzaji mwingine. Hii itakusaidia mwishoni kupata dili nafuu.

Nunua kwa muuzaji mwenye bidhaa nyingi kwani biashara nyingi hazikosekani wachuuzi kwa hivyo pendelea kununua kwa wenye mali na sio mchuuzi. Unaponunua kwa mwenye mali kuna uwezekano mkubwa wa kunufaika kama vile kubadilisha bidhaa na kuchukua nyingine endapo hutazipenda au zina kasoro kadhalika inawezekana kupata punguzo la bei.

Ulizia vipimo halisi:Sio wauzaji wote wa mitandaoni wanafahamu kikamilifu bidhaa wanayouza. Kwa kawaida mitandaoni tunanunua kwa kuona picha, na huwa mara nyingine zinadanganya. Hakikisha muuzaji anakupa vipimo halisi vya bidhaa unayotaka kununua. Hakuna kitu kinaudhi kama kununua kitu mfano, shuka au picha ya ukutani halafu ukaja kukuta kuwa haina ukubwa wa kukidhi hitaji lako.

Kuwa makini na rangi:Usiwe na mazoea ya kuamini rangi ya picha unayoona mtandaoni kwani inawezekana kabisa ikawa siyo halisi. Usishangae kuletewa bidhaa ya rangi tofauti na uliyotegemea kwa hivyo ni muhimu kujiandaa kwa hali hiyo endapo itatokea ufanyeje. Unaweza kumtaka muuzaji akuthibitishie rangi kabla hujanunua.

Hakikishiwa kuwa unaweza kurudisha bidhaa usiporidhika.Pambo fulani linaweza kuonekana kuwa na mvutio wa kipekee mtandaoni, hata hivyo ukajikuta kuwa hujalipenda kwa uhalisia wake. Kama umenunua kwa muuzaji ambaye haruhusu kurudisha utapoteza hela yako.

Fahamu malighafi iliyotengenezea bidhaa:Mathalani, bidhaa nyingi za mbao ngumu ni gharama sana. Unapotaka kununua mapambo kama meza ya kahawa au kabati la runinga hakikisha kuwa hufanyi uamuzi kabla ya kufahamu malighafi iliyotumika kutengenezea bidhaa hiyo.

Pata taarifa za maingizo mapya:Huenda hujapenda bidhaa zilizopo kwa sana, ila uzuri ni kwamba karibia kila mtandao una jinsi ya kumjulisha mfuatiliaji pale kunapowekwa ingizo jipya. Kama unapendelea kufahamu kinachoendelea kwenye ulimwengu wa mapambo ya nyumbani basi jiandikishe kwenye mitandao hiyo ili uhabarike kila wanapoweka ingizo jipya.

Kununua mapambo ya ndani mitandaoni inaweza kukurahisishia maisha kwani unaletewa hadi mlangoni. La muhimu ni msomaji wangu usisahau kuzingatia dondoo hizi.

Zaidi www.vivimachang e.blogspot.com

Habari Kubwa