Zulia pambo unalolistahili

16Mar 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Zulia pambo unalolistahili

MAZULIA ya nyumbani ni muhimu katika kuweka sura inayovutia ndani ya nyumba. Iwe vyumbani au sebuleni.

Japokuwa siyo lazima sana kuweka ndani ya nyumba, lakini zulia lina umuhimu mkubwa katika kuongeza mvuto kutegemea ubora na viwango vya pambo hilo.

Mazulia haya yanaweza kuwekwa katika makundi tofauti. Mosi kuna mazulia makubwa ya kutandika katika sebule nzima, ya kati ya kutandika katika eneo la kuketi tu na vipande vidogo ambavyo vitupiwe eneo mpambaji analotaka.

Mbali na hayo, yapo mazulia ya kuweka mlangoni au pembeni ya kitanda, kwenye verenda, bafuni na chooni.

Katika utandikaji huo tuangalie eneo moja la namna ya kuweka zulia kubwa.

Hatua ya kwanza ya kutandika zulia ni kuhakikisha kwamba sehemu linapotandikwa ni safi na baada ya kutandikwa ndipo zinaweza kupangwa samani mbalimbali juu yake.

Ni vema kuzingatia ukubwa wa zulia lenyewe na linapotandikwa endapo ni katika sehemu ya chakula au sehemu ya sebule kuhakikisha kwamba samani kama viti, meza, stuli na mapambo mengine vinalingana na ukubwa wa zulia lenyewe.

Na kama unaweka mazulia mawili katika sehemu moja yaani kubwa na dogo la kutupia kwa juu ni vema kuwa makini kuhakikisha la juu lisizidi la chini.

Na ni vizuri kuchagua zulia lenye rangi zinazoendana na mapambo mengine ya chumba au sehemu unapotaka kuliweka.

Si lazima lifanane na mapambo yote lakini angalau baadhi ya rangi zilizopo zilandane ili kuleta mfanano.

Yapo makosa mbalimbali ambayo ni vyema kuyaepuka kuhusiana na mazulia ya nyumbani.

Mojawapo ni kuepuka kuchagua zulia dogo ambalo halilingani na eneo unalokusudia kuliweka badala yake unatakiwa kuweka mipango sawa ili unaponunua lisiwe dogo na kulazimika kununua tena. Au pia lisiwe kubwa ili kuepusha kulikatakata.

Mfano unapolibandika sebuleni, ni sehemu inayohitaji kuwa na zulia kubwa la kutosha kwa kuhakikisha kwamba miguu yote ya sofa na samani nyingine zinakuwa juu yake.

Ni imani yetu kuwa eneo la sebule ndilo hutumika sana kwa watu kufanyia maongezi, kwa hiyo inatakiwa kuwa na ukubwa wa kutosha kiasi kwamba miguu ya mbele ya sofa na hata ile ya nyuma ikanyage juu ya zulia na wenye kukaa nao wakanyage juu yake.

Ni vema kuepuka kununua zulia lisilo na muundo wa chumba au eneo unalotaka kutandika.

Kwa mfano endapo chumba kina muundo wa duara, ni vema pia zulia litakalotumika kutandika liwe na umbo la namna hiyo.

Ni vizuri kuepuka kuweka zulia tofauti na hilo kwa sababu linaweza lisienee au kuwa na utulivu badala yake linaweza kwa limevimbavimba na hata kuharibu mwonekano mzuri wa nyumba yako.

Kadhalika kwa chumba chenye pembe nne, nacho kitahitaji kuwa na zulia la muundo huo.

Endapo chumba ni kirefu zaidi na chembamba unaweza kununua zulia la kukata kwa kuzingatia mpangilio mzuri wenye vipimo kulingana na namna unavyopanga kuweka eneo lako.

Epuka kuacha zulia la kufunika ukuta kwa ukuta bila vitupio.

Endapo umeweka zulia la kufunika ukuta kwa ukuta la rangi moja ni vizuri ukatupia mazulia madogo madogo ili kukivuta chumba katika mvuto unaopendeza wengi.

Epuka kuoanisha rangi ya zulia na kila kitu kilichopo katika chumba chako.

Kumbuka kwamba ukichanganya rangi mbili au tatu ndani ya chumba hazichoshi sana na unaweza kukupa mwanya mkubwa wa kupendezesha na kufanya mabadiliko ya baadhi ya vitu hususani pazia na urembo mwingine.

Kwa upande wa mazulia ya mlangoni au bafuni, ni vizuri kuweka yenye mpira kwa chini ili kuzuia yasioze kutokana na maeneo hayo kuwa na ujuzi.

Habari Kubwa