Manyika: Sistahili kusota benchi

25Jan 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Manyika: Sistahili kusota benchi

KIPA wa timu ya Simba, Peter Manyika, amesema kuwa hafahamu sababu zinazomfanya awekwe benchi katika michezo mbalimbali ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

KIPA wa timu ya Simba, Peter Manyika.

Manyika ameichezea Simba mara ya mwisho kwenye mchezo wa nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar Januari 10 iliyomalizika kwa Simba kulala kwa goli 1-0.
Akizungumza na gazeti hili jana Manyika alisema kuwa kitendo cha ‘kusugua’ benchi kinamuamiza 'kichwa' kwa sababu yeye ni mmoja wa wachezaji wanaofanya vizuri mazoezini na anashangaa kuona hapangwi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
"Sifahamu ni kwa nini sichezi, lakini nafikiri ni uamuzi tu wa kocha, muda utafika na mimi nitacheza tu.
Siamini kama mchezo ule (Simba vs Mtibwa Sugar- Zanzibar) ndio sababu ya mimi kutoanzishwa, bado kuna michezo mingi mbele inakuja tusubiri tuone," aliongeza kipa huyo ambaye baba yake Manyika Peter aliwahi kuidakia Yanga na Taifa Stars.
Hata hivyo chipukizi huyo alimpongeza kipa mwenzake wa timu hiyo, Vincent Agban, kwamba anafanya vizuri na anastahili kuwa chaguo la kwanza.
"Kwanza lazima ujue kuwa hakuna golikipa mbaya kwenye timu, kama ingekuwa hivyo tusingekuwa tunasajiliwa," aliongeza.
Alisema kuwa anafanya mazoezi kwa bidii ili kumshawishi kocha wao mpya, Jackson Mayanja kumpa nafasi kwenye michezo inayofuata ya timu hiyo.