Hili la ujenzi holela ni muhimu kuangaliwa

13Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hili la ujenzi holela ni muhimu kuangaliwa

TATIZO la ujenzi holela limeonekana kuwa sugu nchini kutokana na kutofuatwa utaratibu wa mipango miji na baadhi ya watu kujijengea nyumba ovyo.

Ujenzi holela husababisha miundombinu muhimu kushindwa kupitishwa katika baadhi ya maeneo kwa sababu ya kukosa njia za kupita.

Inapotokea majanga makubwa kama ya moto, mafuriko uokoaji hushindwa kutekelezwa kwa wakati kutokana na kukwama kufika eneo husika kwa kukosa barabara.

Tatizo hili la ujenzi holela chanzo kikubwa ni baadhi ya watu kununua ardhi kienyeji kwa kukatiwa vipande bila kujali mpangalio wa kuwezesha miundombinu ya barabara, umeme na maji kupitishwa maeneo yanayohusika.

Ujenzi holela pia umechangia maeneo mengi ya miji kukumbwa na mafuriko kwa sababu njia zinazotakiwa kupita maji hayo kuzuiwa na ujenzi.

Juzi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akiwa katika ziara yake mkoani Singida, aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kusimamia ardhi kuanzia ngazi za mitaa na vijiji ili ziweze kuepuka na ujenzi holela na kurahisisha ufuatiliaji makusanyo ya kodi ya pango la ardhi.

Akitoa agizo hilo Lukuvi alisema ni vyema wakurugenzi katika halmashauri nchini wakawapa wajibu watendaji wa mitaa na vijiji kwa barua kusimamia misingi ya ardhi yenye lengo la kusimamia sheria katika masuala ya ardhi.

Hata hivyo, akatoa tahadhari kuwa watendaji wa mitaa na vijiji watakaokasimia mamlaka ya usimamizi ardhi katika maeneo yao hawatakuwa na jukumu la kugawa, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, bali kuangalia yanayoendelea katika mitaa yao na wakikuta ukiukwaji wowote wa ujenzi holela watakuwa na wajibu wa kusitisha.

Ufafanuzi huo umeweka wazi mipaka ya watendaji hao katika kusimamia suala la ardhi katika vijiji na mitaa yao.

Ni jambo jema kwa watendaji wa mitaa kuzungukia maeneo yao na kusitisha ujenzi holela ambao husababisha kero na migogoro kwa wakazi kwa sababu tu mtu ameamua kuziba njia kwa kujenga ukuta kuzunguka nyumba yake bila kujali wenzake watapita wapi.

Waziri Lukuvi katika agizo hilo amewataka watendaji hao kutengeneza majedwali maalum yenye orodha inayoonyesha kila mmiliki wa kiwanja kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa mitaa kuwajua katika maeneo yao.

"Kumbukumbu zote za masuala ya ardhi wajulishwe watendaji wa mitaa na vijiji ili waweze kufuatilia katika mitaa yao," alisema Lukuvi.

Ofisi za ardhi za mikoa pia zimetakiwa kutoa elimu kwa watendaji wa mitaa na vijiji ili kuwajengea ufahamu wa masuala ya ardhi na kuwawezesha kusimamia vyema masuala hayo katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hata kama manispaa imepanga matumizi bora ya ardhi ni vyema matumizi yake yakawekwa kwenye vipande vya ngazi ya mitaa na kuwa kazi hiyo ni ya halmashauri kwa kuwa mitaa ni jicho lake la kutoa taarifa katika masuala mbalimbali yakiwamo ya ardhi.

Halmashauri zote zimepewa wajibu wa kusimamia ardhi katika maeneo yao na ilichofanya Wizara ya Ardhi ni kuwapatia wataalamu watakaowasaidia kujua namna bora ya kutumia ardhi vizuri.

Habari Kubwa