Tumerejea, tunawaahidi wasomaji na wadau wetu kutimiza makusudio yao

06Sep 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Tumerejea, tunawaahidi wasomaji na wadau wetu kutimiza makusudio yao

BAADA ya kuwa nje kwa miezi 18, hatimaye gazeti letu pendwa la Nipashe Jumapili limerejea rasmi huku likiwa na habari zilizofanyiwa uchunguzi wa kina, makala, burudani na michezo.

Katika kipindi chote hicho, wasomaji wetu walikosa uhondo waliokuwa wakiupata hatua ambayo ilisababisha wengi wao kuhoji kulikoni mpaka ukafikiwa uamuzi wa kulisimamisha gazeti hilo.

Pamoja na kuhoji huko, wengi walikuwa wakitoa ushauri wa kurejeshwa, hivyo kusikia maombi hayo na sasa tumerejea rasmi. Ni ukweli usiopingika kwamba wasomaji wetu walikosa mambo mengi ambayo yalikuwa yakiwapa burudani na elimu.

Kutokana na kusikia kilio cha wasomaji wetu na kuwa wasikivu, tunawaahidi kwamba tutajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kuwaletea kile wanachokitaka kwa kuandika habari, makala na uchambuzi ili kutimiza lengo la kuelimisha, kuonya na kukosoa.

Pia tunaahidi kwamba tutaibua mambo ambayo yatasaidia kubadilisha mitazamo na mwelekeo wa jamii katika nyanja zote za kimaisha, yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Lengo la hayo yote ni kuifanya jamii ya Watanzania kuwa na mtazamo chanya katika muktadha mzima wa maisha. Katika kutekeleza hayo yote, tutazingatia weledi, taaluma na kujali matakwa ya kijamii na yale ya kisheria ili kuhakikisha mambo yote yanayoripotiwa katika gazeti hili yanafuata misingi ya kitaaluma na utawala wa sheria.

Wakati tukiahidi hayo yote, hatuna budi kuwakumbusha wasomaji wetu kwamba huo ndio wajibu wetu, kwa hiyo nao kwa upande wao wanapaswa kutumiza wajibu wao hasa kutoa ushirikiano unaostahili katika kutoa maoni yao.

Kwa kufanya hivyo, ni dhahiri kwamba watatuwezesha kufikia lengo letu la kuhabarisha.

Pia wasomaji wetu, bila kujali taaluma zao, hawana budi kutoa maoni yao juu ya yale wanayoyahitaji kuwamo katika gazeti pamoja na kushauri yaliyomo ndani ili kuboresha habari zetu na kuwavutia wateja.

Tunasema hivyo kwa sababu tunahitaji kuwa na ushirikiano mzuri baina yetu na wasomaji wetu.

Tunatoa rai pia kwa taasisi na mashirika ya umma na binafsi kushirikiana nasi katika kuuhabarisha umma kwa njia mbalimbali ikiwamo uhusiano chanya wa kibiashara.

Imani yetu ni kwamba katika kufanya hivyo kutakuwa na mafanikio makubwa katika maendeleo ya nyanja husika na hatimaye kufikia malengo ya kitaasisi yaliyokusudiwa.

Kipekee, tunawaomba wasomaji na wadau wetu kutupokea na kushirikiana nasi katika kutekeleza jukumu letu la kuuhabarisha umma na kutoa elimu na mabadiliko ya jamii kwa ujumla katika nyanja zote za kimaisha.

Ni matumaini yetu kwamba ushirikiano chanya tutakaoupata kutoka pande zote utawezesha kufika katika upeo wa malengo tuliyojiwekea na hatimaye kutimiza kiu ya wada

Habari Kubwa