Haki itumike Ligi Kuu

16May 2020
Barnabas Maro
Dar es Salaam
Nipashe
Haki itumike Ligi Kuu

HAKI ni kitu au jambo ambalo mtu anastahiki kupata; utendaji, ufuataji na utumiaji wa kanuni katika kutimiza jambo; mali, milki. Kwa ufupi ni jambo linalomstahikia mtu; haki za binadamu.

Wakati serikali ikitafakuri kuhusu kuipa au kutoipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, kumekuwa na mawazo mengi yanayotolewa na makundi mbalimbali.

Upande wa Simba, (kama ambavyo ungekuwa upande wa Yanga kama ingekuwa kwenye nafasi hiyo) unaomba timu yao itangazwe bingwa kwa kuwa ndiyo inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na alama 71 baada ya kucheza mechi 28, kushinda 23, sare 2, kupoteza 3, ikifunga mabao 63 na kufungwa mabao 15.

Nadhani hali hii ndiyo iliyofanya m-bunge aliye mwanachama wa Simba apendekeze Ligi Kuu ifungwe na Simba wapewe kombe lao kwani ndiyo inayoongoza kati ya timu 20.

Hoja hii aliitoa Bungeni! Ndivyo alivyotumwa na wapigakura wake? Nasema hasha (sivyo kabisa)! Hata kama ingekuwa timu yangu (Yanga – timu ya wananchi) ndiyo inayoongoza, ningepinga wazo la kuipa ubingwa kabla ya kukamilisha michezo yote.

Naomba tukubaliane kutokubaliana kuwa ‘kweli’ ni uhakikisho wa jambo kama lilivyo; ingawa najua wapo watakaonibeza na kunifyonya. Hata hivyo wanapaswa kutambua kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu. “Kweli ikidhihiri, uongo hujitenga.”

Methali hii yatukumbusha kwamba ukweli wa jambo utokeapo, uongo unaolihusu hautambuliwi au hauna nafasi. Huweza kutumiwa kumnasihi mtu anayejaribu kusema uwongo waziwazi.

Mpaka Ligi Kuu iliposimamishwa kutokana na woga wa maambukizi ya virusi vya corona, zilikuwa zimesalia mechi tofauti tofauti kati ya timu zinazoshiriki.

Kwa ujumla, timu zote 20 za Ligi Kuu zatakiwa kucheza michezo 38 kila moja. Kati ya timu 20 zinazoshiriki, 11 zimecheza mechi 29; timu nane zikiwamo Simba na Azam zikiwa zimecheza mara 28. Timu hizo zinafuatiwa na Yanga, timu pekee iliyocheza michezo 27.

Kwa nini nashauri Ligi Kuu iendelee? Ligi Kuu ya msimu ujao itakuwa na timu 16 tu. Katika msimamo huo, timu nne zitashushwa daraja, yaani hazitakuwapo kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa maana hiyo timu zilizo mkiani, yaani Singida United, Mbao FC, Alliance FC na Mbeya City ndizo zilizo kwenye hatari ya kushushwa daraja kwa maana ya “Kwaheri Ligi Kuu.”

Timu zilizo nafasi za juu ikiwamo Simba ambayo labda ifanyike miujiza ndio ishindwe kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, ni Azam FC iliyo nafasi ya pili, Yanga kwenye nafasi ya tatu ikifuatiwa na Namungo ikiwa nafasi ya nne kutoka juu.

Ni wazi timu hizo tatu kila moja inaiombea nyingine mabaya ili ipate nafasi ya kwenda juu ili zishiriki michezo ya kimataifa. Kama, kwa mfano, Simba ikiteleza na kushindwa kutwaa kombe lililo kwenye kizingiti cha jengo lao pale Msimbazi jijini Dar es Salaam, hapana shaka itakuwa katika nafasi ya pili.

Hilo halina ubishi. Ikiwa hivyo, kwa Simba itakuwa sawa na methali isemayo: “Ajabu ya shingo kukataa kulala kitandani.” Ajabu inayorejelewa hapa, ni ya shingo kukataa kulala ingawa mwenyewe anataka kulala!

Hii ni methali ya kutumiwa kumrejelea mtu anayetaka kitu fulani lakini anajifanya hakitaki ilhali anakitaka! Kama Simba wakishindwa kutwaa ubingwa (chondechonde, sio ‘Ndoo’ kama iandikwavyo magazetini), warudi na kujiuliza wamekosaje taji hilo msimu huu na hapo waweza kuuhusisha 'uchawi'.

“Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyae mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema.

Bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.” (Yeremia 17:5-6). “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake.

Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.” (Yeremia 17:7-8).

Endapo Ligi Kuu itafutwa na Simba kupewa kombe, italeta manung’uniko kwa timu saba – tatu za juu zilizo chini ya Simba na nne za chini zitakazoshushwa daraja kwani msimu ujao watanakiwa kuwa na timu 16 tu. Itakuwa vilio na kusaga meno! Ligi Kuu ichezwe hata bila watazamaji ili ikamilike.

Tena iwe ndani na nje ili kila timu itumie fedha kwa usafiri wa kuzifuatia timu zingine na pia kufaidi viwanja vya nyumbani. Watazamaji waangalie kwenye runinga majumbani na ‘vibanda hasara’ mitaani. [email protected] 0784 334 096

Habari Kubwa