Diaspora wapewe moyo kufanya makubwa zaidi

02Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Diaspora wapewe moyo kufanya makubwa zaidi

MARA kadhaa baadhi ya watu wamekuwa wanaeleza umuhimu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni maarufu kama Diaspora katika maendeleo ya nchi.

Hoja ambayo husisitizwa na watu hao wakiwamo viongozi wakuu wa taifa letu ni kuwa ushiriki wa Diaspora kama watahamasishwa na kuhamasika katika maendeleo ya nchi unaweza kuchangia nchi kupanda chati kiuchumi.

Faida ya kuwashirikisha ni kuwa wanaweza kuchangia kwa kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali, wakiwa na nia nzuri kutokana na kuwa wao ni sehemi ya Tanzania.

Katika miaka ya karibuni tulianza kuona dalili kuwa Diaspora wameanza kuhamasika kutokana na kauli wanazozitoa za kuwa tayari kuwekeza nchini, na kuchangia kukuza uchumi wa nchi yetu.

Uamuzi wa serikali zetu mbili ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kuendelea kuwahamasisha na kuwashawishi Diaspora kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi yetu kumesababisha pamoja na mambo mengine kufanyika kwa mikutano yao kila mwaka nchini kwa lengo la kuzungumza masuala yao na nafasi yao katika maendeleo ya nchi.

Tayari wameshaanza kushiriki kwa kusaidia baadhi ya miradi ya kijamii pamoja na kuwekeza katika miradi ya kiuchumi na wanaendelea kujipanga kufanya mambo makubwa zaidi.

Tumepokea kwa furaha na moyo mkunjufu taarifa kuwa uongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) uko tayari kusimamia ujenzi wa daraja refu la kisasa lenye uwezo wa kuunganisha miji miwili ya Dar es Salaam na Zanzibar katika harakati za kuimarisha uchumi na mawasiliano.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo akiwa pia mjumbe wa kamati ya biashara Tanzania, Jonas Njao, akiiongoza timu ya wanajumuiya hiyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.Jonas alisema Diaspora imeanza harakati za maandalizi ya kufanya utaratibu wa kuziomba serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kuuridhia mradi huo mkubwa wa kimataifa utakaoweza kupunguza tatizo la ajira kwa kundi kubwa la Watanzania.

Alisema wataalamu pamoja na wafadhili wa ujenzi wa mradi huo wa kiuchumi wameshajitokeza na kinachosubiriwa kwao kwa sasa ni kukubalika kwa maombi ya mradi ambao bado umekuwa adimu ndani ya Bara la Afrika.

Kwamba fursa wanazozipata za kuwasiliana na taasisi na kampuni wanazozunguka katika mataifa tofauti duniani zimelenga kutafuta nafasi za ajira zitakazosaidia kuimarisha ustawi wa wananchi kutokana na vijana wao kujikomboa katika masuala ya ajira.Tunaishukuru na kuipongeza jumuiya ya Diaspora kwa kuona fursa hiyo, ambayo itatengeneza fursa za ajira kwa wingi pamoja na fursa kubwa na ya kipekee na ya kusasa ya miundombinu.

Kujengwa kwa daraja hilo itakuwa ni historia katika bara la Afrika, na kwa hakika kutasaidia kurahisisha usafiri wa wananchi na bidhaa pande zote kutoka upande mmoja kwenda mwingine badala ya kutegemea njia usafiri wa majini na wa angani, ambao umekuwa na changamoto nyingi.

Sekta nyingine ambayo itanufaishwa na mradi huo mkubwa na muhimu ni ya utalii, kwa kuwa watalii wengi watavutiwa kuja kuangalia kivutio hicho.

Tunazishauri serikali zote mbili kuupokea mradi huo kwa mtazano chanya na kuuridhia haraka ili utekelezaji wake uanze mara moja na kuinufaisha nchi yetu kujamii na kiuchumi, huku huku jitihada endelevu zikiendelea kuwahamasisha na kushawishi Watanzania wanaoishi ughaibuni kuendelea kushiriki katika ujenzi wa uchumi wetu.