Nani anawapa jeuri hawa ‘panya road’

04May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Nani anawapa jeuri hawa ‘panya road’

KUNA swali moja ambalo linahitaji majibu. Swali hilo ni nani hasa analipa jeuri kundi la kihalifu maarufu kwa jina la ‘panya road’ ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa likifanya matukio ya kihalifu mkoani Dar es Salaam bila woga wala hofu ya kushughulikiwa.

Vitendo hivyo ni kuvamia watu mitaani, kwenye maduka na nyumbani kisha kuwajeruhi kwa kutumia mapanga na kuwapora mali mbalimbali, zikiwamo fedha.

Tumeliuliza swali hili ili yapatikane majibu yasiyoacha shaka yoyote kuhusu kundi hili la wahalifu linapewa jeuri na kulindwa na nani kwa miaka yote.

Kuna mambo kadhaa yanatushangaza yakiwamo umri mdogo wa vijana wanaounda kundi hilo la kihalifu ambao inaelezwa kuwa ni kuanzia miaka 15 hadi 25.

Kwamba inakuwaje wanafanya matukio haya bila kujulikana wakati wengi wao wanaishi na wazazi wao? La pili, je, mamlaka mbalimbali kama za mashina, mitaa na kata haziwafahamu wala familia wanazotoka.

Tatu, je, inakuwaje vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi kutowafuatilia na kuharibu mtandao wao kwa miaka yote ambayo wamekuwa wakihatarisha maisha ya wananchi na mali zao?

Haya yote yanatufanya tubaki na swali hilo tuliloliuliza awali kwamba ni nani hasa anawalinda na kuwapa jeuri ‘panya road’, ambao wamedhihirisha kwamba hawaogopi chochote wala mamlaka yoyote licha ya maonyo ambayo yamekuwa yakitolewa na vyombo vya dola na viongozi wa serikali.

Kikundi hiki kimeibuka upya hivi karibuni na kufanya vitendo hivyo katika maeneo ya Chanika, Tabata kabla ya kutenda unyama Kunduchi siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan Jumapili kutoa onyo dhidi ya vitendo vya kihalifu na kulitaja moja kwa moja kundi la ‘panya road’.

Jumatatu wiki hii majira ya jioni vijana hao walidaiwa kuwakata mapanga watu 19 na kupora mali mtaa wa Mtongani Kata ya Kunduchi mkoani Dar es Salaam, huku Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likithibitisha kuwakamata sita kati yao.

Tukio hilo ni la pili katika mkoa huo baada ya wiki moja iliyopita katika Wilaya ya Ilala kundi linalodaiwa kuwa la ‘panya road’ kuvamia nyumba 23, kujeruhi na kuiba mali na fedha.

Mfululizo wa vitendo vinavyofanywa na kundi hilo ni dalili za tishio kubwa la usalama wa maisha ya wananchi na mali zao, kiasi kwamba Rais Samia ameliona hilo na kulitolea kauli.

Rais Samia akizungumza na wafanyakazi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jijini Dodoma Jumapili, alikemea vitendo vya uhalifu na kuwataka wahusika, wakiwamo ‘panya road’ kuacha mara moja.

Tukio la Kunduchi lichukuliwe kama changamoto kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua sasa kuhakikisha kwamba kundi hilo linatokomezwa kabisa, kwa kuwa limeonyesha jeuri hata kwa mkuu wa nchi aliyetoa onyo siku moja kabla.

Vyombo hivyo hususan Jeshi la Polisi halinabudi kuweka utaratibu endelevu kuhakikisha kwamba vitendo vyote vinavyofanywa na vijana hao vinadhibitiwa kabla, ikiwamo kuwashirikisha viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi za mitaa na jamii nzima kupitia ulinzi shirikishi.

Tatizo tunaloliona ni kwamba yanapotokea matukio la uhalifu, Jeshi la Polisi na wanasiasa wanatoa ahadi za haraka za kuyakomesha, lakini hatua hizo haziwi endelevu, hivyo kujirudia baada ya muda si mrefu.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, aliitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo na kusema wataanzisha operesheni endelevu ya kupambana rasmi na vikundi vya vijana wahuni.

Alisema hawawezi kuwaacha vijana hao wakitamba na bisibisi na mapanga na kutia hofu kwenye jamii, na kwamba kuanzia siku hiyo hakuna atakayesalimika.

Tunaunga mkono tamko la Makalla, lakini ahakikishe operesheni dhidi ya uhalifu inakuwa endelevu. Tunaamini hatua hizi zikichukuliwa, jibu la swali nani anawapa jeuri ‘panya road’ litapatikana sambamba na kuufuta kabisa mtandao huo.

Habari Kubwa