Wafanyabiashara wadogo watumie fursa hii kikamilifu

04Jan 2018
Mhariri
Nipashe
 Wafanyabiashara wadogo watumie fursa hii kikamilifu

WAFANYABIASHARA wadogo nchini wamekuwa na kilio cha muda mrefu sana cha kudaiwa kodi muda mfupi baada ya kuanza biashara.

Wamekuwa wakidai kuwa kudaiwa mapema kabla ya kuanzisha biashara kumekuwa kukiwakwaza kwa kuwa wanakuwa hawajaanza kupata faida.

 

Ni malalamiko ambayo serikali zilizotangulia zilikuwa zikiyapokea na kutoa ahadi kuwa yatashughulikiwa.

Kimsingi, malalamiko hayo yalikuwa na mantiki kwa kuwa haileti maana kumdai kodi mfanyabiashara kabla ya kuanza kufanya biashara na mwenendo wake kuonekana, ikiwamo faida.

 

Hatimaye kilio hicho kimesikika, baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutangaza kuwa imeondoa utaratibu wa awali kwa walipakodi wadogo kulipia kodi kabla ya kuanza kufanya biashara, badala yake kuwataka kulipia robo ya kwanza ndani ya siku 90 tangu kusajiliwa.

 

Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya, ndiye aliyetangaza uamuzi huo juzi jijini Dar es Salaam ambao ni neema kwa walipakodi wadogo.

Kamishna huyo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa Walipakodi na kusema kuwa  jukumu la usajili wa walipakodi kwa Mamlaka hiyo ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, kuongeza makusanyo pamoja na kuwa na taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi, ili kuchangia Pato la Taifa.

Alisema kwamba kampeni hiyo imekwenda sambamba na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na TRA kwa walipakodi wadogo kwa kuwapa siku tisini za kulipa kodi kwa robo ya kwanza ya malipo pindi tu watakapokuwa wamesajiliwa.

Kwa mujibu wa Mwandumbya, mabadiliko hayo yatakuwa chachu katika usajili kwa kuwa wanatarajia kusajili walipakodi takribani milioni moja nchi nzima.

Tunaipongeza serikali kwa kukiona kilio hicho cha muda mrefu cha walipakodi wadogo, ambao wengi wanajihusisha na shughuli za kujitafutia riziki na sio kutengeneza faida.

 

Uamuzi huu unadhihirisha kwa vitendo jinsi serikali ya awamu ya tano ilivyo sikivu na ilivyodhamiria kutekeleza ahadi yake ya kuwaondolea kero wanyonge, wakiwamo wafanyabiashara wadogo.

Kwa uamuzi huo tunaweza kusema kuwa walipakodi wadogo wamewekewa mazingira bora ya kufanya shughuli za ujasiriamali bila bugudha waliyokuwa wanakumbana nayo kutoka kwa mamlaka kadhaa, zikiwamo halmashauri na TRA.

Kwa kuwa Mamlaka hiyo inasema kuwa usajili wa TIN ni bure na utafanyika katika ofisi zote za Mamlaka hiyo na katika vituo maalum vitakavyokuwa vimeteuliwa na kutangazwa kupitia vyombo vya habari na matangazo katika maeneo husika, tunawashauri walipakodi wadogo kwenda kijisajili, ili wafanye biashara katika mazingira bora na tulivu.

Wazingatie pia maelekezo ya TRA kujihadhari na vishoka wanaoweza kutumia mwanya wa kuharibu nia njema ya kampeni hiyo kwani hakuna wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili wala kutoa fomu za usajili wa zoezi hilo.

Kwamba mhusika lazima aende mwenyewe, ili apigwe picha na kuchukuliwa alama za vidole pia atatakiwa aende na mkataba wa pango au uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua yenye muhuri na namba ya simu ya Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pamoja na kitambulisho cha muhusika kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura.

Ni matumaini yetu kuwa kampeni hiyo itawasaidia walipakodi wachache wengi kunufaika na biashara na tunawasisitiza kuhakikisha kila anayestahili kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipakodi anakwenda kusajiliwa na kupata namba hiyo kwa urahisi na haraka.

 

 

Habari Kubwa