‘Tunasaluti’ miaka 57 Mapinduzi ya Zanzibar

12Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
‘Tunasaluti’ miaka 57 Mapinduzi ya Zanzibar

LEO ni maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Tunawapongeza Watanzania wa Zanzibar na Pemba wanapokumbuka siku hii muhimu ya kihistoria iliyoleta uhuru.

Tunaposherehekea Mapinduzi tunatizama nyuma na kufurahia mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa nchi yetu.

Miongoni mwa malengo makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar yanabakia kuleta maendeleo kwa wananchi.

Ikiwa pamoja na elimu, afya, barabara, makazi na nishati ili kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuyafanya yawe bora zaidi kutokana na ukandamizaji uliodumu kwa karne kadhaa.

Leo Watanzania tuna kila sababu ya kufurahia mafanikio miongoni mwa sekta zilizobadilisha maisha ya wananchi wetu kiuchumi hasa wanaoishi vijijini.

Tukitazama maisha ya Wazanzibari wengi tunafurahi kuwa yamekuwa bora kutokana na uwepo wa umeme.

Tunalipongeza Shirika la Umeme (ZECO) kwa kuwafikishia wananchi kwa asilimia 80 huduma hiyo.

Limesambaza nishati hiyo muhimu kutoka mijini hadi vijijini na kusaidia kuwapo kwa mabadiliko makubwa ya ukuaji wa uchumi na kupambana na umaskini miongoni mwa Watanzania.

Tunawakumbuka na kuwaenzi waasisi kwa kusaidia kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya umeme ukiwa ni pamoja na kupitisha waya baharini ili kuusafirisha umeme kwa wananchi bila kujali gharama wala usumbufu.

Ni dhahiri Wazanzibari wengi wanaoishi mijini na vijijini watakubaliana nasi kuwa juhudi za ZECO za kuvifikishia umeme vijiji 2,695 kati ya vijiji vyote 3,260 viliopo Unguja na Pemba zinastahili kushangiliwa kwa kuwa zimeakisi kikamilifu lengo la mapinduzi.

Kila mmoja anazifahamu faida za umeme ambazo pamoja na kumulika na kutuondoa gizani ni nuru shuleni inayowawezesha watoto wetu kusoma bila kujali ni mchana au usiku.

Aidha, ndicho chanzo cha kuendesha mitambo kuanzia mashine ndogo vijijini zinazotumiwa na wajasiriamali kuzalisha na kubadili maisha yao na kuondokana na umaskini hadi kusukuma mitambo ya viwanda vikubwa.

Tunapoadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi ZECO imevifikishia umeme visiwa vidogo viliopo Unguja na Pemba na nishati hiyo imebadilisha maisha ya wakazi wa sehemu hizo wakiwamo wavuvi ambao kinachoonekana ni mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Yote hayo yanapunguza pengo la utofauti kati ya maisha ya mjini na vijijini kupunguza umaskini.

Kama wazalendo na wapenda taifa letu, tuendelee kuenzi mapinduzi kwa kuendeleza hisia za upendo na uvumilivu baina yetu huku tukidumisha amani na utulivu.

Ili Watanzania tufurahie maendeleo na mafanikio kwenye sekta muhimu hasa elimu, afya, ajira, miundombinu na nishati ni lazima serikali zifanye juhudi kubwa za kufanikisha upatikanaji wa kazi (ajira).

Tunahitaji kuona nafasi nyingi zaidi za kazi ili kuwapa watu wetu mapato ziwe za kujiajiri au za kuajiriwa ili wananchi wamudu maisha yao kikamilifu.

Tunahitaji kuona Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar zikishirikiana na kuanzisha uwekezaji mkubwa wa bahari kuu ili uchumi wa bluu unufaishe Watanzania.

Tunapoona fahari kusherehekea Mapinduzi, tuone uchungu kuwa kwa miaka 57 hatujaweza kufanikisha uwekezaji uchumi wa bahari kuu.

Ni wazi kuwa tumejenga miundombinu ya kisasa, kuzalisha umeme na kuusambaza vijijini, kujenga shule na vyuo vikuu pamoja na kuongeza wasomi, lakini hatujawezekeza kwenye bahari kuu na kuvuna kikamilifu rasilimali zilizoko.

Tunaamini ni sekta muhimu itakayoleta ajira na kuinua uchumi wa Mzanzibari na Jamhuri yetu, shime serikali zisikie hili.

Habari Kubwa