981 kupata mimba Kibondo tishio kwa ustawi wa mtoto wa kike

21Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
981 kupata mimba Kibondo tishio kwa ustawi wa mtoto wa kike

JUMLA ya wanafunzi 981 wilayani Kibondo, mkoani Kigoma walipata mimba katika kipindi cha miezi sita, Januari hadi Juni, mwaka huu, sasa wako nyumbani wamekosa haki yao ya kupata elimu.

Takwimu hizo ni wastani wa wanafunzi 163 kila mwezi na mwezi na mwezi mmoja ulikuwa na wanafunzi 164, mwezi mwingine 165 ambao waliacha masomo kwa sababu ya kupata mimba.

Takwimu hizo ni kwa waliopata mimba bado za utoro ambao uhusisha wanafunzi wa kike na kiume hazijatajwa, na hii ni kwa wilaya moja kwamba ndoto za wanafunzi hawa zimekufa kwa kulazimishwa, kulaghaiwa au kwa uwezo mdogo wa kuchambua mambo na kujikuta kwenye mitego wa waharibifu.

Hali hii siyo ya kuridhisha kwa kuwa inaongeza idadi ya wajinga kwenye jamii ambao sasa watazaa watoto ambao huenda wakapita njia hiyo hiyo, mama hakusoma na mtoto naye hatasoma maana yake inaandaliwa jamii isiyoelimika ambayo ni ngumu kufanya uamuzi au kuchangia uchumi wa nchi bali kuendelea kuzalisha wategemezi.

Ujinga ni mzigo wa taifa na ndiyo maana zimekuja shule ili watu wasome na kuelimika kwa namna tofauti, ikiwamo kujua kusoma na kuandika ili kumudu maisha kwa kuwa yanahitaji watu walioelimika.

Jambo hili lina sura nyingi mojawapo ni wazazi au walezi kushindwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao, kwa kuwa inaonekana wanajilea wenyewe.

Mifano ni mingi ambayo inaonyesha wapo watoto wanajilea wenyewe, na wakati mwingine wazazi wanawageuza watoto mtaji wa kujipatia kipato kiasi cha baadhi kujihusisha na mambo yasiyostahili.

Ni wajibu wa wazazi, walezi na serikali kushirikiana kukomesha tabia hii, inawezekana hao wamefahamika, lakini kuna idadi kubwa ambao hawajafahamika na waliacha shule wanalea watoto, mtoto analea mtoto mwenzake.

Yawezekana kuna ambao wako shuleni na wana ujauzito, lakini kwa kuwa bado hawajapimwa ni rahisi kujificha na kuacha shule au kuendelea na masomo kwa kuwa maumbile hutofautiana.

Hatari nyingine ni za kiafya kwamba kwa umri wa chini ya miaka 18 kujifungua ni kwa tabu na kuna uwezekano wa kupoteza maisha, huku wengine wakipata fistula na maradhi mengine yanayosababishwa na uzazi katika umri mdogo.

Sheria ya elimu imeweka wazi adhabu inayotolewa kwa mtu anayebainika kumpa ujauzito mwanafunzi ni kifungo cha miaka 30 jela, ni lazima hatua zichukuliwe ili iwe fundisho kwa wengine wanaotamani kuwa kwenye mahusiano na wanafunzi.

Ifike mahali jambo hili lizungumzwe kama agenda muhimu kwenye mikutano ya hadhara ya kijiji ambayo hujumuisha wenyeviti wa vitongoji vyote na wananchi, na kamati ya ushauri ya kata (WDC) ambayo mwenyekiti wake ni diwani wa kata na wajumbe ni wenyeviti wa vijiji huku mtendaji wa kata akiwa katibu na baadaye kwenye Baraza la Madiwani ambalo huundwa na madiwani wa kata zote za wilaya au eneo la utawala la halmashauri ambao huchagua Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji huwa Katibu wa kikao na wajumbe wengine ni wakuu wa idara za halmasahuri husika, ili ijulikane na hatua zichukuliwe kuhakisha kizazi cha baadaye kinaokolewa.

Kukiwa na ushirikiano baina ya serikali na wadau wote kuna uwezekano mkubwa wa kushughulikia tatizo hilo, ikiwamo kuja na mkakati maalum wa kuwaendeleza wanafunzi hawa ambao haki yao ya kusoma imekatishwa kwa kulaghaiwa, kukubali wenyewe au kubakwa.

Jitihada nyingi zinafanyika kuongeza idadi ya wanawake waliosoma, kwenye ngazi za uamuzi na nguvu ya kiuchumi, sasa kinapotokea kikwazo kama hiki maana yake idadi ya wanawake waliosoma inapungua, wenye nguvu ya kiuchumi na wanaoweza kushika madaraka katika uamuzi mbalimbali.

Miongoni mwa wanafunzi hao 981 wapo madaktari, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mkoa na wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri mbalimbali, lakini kwasababu ya ujauzito wameshindwa kuendelea na masomo yao kama watoto wengine.

Habari Kubwa