Adhabu ya kifo inahitaji mjadala mpana wa kitaifa

14Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Adhabu ya kifo inahitaji mjadala mpana wa kitaifa

UAMUZI wa Rais John Magufuli wa kukataa kusaini hukumu zinazotolewa na mahakama za kuwanyonga watu waliopatikana na makosa yanayostahili adhabu hiyo, umewaibua wanaharakati na taasisi nyingine za kutetea haki za binadamu.

Wanaharakati na taasisi ya kutetea haki za binadamu zimekubaliana na kauli ya Rais na kumuunga mkono kwa uamuzi huo.

Jumatatu wakati akimuapisha Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Rais John Magufuli alisema anatambua ugumu wa kutekeleza adhabu hiyo, hivyo akaitaka mahakama kutompelekea orodha ya waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Alisema ana taarifa kuwa wapo watu wengi walioidhinishwa kunyongwa, lakini aliuomba mhimili wa mahakama usimpelekee orodha hiyo kwa ajili ya kusaini wanyongwe hadi kufa kwa sababu anajua ugumu wake ulivyo.

Kutokana na uamuzi wa Rais, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imempongeza kwa kusema kuwa ni tamko lenye kuzingatia haki ya msingi ya kuishi.

Mwenyekiti wa THBUB, Tom Nyanduga, alisema tume inaungana na wadau wengine kumpongeza Rais kwa tamko hilo ambalo limekuja muda mfupi kabla ya Siku ya Kimataifa ya kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta adhabu ya kifo, ambayo huadhimishwa Oktoba 3 ya kila mwaka.

Kwamba uamuzi wa Rais Magufuli unaendana na Mkataba wa Kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayozitaka nchi wanachama kufuta au kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo.

Alisema Tume inatambua kwamba adhabu ya kifo haijatekelezwa hapa nchini katika kipindi cha takribani miaka 20 iliyopita na hivyo kudhihirisha kwamba Tanzania ni nchi isiyotekeleza adhabu ya kifo kwa hiari yake yenyewe pamoja na uwapo wa adhabu hiyo katika sheria za nchi.

Kwa kuzingatia kauli ya Rais pamoja na mahitaji ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, Tume inaishauri Serikali iridhie Itifaki ya pili ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa Itifaki ambayo inazitaka nchi wanachama kufuta adhabu ya kifo.

Kwa upande wake Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Dk. Hellen Kijo-Bisimba,
kimempongeza Rais Magufuli kwa uamuzi huo na kushauri serikali ianze mchakato wa kubadili Sheria ya Kanuni za Adhabu sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambayo inatoa adhabu ya kifo kwa makosa ya uhaini, ugaidi na kuua kwa kukusudia.

Sisi pia tunampongeza Rais kwa uamuzi wake huo kutokana na ugumu uliopo wa kuitekeleza hukumu ya kunyonga.

Ugumu huo unabainishwa na takwimu zilizopo ambazo zinaonyesha tangu mwaka 1994 hadi 2015 jumla ya watu 472 walihukumiwa kunyongwa, lakini adhabu hiyo haijatekelezwa tangu mwaka huo.

Hata hivyo, sisi hatuoni kama ni sahihi kukurupuka tu na kuifuta sheria hiyo bila jamuiya yetu kwanza kufanya tafakari ya kutosha kisha kuamua kama sheria hiyo ifutwe au iendelee kuwapo.

Kimsingi sheria hii ilitungwa kwa ajili ya kudhibiti makosa makubwa yatokanayo na vitendo vya jinai vya uhaini, ugaidi na kuua kwa kukusudia. Ni matendo ambayo yanasababisha baadhi ya kuwaua wengine.

Athari inayoweza kutokea ikiwa adhabu ya kifo itafutwa bila tathmini ya kutosha, ni watu kuacha kuogopa sheria kwa kuamini kuwa wakiua watafungwa maisha tu badala ya kunyongwa hadi kufa.

Tunashauri kwamba uwapo mjadala mpana wa kitaifa kulijadili suala hili na kupata mwafaka wa pamoja, ili baadaye jamii isijutie uamuzi huo.

Changamoto kwa THBUB, LHRC na asasi zingine za haki za binadamu ni kuandaa majukwaa ya mijadala kwa ajili ya kujadili suala hilo, ili uamuzi utakaotolewa wa kutaka adhabu hiyo kuendelea kuwapo au kufutwa uwe shirikishi na kuondoa lawama katika siku za usoni.

Habari Kubwa