Afadhali Masauni ameliona hili Nida

02Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Afadhali Masauni ameliona hili Nida

KASI ndogo ya utolewaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi, imekuwa ikielezwa kuwa inasababishwa na mambo kadhaa.

Wananchi kadhaa wamekuwa wakiitupia lawama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuwa maofisa wake ni warasimu, hivyo kusababisha kasi ndogo ya kutolewa kwa vitambulisho hivyo.

Hata hivyo, wakati mwingine malalamiko ya baadhi ya watu yanaonekana kutokuwa na mashiko kwa kuwa mchakato wa kutolewa kwa vitambulisho hivyo ulianza miaka kadhaa iliyopita.

Kimsingi, wananchi wengi hawakujitokeza au kwa lugha nyingine hawakuchangamkia fursa hiyo hadi baada ya serikali kutangaza utaratibu wa kusajili laini za simu kwa njia ya vidole gumba.

Wengi walipuuzia kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho kutokana na kutokuona umuhimu, kicha ya hamasa iliyokuwa ikitolewa, hadi baada ya kuona muda wa kuzima laini unakaribia ambao ulikuwa Desemba 31, mwaka jana, kabla ya Rais John Magufuli kuongeza siku 20 kuanzia jana hadi Januari 20.

Inawezekana Nida ikawa na udhaifu kwa baadhi ya watumishi wake, lakini si jambo la busara kuitupia lawama hizo, kwa kuwa hata baadhi ya wananchi wanakaidi kufuata maelekezo yanayotolewa na taasisi hiyo kuhusiana na taratibu za kufuata kupata vitambulisho.

Jana serikali ilibaini moja ya usumbufu wanaoupata wananchi wanapokwenda kutafuta vitambulisho hivyo, ambao ni mawakili binafsi wanatoza Sh. 6,500 kwa ajili ya kupata viapo.

Moja ya masharti ya kupata vitambulisho hivyo ni mwombaji kuwa na kitambulisho cha kuzaliwa, hivyo kama hana, anatakiwa kuapa kwa wakili au mahakamani.

Kutokana na kuona fursa hiyo, mawakili binafsi wamekuwa wakienda karibu na ofisi za Nida kwa ajili ya kuwahudumia waombaji wa vitambulisho kwa kuwapa viapo kwa malipo.

Hata hivyo, kutokana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masaini akiwa mjini Morogoro katika ofisi za Nida na kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu kutozwa kiasi hicho cha fedha, akiwapiga marufuku baadhi ya wanasheria binafsi Mkoa wa Morogoro kuwatoza fedha wananchi kiasi hicho 6,500 kwa ajili ya kugharamia hati ya kiapo, ili kukidhi vigezo vya kupata namba ya kitambulisho na badala yake ameahidi kutoa wanasheria wa serikali kutoka ofisi ya mkoa ili kusaidia kutoa huduma hiyo.

Ni kweli malipo hayo ni makubwa kwa wananchi wengi ambao kipato chao ni kidogo, hivyo kukwama kukidhi matakwa ya kupata vitambulisho vya Taifa.

Sisi tunaona kuwa kama serikali ingeweka utaratibu tangu awali wa kuwapeleka mawakili wa serikali kuwahudumia wananchi kuwapa viapo, watu wengi wangekuwa wamevipata, ingawa tunaelewa pia kwamba mawakili wa serikali hawatoshi kutoa huduma hiyo kwa Watanzania wote.

Tunaamini kuwa kama utawekwa utaratibu mzuri jambo hili linawezekana katika mikoa mingine, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, kukubali kutekeleza agizo la Masauni la kupeleka wanasheria wa serikali kusaidia.

Tunawasisitiza wananchi kufuata maelekezo ya Nida wakati wote wa mchakato wa kutafuta vitambulisho vya taifa hata baada ya kumalizika muda wa kusajili laini za simu.

Tunasema hivyo kwa kuwa vitambulisho vya taifa ni suala nyeti kwa kuwa bila mamlaka husika kuwa makini, vinginevyo inaweza kuwapa vitambulisho watu wasio raia wa nchi hii.

Habari Kubwa