Afcon inawezekana Stars ikiivaa Uganda kama fainali

18Mar 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Afcon inawezekana Stars ikiivaa Uganda kama fainali

Hatima ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufuzu ama kutofuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) itajulikana Jumapili baada ya dakika 90 ya mtanange wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Uganda ('The Cranes') utakaopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ya Kundi L, linalojumuisha pia Cape Verde na Lesotho, ni muhimu kwa Stars kushinda ili kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika nchini Misri Juni mwaka huu.

Katika kundi hilo Uganda iko kileleni ikiwa na pointi 13 ikifuatiwa na Taifa Stars yenye alama tano sawa na Lesotho, huku Cape Verde ikiburuza mkia kwa pointi zake nne.

Kwa Uganda itakuwa ikikamilisha tu ratiba kwa kuwa imeshafuzu kutokana na ukweli kwamba hakuna timu kwenye kundi lake inayoweza kufikisha pointi zake.

Lakini pamoja na kuwa na tiketi hiyo mkononi, bado Uganda ambayo katika mechi yake ya kwanza nyumbani ililazimishwa sare na Stars, huku michezo mingine minne ikishinda, inaonyesha kudhamiria kutopoteza mchezo wowote na leo imeingia kambini nchini Misri kujiandaa na mchezo huo.

Kwa ujumla licha ya Stars kuwa nyumbani, mechi hiyo haitakuwa rahisi kwao na kinyume cha ushindi haitaweza kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu 1980. Ikumbukwe kwamba Stars, Lesotho na hata Cape Verde zote zina nafasi ya kuungana na Uganda kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, endapo Stars itapoteza dhidi ya Uganda Jumapili mshindi kati ya Cape Verde na Lesotho ataungana na Uganda kufuzu fainali hizo.

Lakini pia hata kama Stars itatoka sare katika mechi hiyo ya mwisho huku timu moja kati ya Lesotho na Cape Verde ikipata ushindi iliyoshinda ndiyo itakayoungana na Uganda. Hivyo kinachotakiwa kwa Stars ili kufuzu ni kushinda tu Jumapili na si vinginevyo, jambo ambalo Nipashe tunaamini linawezekana.

Tunaamini kikosi kilichoitwa na Kocha Emmanuel Amunike, kinaweza kutimiza malengo hayo ya Tanzania kufuzu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 ingawa mechi hiyo itakuwa ngumu, hilo halitupi hofu sana kwa kuwa kama Stars iliweza kupata sare ugenini dhidi ya Uganda, kupata matokeo nyumbani ni jambo linalowezekana.

Ni wazi Amunike atakuwa ametambua ni wapi kikosi chake kilifanya makosa katika mechi iliyopita na kuyafanyia kazi kabla ya Jumapili.
Lakini pia kwa siku hizi tano kabla ya Jumapili, tunaamini zinatosha kabisa kurekebisha kasoro ndogondogo za kimfumo na Stars kuweza kupata matokeo.

Nipashe tunaamini wachezaji na benchi zima la ufundi hawatatuangusha hivyo kilichobaki ni Watanzania kwa ujumla kuelekeza dua na maombi kwa Stars ishinde.

Lakini pia tukumbuke shabiki wa soka ni mchezaji wa 12 uwanjani hususan timu inapokuwa uwanja wake wa nyumbani.

Na katika kulitambua hilo, tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), limetangaza kiingilio cha chini kabisa cha Sh. 3,000 ambacho ni rafiki kabisa kwa kila mtu mwenye mapenzi mema na Stars kumudu kwenda kuishangilia.

Hivyo, tujitokeze kwa wingi kwenda kuiunga mkono Stars kwani kwa pamoja Afcon 2019 Misri inawezekana wakati huu kikosi hicho cha Amunike kikitarajia kucheza mechi hiyo kama fainali.

Habari Kubwa