Agizo la Waziri Lugola kwa trafiki litekelezwe

21May 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Agizo la Waziri Lugola kwa trafiki litekelezwe

KWA muda mrefu madereva wamekuwa wakilalamikia tabia ya baadhi ya askari wa usalama barabarani kuwabambikia kesi za makosa ya picha za mwendokasi (speed rader).

Kilio cha madereva ni kuwa picha hizo hazina uhalisia, na kwamba lengo la askari hao ni kujipatia mapato.

Baada ya kilio hicho cha muda mrefu dhidi ya askari hao, serikali imefunguka na kutoa onyo kwa askari hao, kwamba wakiendelea na tabia hiyo watawajibishwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, andiye aliyetoa angalizo kwa askari hao, akisema kwamba trafiki wanaowabambikia madereva makosa hayo wakibainika watawajibika kuzilipa wao wenyewe faini hizo sambamba na kuondolewa katika kitengo hicho.

Alitoa agizo hilo juzi mjini Morogoro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maafikiano kati ya vyama vya watoa huduma za usafirishaji nchini kuhusu kusitisha kusudio la madereva wa mabasi ya abiria kufanya mgomo wakishinikiza kutimiziwa madai yao mbalimbali ikiwamo ya mikataba ya kazi.

Alisema maamuzi hayo yametokana na makubaliano ya pamoja kati ya viongozi wa vyama hivyo vya usafirishaji pamoja na wizara mtambuka za serikali kwa nia ya kutatua changamoto walizowasilisha katika kikao hicho kuhusu kubambikiwa makosa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Waziri Lugola, alisema moja ya makosa yanayolalamikiwa na madereva hao ni pamoja tochi zinazopiga picha mabasi na kurushwa kwenye simu za askari zinakosa uhalisia wa tukio ikiwamo kutoonekana kwa namba za usajili pamoja na vibao vya kuzuia makatazo mbalimbali na kusababisha utata na mivutano yenye nia ya kujenga mazingira ya rushwa.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kuanzia sasa askari hao wanapaswa kupiga picha katazo mbalimbali za barabara mbele ya gari ikionyesha mwonekano usio na shaka, namba ya usajili pamoja na eneo la alama iliyokiukwa na dereva ili kuwapo na ushahidi halali, vinginevyo dereva huyo asichukuliwe hatua yoyote.

Alisema dereva anapokuwa na shaka na picha iliyopigwa dhidi ya gari lake kama haionyeshi usajili wa namba za gari na eneo la kibao cha zuio asikubali kuadhibiwa badala yake amweleze huyo askari azitume picha hizo kwa msimamizi wa kikosi cha usalama barabarani na aende huko.

Uamuzi huo umetolewa wakati mwafaka, kutokana na madereva wengi kulalamikia vitendo vya baadhi ya trafiki hao ambavyo vinaashiria kuwa lengo lao ni kujitafutia kipato kupitia rushwa.

Tunatambua mchango mkubwa wa trafiki katika kusimamia usalama barabarani, ikiwamo kupunguza matukio ya ajali, lakini jambo la msingi ni kuwa hawanabudi kuelewa kuwa hawapo juu ya sheria bali wanapaswa kiziheshimu na kuzifuata.

Kwamba kinyume cha hapo watapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ni matarajio yetu kuwa askari wote wa usalama barabarani wamesikia katazo la Waziri Lugola na watalizingatia.

Kwa upande wao madereva wasikubali kutekeleza maelekezo ambayo yanakwenda kinyume cha katazo la waziri, badala yake watoa taarifa kwa mamlaka za juu kama ofisi za trafiki mikoa, makao makuu na kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, askari watakaokaidi washughulikiwe.

Sio sawa kwa askari wanaoendekeza uonevu na vitendo vya rushwa kuwageuza madereva kuwa chanzo chao mapato bila sababu za msingi.

Ifike mahali Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa itumike kuwafuatilia na kuwatia mbaroni trafiki wanaofanya vitendo hivyo ili sheria ichukue mkondo dhidi yao.

Habari Kubwa