Ahadi Serengeti Boys ikifuzu zitolewe sasa

15Apr 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ahadi Serengeti Boys ikifuzu zitolewe sasa

FAINALI za Mataifa za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon U-17), zimeanza kutimua vumbi nchini, safari hii Tanzania ikiwa mwenyeji kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo.

Utepe wa fainali hizo ulikatwa rasmi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salama jana, kwa wenyeji Serengeti Boys kucheza dhidi ya Nigeria kabla ya Angola kuvaana na Uganda, hizo zikiwa ni mechi za Kundi A.

Leo michuano hiyo itaendelea kwa upande wa Kundi B kwa Guinea kuvaana na Cameroon na baadaye tukiishuhudia Morocco ikicheza na Senegal.

Wenyeji Tanzania, Serengeti Boys watarudi tena uwanjani Jumatano kuvaana na Angola katika mechi yake ya pili kwenye mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, Caf.

Ikumbukwe michuano hiyo ndiyo itakayotoa wawakilishi wanne wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia U-17 zitakazofanyika nchini Brazil Oktoba mwaka huu. Na kwa mujibu wa Caf, mshindi wa kwanza na wa pili kutoka katika kila kundi atafuzu moja kwa moja fainali hizo za Kombe la Dunia.

Kutokana na mchakato ulivyo, timu itakayoshinda mechi mbili tu, itakuwa tayari imejihakikishia tiketi ya kushiriki fainali hizo Oktoba mwaka huu.

Hivyo, kinachotakiwa kwa sasa ni kuendelea kuisapoti Serengeti Boys ndani na nje ya uwanja ili iweze kufuzu kwani ushindi wake ni wa Watanzania wote.

Tunatumai Watanzania kwa ujumla wataendelea kujitokeza kwa wingi kuisapoti Serengeti Boys kama walivyotumia vema nafasi yao kwa kuwasapoti kaka zao, Taifa Stars dhidi ya Uganda (Cranes) na hatimaye kufuzu Afcon 2019 nchini Misri.

Tunatambua shabiki ni mchezaji wa 12 kwa timu inapokuwa dimbani, hivyo Watanzania hatuna budi kuitumia nafasi hiyo muhimu hasa ukichukulia michuano hii inafanyika ardhi ya nyumbani, kwani mahudhurio ya jana hayakuwa na afya kama ambavyo wengi walijitokeza kwenye mechi ya Stars dhidi ya Uganda.

Hatuna budi kuanza kwa kuhakikisha tunakuwa kitu kimoja kwa kuisapoti kwa hali na mali ifuzu kwanza Kombe la Dunia na kisha ndipo tugeukie kutumia nafasi zetu kuiwezesha kutwaa ubingwa huo wa Afcon U-17.

Hata hivyo, ili kuhakikisha hilo linawezekana, kama ambavyo tumeona Mlezi wa Serengeti Boys, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akiahidi kutoa Sh. milioni 20 kwa kila mchezaji endapo watafuzu Kombe la Dunia, ndivyo ambavyo kwa wingi wetu tunatakiwa kujitokeza kutoa ahadi zetu sasa.

Kuna 'kautamaduni' kamejengeka kusubiri hadi mafanikio yapatikane ndipo mhusika aanze kuzawadiwa na ahadi kedekede zikitolewa, katika hilo Watanzania tunapaswa kubadilika sasa kwa kuiga hiki kilichofanywa na Dk. Mengi kwa kuwaahidi mapema Serengeti Boys mamilioni ya shilingi kila mmoja.

Nipashe tunaamini ahadi kama hizo zikitolewa mapema zitaongeza morali ya kupambambana kwa wachezaji na hatimaye kufuzu kirahisi na kabla ya kuutwaa kabisa ubingwa huo.

Lengo letu ni kuona Tanzania ikiandika historia mpya kwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia na kutwaa ubingwa wa U-17 mwaka huu, hivyo hilo linaweza kutimia kirahisi zaidi kama wote tukiguswa kama Dk. Mengi kwa kuwaongezea ari Serengeti Boys.

Kunapokuwa na zawadi mbali ya kufuzu Kombe la Dunia na kutwaa ubingwa huo, ni wazi moyo na ari ya kujituma zaidi itaongezeka kuliko kusubiri mwishoni baada ya timu hiyo kupata mafanikio.

Hivyo, ni matarajio yetu Watanzania wenye mapenzi mema ya kuona Serengeti Boys inapata mafanikio hayo mbali na kwenda uwanjani kuisapoti, watajitokeza sasa kutoa ahadi kwa wachezaji ili kuwaongezea kiu ya kufikia malengo yao hayo.

Na katika hili Nipashe tunapenda kusisitiza kuwa halihitaji hadi uwe na mamilioni ndipo ujitokeze kuahidi, kwa kuwa kidogo chako ni kikubwa katika kuyatafuta mafanikio kwa vijana hawa waliodhamiria kuitoa kimasomaso Tanzania. Tunaitakia Kila la Kheri Serengeti Boys.

Habari Kubwa