Ahadi ya serikali kwa wastaafu itekelezwe

19May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ahadi ya serikali kwa wastaafu itekelezwe

SERIKALI imewaahidi wastaafu kwamba imejipanga kumaliza kutatua changamoto ya kupata mafao yao mapema kuanzia mwaka ujao wa fedha.

Katika kushughulikia hilo, imesema kuwa imewaweka katika kipaumbele cha kuhakikisha wanapewa mafao yao kwa wakati.

Imesema kuwa imeendelea kufanya uhakiki wa daftari la pensheni kila mwezi kabla ya malipo, kuandaa vitambulisho vipya vya wastaafu vya kielektroniki katika mfumo wa “smart cards” na kuboresha mfumo unaotumika kutoa huduma kwa njia ya mtandao.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ndiye aliyewapa matumaini hayo wastaafu mwishoni mwa wiki bungeni, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za wabunge waliotaka kufahamu mikakati ya serikali katika kuhakikisha mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati.

Katika kutoa majibu ya hoja hizo zilizoibuliwa na wabunge waliochangia katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, Dk. Mpango alisema kinachochelewesha wastaafu kulipwa kwa wakati ni udhaifu katika taarifa, lakini mikakati inaandaliwa ya kuhakikisha wazee waliolitumikia taifa wanastaafu vizuri na kwa amani.

Kwa mujibu wa Waziri Mpango, suala la malipo ya mafao ya wastaafu ni miongoni mwa vipaumbele vya Wizara kuhakikisha wastaafu wanastaafu vizuri.

Alifafanua zaidi kuwa, wizara inawajibika kulipa mafao na pensheni kwa watumishi wa umma, ambao hawachangii katika mifuko ya hifadhi ya jamii, mirathi na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi wa Serikali walio katika mikataba na viongozi wa kisiasa.

Ahadi ya Waziri Mpango kuhusiana na malipo ya mafao wa watumishi wa staafu wa umma kulipwa mapema ni ya pili kutolewa mwaka huu na serikali.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, alisema aliahidi kuwa serikali itahakikisha malipo hayo yanalipwa mapema.

Mkuchika alisema wameshabaini kuwa wanaosababisha malipo hayo kuchelewa kulipwa ni maofisa utumishi, ambao alisema wanachelewa kuandaa utaratibu wa kuwalipa, na kuonya kuwa atakayesababisha ucheleweshaji huo atachukuliwa hatua.

Kimsingi, watumishi wengi wastaafu wa umma bado wanaendelea kusotea malipo ya mafao yao, hali inayowafanya waishi katika hali ngumu ya maisha na unyonge.

Baadhi wanalalamikia urasimu kwamba wanapoenda kudai wanaelezwa waende makao makuu ya serikali Dodoma, hivyo kuwapa wakati ngumu, kwa kuwa kwenda Dodoma wanatakiwa kuingia gharama kubwa za usafiri, chakula na malazi.

Kwa ahadi hii ya Waziri Dk. Mpango ya kutatua changamoyo ya muda mrefu ya malipo ya mafao ya watumishi wastaafu wa umma, ni matarajio yetu kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha, hatutawasikia tena wastaafu wakilalamikia malipo ya mafao yao na kuendelea kunyanyasika.

Sisi Nipashe tunaona kuwa Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ndizo zinazohusika katika mchakato wa ulipwaji wa malipo ya mafia kwa watumishi wa umma.

Kutokana na hali hiyo, kuna umuhimu wa kuwapo kwa utaratibu wa mamlaka hizi kuwa na vikao vya pamoja kwa ajili ya kufuatilia mchakato wa ulipaji wa mafao ya watumishi wa umma kwa wakati mwafaka.

Hatua hii itawezesha kuondoa urasimu, uongo na ubabaishaji wa watumishi wachache wanaokwamisha malipo ya mafao ya watumishi wastaafu, hivyo kuipaka doa serikali.

Kwa jinsi Mkuchika na Dk. Mpango walivyoeleza kuguswa na kunyanyasika wastaafu katika kudau malipo yao, bila shaka watahakikisha kuwa tatizo hilo linamalizika kuanzia mwaka ujao wa fedha, hivyo kuthibitisha kivitendo kuwa serikali ya Rais John Magufuli inawatetea na kuwajali wanyonge.

Habari Kubwa