Ajira mpya afya zipunguze taabu

08Nov 2017
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajira mpya afya zipunguze taabu

SERIKALI imetoa ajira 2,058 za sekta ya afya ambapo watumishi hao watasambazwa katika wilaya mbalimbali nchini, kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Seleman Jafo.

Inafahamika kuwa sekta ya afya, ndiyo iliyo muhimu zaidi katika ustawi wa jamii kuliko nyingine yoyote, hasa kutokana na kuhusiana moja kwa moja na uhai wa binadamu.

Na inafahamika pia kuwa sekta ya afya, pengine, ndiyo yenye upungufu mkubwa wa watumishi wa kada mbalimbali kuliko sekta nyingine zozote za huduma ya jamii nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya za mwanzoni mwa mwaka kwa mfano, nchi ilikuwa ikihitaji na upungufu wa madaktari 3,510 na katika idadi hiyo, mahitaji zaidi yapo kwenye hospitali za wilaya walikokuwa wakihitajika madaktari 832.

Na upugufu wa madaktari, tunafahamu Nipashe, ni tone tu katika changamoto ya ukosefu wa watumishi wa afya kabla ya uamuzi wa serikali wa kuajiri watumishi zaidi ya 2,000 hao wiki hii.

Changamoto ya ukosefu wa watumishi wa afya kabla ya uamuzi wa serikali wa kuajiri watumishi zaidi ya 2,000 hao wiki hii, tunasema Nipashe, kwa sababu nje ya madaktari hali ni mbaya zaidi.

Nje ya madaktari hali ni mbaya zaidi, tunasema Nipashe, kwa sababu tangu takwimu za mwanzoni mwa mwaka, serikali iliingia katika zoezi la kuondoa watumishi wenye vyeti feki ambako wauguzi na wauguzi wa wasaidizi wengi walikuwa miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 9,000 wa aina hiyo katika utumishi wa umma waliogunduliwa.

Na tuliandika habari nyingi kama moja ya vyombo vya upashaji, Nipashe, juu ya hali ngumu iliyovikuta vituo vya afya katika wilaya mbalimbali nchini ambako baadhi vilipoteza mpaka wastani wa asilimia 70 ya watumishi wake.

Katika mazingira hayo, taarifa ya kutolewa kwa ajira 2,058 za sekta ya afya ambapo watumishi hao watasambazwa katika wilaya mbalimbali nchini, ni taarifa njema ambayo tunataraji, Nipashe, itapunguza taabu ambazo wananchi walikuwa wakikutana nazo katika zahanati na vituo vya afya.

Tunafahamu, hata hivyo, Nipashe, kuwa kutolewa kwa ajira peke yake tu hakutokuwa msingi wa kupatikana kwa ahueni hiyo kwa wananchi kama waajiriwa wenyewe hawatokwenda kufanya kazi kwa moyo, upendo na uzalendo juu ya wananchi wenzao.

Bahati nzuri, serikali imeshaweka mazingira mazuri ya watumishi hao kukosa visingizio vya kuzembea kazini baada ya Waziri Jafo kuagiza wakurugenzi wa halmshauri si tu kuwapangia vituo vya kazi mara moja waajiriwa hao bali pia kupatiwa stahiki zao kabla ya kuanza ajira hizo.

Tunafahamu siku za nyuma, kutokana na serikali kutotimiza malipo kwa wakati na hivyo kupelekea kuwapo kwa malimbikizo ya madai mbalimbali, watumishi wa umma, wa sekta ya afya wakiwemo hawakuwa na morali ya kazi.

Lakini kwa kuwa serikali ya awamu ya tano ni ya kazi tu, na kwa kuwa itakuwa imeshamaliza kazi ya kulipa stahiki za watumishi hao kabla ya kuondoka vituoni mwao, wakafanye kazi kweli kweli.