Alama ya Mkapa madarakani iwafundishe viongozi wengine

15Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Alama ya Mkapa madarakani iwafundishe viongozi wengine

JANA ilikuwa ni kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Mkapa, aliyezaliwa katika Kijiji cha Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara, kukiwa na mjadala na salamu kutoka kwa watu maarufu duniani, katika kongamano hilo ambalo mgeni rasmi alikuwa ..

Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayati Mkapa ni rais ambaye atakumbukwa kwa mengi ambayo alijenga msingi thabiti na hadi sasa yanaendelea na yataendelea kugusa maisha ya kila Mtanzania, pia viongozi wa kimataifa wamepaza sauti kupitia mtandao na wengine walikuja nchini kwa ajili hiyo, akiwamo Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, Tony Blair.

Alama za Hayati Mkapa zinaishi na zimeendelea kuisaidia nchi hasa katika uanzishaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akiwa na kaulimbiu ya kodi kwanza, pia alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao umeendelea kuwapo hadi sasa.

Alama nyingine ni kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mfuko wa Barabara ambao uliwezesha kujengwa kwa barabara nyingi za kuunganisha mikoa, wilaya na kazi ambayo iliendelezwa na Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete na baadaye Hayati Joseph Magufuli.

Aidha, Mkapa ameacha alama ya kupambana na umaskini kwa kuanzisha Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), pia wakati wake ulianzishwa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA), ambao ulilenga kuinua hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kwenye elimu Mkapa anakumbukwa kwa kuanzisha Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) na Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa Walioikosa (MMES) na shule za mwanzo kabisa za kata ambazo zilisaidia wanafunzi wengi kuendelea na masomo ya sekondari, kutokana na wengi kufaulu, lakini wapo waliokaa nyumbani kwa kukosa shule za kwenda kusoma na kuanzia hapo rais aliyefuata aliendeleza utaratibu huo na kukawa na mwamko mkubwa wa kila kata kuwa na shule ya sekondari.

Kutokana na mipango hiyo watu wengi walijiendeleza kielimu na kuwa na elimu ya msingi, sekondari na baadhi walifika hadi vyuo vikuu, walimu wa UPE (Universal Primary Education) walijiendeleza na kupata vyeti vya kidato cha nne na sita, huku wengine wakifika vyuo vikuu na hata walivyostaafu walikuwa kwenye hali nzuri zaidi ya kipato kutokana na kupanda madaraja.

Eneo jingine ni kwenye afya ambalo baada ya kustaafu alianzisha Mkapa Foundation ambayo ilijikita kwenye kuboresha afya maeneo ya vijijini ikiwamo kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuikabidhi serikali, pamoja na kutoa vifaa tiba muhimu.

Hali hii ilisaidia sana maboresho makubwa ya huduma za afya hasa vijijini na hadi sasa wameendelea na kazi hiyo, na pia anakumbukwa kwa kuanzisha Tume ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS), ambayo ilisaidia mengi kwenye eneo hilo ikiwamo kutoa afua mbalimbali, elimu ya Ukimwi na udhibiti ikiwamo kuwa na miongozo mbalimbali ya utaoji huduma.

Pia Mkapa alianzia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo imesaidia kupambana na rushwa na kuna nyakati ilionekana kushamiri kiasi cha huduma muhimu za kijamii kuuzwa badala ya kutolewa bure.

Alama ya Mkapa ipo pia kimataifa kiasi cha kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro mingi na unaokumbukwa sana ni wa mwaka 2007 nchini Kenya, baada ya uchaguzi Mkuu ambao ulitawaliwa na vurugu na vifo vya baadhi ya watu, lakini kwa kushirikiana na viongozi wengine Mkapa aliongoza timu ya usuluhishi.

Habari Kubwa