Amunike, nyota Stars wanahitaji kuaminiwa

08Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Amunike, nyota Stars wanahitaji kuaminiwa

KIKOSI cha wachezaji 32 wanaounda Timu ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars), kiliondoka nchini kuelekea Misri kwa ajili ya kuendelea na mazoezi ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019).

Fainali hizo zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinatarajiwa kuchezwa kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu kwa kushirikisha timu 24.

Taifa Stars ni moja kati ya timu zilizofuzu kucheza fainali hizo, na imepangwa katika Kundi C ikiwa na nchi za Senegal, Algeria na majirani zetu kutoka Afrika Mashariki , Kenya maarufu Harambee Stars.

Katika kujiweka imara kabla ya kuanza kwa fainali hizo, Taifa Stars inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji Misri na Zimbabwe.

Mechi hizo mbili za kirafiki, ni moja ya sababu ya kikosi cha Stars kuamua kwenda mapema Misri, ili kuanza kuzoea hali ya hewa ya nchi hiyo ambayo ni tofauti na iliyoko jijini Dar es Salaam, mahali ambapo 'askari' wa Tanzania walianza kujinoa.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko na mitazamo tofauti baada ya Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike, kutangaza wachezaji wanaokwenda Misri, ikiwa ni mchujo wa awali.

Wakiwa Misri, Mnigeria huyo atafanya tena mchujo na kubakisha idadi ya wachezaji 23 ambao ndio wanatakiwa kusajiliwa kwenye michuano hiyo, kama kanuni za CAF zinavyoelekeza.

Nipashe linawataka wadau kumpa ushirikiano Amunike ili aweze kuiongoza vema timu hiyo kama alivyokuwa akipambana katika  safari ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali hizo, ambazo Watanzania tulizikosa kwa miaka 39.

Kumekuwa na maoni tofauti baada ya kocha huyo kutangaza kuwaacha nyota sita, katika mchujo wa awali akiwamo, nahodha na mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu na kiungo wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Jonas Mkude.

Amunike ndiye kiongozi mkuu wa benchi la Stars, uwezo wake ndio ulifanya akapewa dhamana ya kuiongoza timu hiyo, hivyo anatakiwa kuungwa mkono kwa ajili ya kupambana na kupata matokeo chanya kwenye michuano hiyo ambayo atakutana na vigogo wa Afrika Magharibi.

Kama wadau wataendelea kuona uamuzi wa kuwaacha Mkude na Ajibu, haikuwa sahihi, hali hiyo inaweza kuwavunja moyo wachezaji ambao wamebakia kwenye kikosi hicho, wakashindwa kupambana kutokana na kuonekana hawana uwezo ukilinganisha na nyota hao waliotemwa.

Amunike ameweka wazi kuwa yeye ataendelea kuamini kwamba mchezaji bora ni yule mwenye uwezo wa juu na mwenye nidhamu, bila ya kuzingatia anatoka timu gani, na kufunguka zaidi kuwa sifa hizo ni baadhi ya vitu vilivyomfanya yeye apate nafasi ya kucheza soka katika klabu kubwa ya Barcelona huko Hispania.

Kama wadau wataendelea kuanza kuwagawa wachezaji, hilo linaweza kupunguza morali kwenye kikosi hicho ambacho kinasubiriwa kuwapa burudani Watanzania ambao kwa muda mrefu walikuwa watizamaji.

Gazeti hili linawaomba wadau wa michezo na hasa wa mpira wa miguu kumpa ushirikiano Amunike pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanikisha Stars kufanya vema katika fainali hizo na si kusindikiza timu nyingine.

Kila la kheri Taifa Stars, Kila la kheri Tanzania. Afcon 2019 Ni Zamu Yetu.

Habari Kubwa