Angalizo la Makamu wa Rais mazingira litekelezwe

02Aug 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Angalizo la Makamu wa Rais mazingira litekelezwe

UTEKELEZAJI wa miradi mikubwa umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu sana na serikali pamoja na wadau wa mazingira, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mazingira yanabaki salama bila kuathiriwa.

Serikali ina utaratibu wa kufanya tathmini ya athari za mazingira pale mwekezaji anapojiandaa kuanzisha mradi, na pale inapobainika kuwa kutakuwapo na athari za mazingira mradi huo hauwezi kukubaliwa wala mhusika kupewa cheti kutoka kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Aidha, wadau na mashirika yasiyo ya kiserikali hususan yanayojihusisha na masuala ya mazingira yamekuwa yakifuatilia kwa karibu miradi inayotekelezwa nchini, na pale inayobainika kuwa itasababisha athari za mazingira wamekuwa wakiendesha kampeni za kukosoa serikali isiikubali kutekelezwa.

Moja ya miradi mikubwa ambayo wadau wa mazingira walifanya kampeni kubwa ya kuupinga ni wa kufuga samaki aina ya kamba katika Delta ya Rufiji mkoani Pwani mapema miaka ya tisini. Hakika jitihada zao zilifanikiwa baada ya ukweli kubainika bila kuacha shaka yoyote kwamba ungesababisha uharibifu wa mazingira, ikiwamo kukatwa kwa miti aina ya mikoko.

Jitihada mbalimbali za kulinda mazingira ambayo ni moja ya ajenda muhimu katika suala la maendeleo endelevu zimekuwa zikiendelea kufanywa na serikali pamoja na wadau.

Kwa mfano, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema kuna mzigo mkubwa wa kutunza mazingira katika mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Rufiji ili kuhakikisha maji yanatiririka na hayazuiliki kwa shughuli yoyote.

Makamu wa Rais alitoa kauli hilo juzi  jijini Dodoma alipokuwa akifungua Jukwaa la Maendeleo Endelevu kuhusu usimamizi bora wa misitu kwa upatikanaji wa rasilimali maji endelevu lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

Samia alisema kwamba  ni lazima kujipanga vizuri ili maji yaweze kutiririka kuanzia vyanzo vya juu vya eneo hilo na yasizuilike popote.

Kwa mujibu wa Samia, kila mmoja anajua mabwawa ya maji makubwa yanayozalisha umeme ni kwa maendeleo ya taifa, na tunajua mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Rufiji utategemea mtiririko endelevu wa maji kutoka vyanzo vikuu ikiwamo mito na madakio ambayo yanaanzia kwenye misitu na maeneo mengine.

Kwamba mwaka juzi kulikuwapo  na kampeni ya utiririshaji maji katika Mto Ruaha kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa kipindi hicho.

Samia alisema wanyama wanahitaji sana maji katika maeneo ya hifadhi kiasi cha kuweka foleni kiasi cha kutegemea tembo wakati mwingine wawasaidie wengine kuchimba kama alivyowahi kushuhudia katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Kwa hiyo jamii nzima ya Watanzania tunapaswa kuichukulia kauli ya Makamu wa Rais kama changamoto  katika suala  zima ambalo yeye ameliita kuwa ni mzigo mkubwa wa kutunza mazingira katika mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Rufiji ili kuhakikisha maji yanatiririka na hayazuiliki kwa shughuli yoyote.

Samia akisema hivyo akimaanisha umuhimu mkubwa wa kulinda mazingira katika eneo hilo ambalo limeanza kujengwa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji megawati 2,100, hivyo kuisaidia nchi yetu kumaliza changamoto kubwa na ya muda mrefu ya uhaba wa nishati ya umeme.

Tumaamini kuwa kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anazingatia ushauri huo, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa maji ya Rufiji yanaachwa yatiririke bila kuzuiliwa kwa ajili ya shughuli nyingine ambazo zinaweza kusababisha athari za mazingira.

Habari Kubwa