Angalizo la TPSF kuhusu kupunguza wafanyakazi sahihi

25Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Angalizo la TPSF kuhusu kupunguza wafanyakazi sahihi

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imewaasa wanachama wa taasisi hiyo, wasitumie ugonjwa wa corona kupunguza wafanyakazi katika viwanda au kampuni wanazozimiliki.

Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Angelina Ngalula, ndiye aliyetoa angalizo hilo alipokuwa akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, kwa kusema kwamba Tanzania na dunia kwa jumla zinapita katika kipindi kigumu kutokana na ugonjwa wa corona.

Hata hivyo, alisema kuwa siyo busara kutumia tatizo hilo kupunguza wafanyakazi.

Alisema kupunguza wafanyakazi litakuwa ni tatizo kubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo aliwaomba waajiri kote nchini tushughulikie changamoto zilizopo kwa pamoja ili kulinda ajira nchini.

Ngalula alieleza zaidi kuwa kutumia matatizo kujinufaisha siyo utamaduni wa Watanzania.

Alizitaka baadhi ya sekta mfano utalii na kilimo, ambazo zimeathirika moja kwa moja kutokana na ugonjwa wa corona zikusanywe taarifa zinazoonyesha namna mtu mmoja mmoja alivyoathirika na taarifa hizo ziwasilishwe kwenye kikosi kazi ambacho kimeshaundwa.

Kwa mujibu wa Ngalula, taarifa hizo zitachambuliwa na wataalamu wao na kufikishwa serikalini, na kuonya kuwa waajiri wasitengeneza makundi yenye lengo la kujinufaisha badala yake Watanzania waendelee kufanya kazi kama Rais John Magufuli alivyoelekeza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, aliiomba serikali kuondoa baadhi ya tozo kwa taasisi au kampuni zitakazoathiriwa na corona.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga, alisema kutumia corona kupunguza ajira ni kuhatarisha uchumi wa nchi.

Taasisi hizi mbili zimetoa angalizo hilo pengine baada ya kufuatilia kinachoendelea katika sekta mbalimbali, na kubaini kuwa kuna uwezekani kwa wafanyakazi kupoteza ajira zao kwa kisingizio cha ugonjwa wa corona.

Tunakubaliana na angalizo hili tukiamini kuwa wako baadhi ya waajiri ambao watatumia kisingizio cha janga la corona kuwaondoa kazini wafanyakazi wakati hakuna athari zozote kiuchumi ambazo zimetokea nchini hadi sasa.

Maelekezo yaliyotolewa na Rais Magufuli Jumapili, tunaona kuwa yanaweza kuwa mwarobaini wa athari za kiuchumi kwa nchi yetu, kwa kuwa wananchi wakiendelea na uzalishaji bila kujifungia ndani, wataendelea kuzalisha na kujipatia kipato na wakati huo huo serikali ikiendelea kupata kodi na kutoa huduma muhimu zikiwano za kijamii.

Ndiyo maana ATE kupitia kwa Dk. Aggrey Mlimuka, imesema huu si wakati mwafaka kwa watu kufungiwa ndani kwani
athari zake zitakuwa kubwa kwenye ajira na uchumi wa nchi utaporomoka.

Zipo nchi zimefunga ofisi zote za umma na binafsi kukabiliana na ugonjwa wa corona, lakini kwa nchi yetu na nyingine zinazoendelea hazina uchumi mkubwa wala bajeti ya ziada kwa ajili ya kufanya hivyo.

Msisitizo wetu ni kuwa hatua za tahadhari zilizoshatolewa na zinazoendelea kutolewa na serikali yetu ziendelee kutekelezwa, huku kila mwananchi popote alipo akiendelea kuchapa kazi kwa bidii ili taifa letu lisisimame.

Tunaamini serikali itatumia mamlaka yake kuhakikisha waajiri wenye nia ovu kupunguza wafanyakazi bila sababu za msingi wanadhibitiwa.

Habari Kubwa