Asante JPM kwa kuliona hili

07Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Asante JPM kwa kuliona hili

JANA kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini, Rais John Magufuli aliwaonya wapelelezi wa kesi na wasimamizi wa sheria kwa alichokisema kuwaumiza wanaopelekwa mahabusu kwa kuchelewesha kazi kwa wakati.

Pia, akielezea suala hilo amesema wapelelezi wa kesi wamekuwa chanzo cha watu kuwekwa kwenye magereza bila hatia huku wengine wakiwekwa kutokana na shinikizo la matajiri.

Kauli ya Rais Magufuli imetoa faraja kubwa hasa kwa watu wenye ndugu zao wanaoteseka gerezani na mahabusu kwa kucheleweshewa upelelezi wa kesi zao huku kila siku wakipangiwa tarehe za kurudi mahakamani.

Baadhi ya watu waliopo mahabusu wanadaiwa kuwekwa huko kwa uonevu na kujikuta wakikaa miaka mingi bila kushughulikiwa madai yao kwa wakati.

Kumekuwa na malalamiko miongoni mwa familia zenye ndugu waliopo kwenye mahabusu kwa uonevu wa kufanyiwa visasi na watu wenye uwezo pengine kwa sababu ya kutoelewana kwenye kitu hata kisicho na msingi ili kumkomoa mtu asiyekuwa na hatia.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa dini nchini kuwaombea wapelelezi wanaofanya vitendo hivyo wapate laana.

Ameeleza idadi ya wafungwa waliopo katika magereza nchini ni ndogo ikilinganishwa na mahabusi na kutaja idadi ya wafungwa kuwa ni 13,455 wakati mahabusi wakiwa 17,632.

Kwa takwimu hizi inaonyesha jinsi gani kiwango hicho cha mahabusi ambao kesi zao hazishughulikiwa wanavyotekeseka. Wengine wanakaa zaidi ya miaka minne bila upelelezi kukamilika na suala lake linapofanyiwa kazi hukutwa hakuwa na hatia.

Jambo hili linakatisha tamaa na wananchi kutokuwa na imani na watu waliopewa mamlaka ya kusimamia haki zao.

Rais Magufuli alitaja idadi ya mahabusi walioachiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) baada ya kubainika kubambikiziwa kesi kuwa ni 1,422.

“Mimi nimeshuhudia ukienda kwenye magereza yetu watu wanalia na wengine ni kesi za kusingiziwa, wapo wengine wamewekwa kule ndani kwa sababu ya matajiri kwamba akitaka kukukomesha utaenda kwanza mahabusu.”

Serikali kila mara imekuwa ikilalamikia gharama za kuwahudumia wafungwa na mahabusi za kuwalisha na pengine matibabu wanapokuwa wagonjwa.

Gharama hizi za kuwahudumia wafungwa na mahubusi, zingeweza kutumika katika suala lingine la maendeleo kwa kupunguza idadi ya watu wanaokaa kwenye magereza na mahabusu kwa muda mrefu kwa sababu ya kesi zao kutoshughulikiwa upelelezi kwa wakati.

Ni matarajio yetu kuwa kwa kauli hii ya Rais, waliotajwa kuwa chanzo cha msongamano kwenye magereza na mahabusu, wataichukua kama changamoto na kuifanyia kazi ili haki iweze kutendeka bila upendeleo na Watanzania wawe na Imani na waliopewa jukumu la kuwashughulikia.

Kila kazi ina changamoto yake, lakini zinapofanyiwa kazi huondoa malalamiko na hata wanaopewa huduma huondoa malalamiko kutokana na kuridhika na huduma wanayopewa.

Ni matumaini yetu kuwa changamoto iliyotolewa kwa wapelelezi itakuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu yao kwa weledi na umakini.

Mungu ibariki Tanzania.

Habari Kubwa