Asasi zikitumika vizuri zina mchango mkubwa

07Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Asasi zikitumika vizuri zina mchango mkubwa

Asasi zisizo za kiserikali zina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa namna mbalimbali.

Asasi hizi zinafanya mambo mengi na mazuri, hivyo kuisaidia serikali katika mambo mengine ambayo utekelezaji wake una changamoto.

Kimsingi, serikali haiwezi kufanya kila kitu katika kuwaletea wananchi maendeleo, kwa sababu wakati mwingine inakabiliwa na ufinyu wa bajeti.

Kwa hiyo asasi hizo zimekuwa zikichangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa ikiwamo kutoa ajira kwa wananchi pamoja na kusapoti miradi kadhaa ya maendeleo ambayo serikali ingetakiwa kuitekeleza kwa kutumia fedha nyingi.

Maadhimisho ya Wiki ya Azaki yanayofanyika jijini Dodoma yamebainisha bila kuacha shaka kuhusiana na namna gani azaki zinatoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na maendeleo kwa ujumla.

Mambo yaliyobainishwa kuchangiwa na azaki hizo katika uchumi wa taifa ni dhahiri kuwa yangegharimu fedha nyingi za walipakodi, ambazo kwa sasa zinatukuka kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo mikubwa ya kimkakati.

Aliyoyaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze, kuhusiana na mchango wa Azaki katika uchumi wa taifa, yanaakisi uhalisia.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuwasilisha mada ya mchango wa asasi za kiraia kwenye uchumi wa nchi, ikiwa sehemu ya maadhimisho hayo jijini Dodoma juzi, Eyakuze, alisema kwamba katika utafiti walioufanya kwa kipindi ya miaka mitatu 2016-2018, mchango wa asasi za kiraia 16 kwenye uchumi wa nchi ni kiasi cha Sh. bilioni. 236.

Alisema kiasi hicho cha fedha kilichopatikana kutokana na asasi za kiraia kwa kipindi cha miaka mitatu ni sawa na kilo 2,181 za dhahabu zinazosafirishwa na kuuzwa nje.

Pia, kiasi hicho cha fedha ambacho kimechangiwa na asasi hizi 16, kwa kipindi hicho ni sawa na serikali kuingiza watalii 42,316 na kukaa nchini kwa wiki moja au ni sawa na lita 247 milioni za petroli, dezeli na mafuta ya taa, na kuwa katika kipindi cha miaka mitatu 2016/18 kiasi cha kodi ambayo imelipwa na azaki hizo 16 kwa serikali ni Sh. bilioni 19.

Kwamba kiasi hicho cha kodi kilichokusanywa kwa kipindi hicho ni sawa na mapato yatokanayo na maji ya kunywa, vinywaji laini na sigara ya mwaka 2018/19 ambayo yalikuwa ni Sh. bilioni 18.8.

Au kiasi hicho cha kodi kilichokusanywa kinaweza kulinganisha na kodi iliyokusanywa na Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) 2018/19 katika mikoa ya Rukwa, Lindi, Simiyu, Songwe na Katavi kwa pamoja ambayo makusanyo yao ni Sh. bilioni 21.

Mchango huu ni mkubwa kwa uchumi wa taifa letu, hivyo kwa maoni yetu tunaona kuwa azaki ziendelee kuwa mdau mkubwa wa serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa serikali inauona mchango huo na kuuthamini, kwa kuwa unawezesha wananchi na taifa kupata maendeleo na kupaa kiuchumi.

Tunashauri kuwa serikali iendelee kuziwekea azaki mazingira mazuri ya kufanyia kazi, ili ziendelee kuchangia katika maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa.

Kwa upande mwingine, azaki nazo ziwajibike kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, ili kuepuka kuingia katika migogoro na serikali.

Ni jambo la kutia moyo kusikia kwamba serikali inathamini mchango huo kutokana na kauli iliyotolewa katika maadhimisho hayo na Mratibu wa Asasi za kiraia nchini kutoka Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- Tamisemi), Denis Londo, kwamba asasi la kirai zina mchango mkubwa kwa taifa.

Habari Kubwa