Askofu Mokiwa na wafuasi wakubali

14Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Askofu Mokiwa na wafuasi wakubali

KANISA la Aglikana Tanzania juzi lilimemtoa rasmi katika uongozi, aliyekuwa askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa.

Hatua hiyo ya mwisho ya kukamilisha mchakato wa kumuondoa kwenye mamlaka Askofu Mokiwa iliyoanza Januari 7, ilifikiwa kwenye Ibada Kuu ya Kiaskofu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye magazeti mbalimbali jana, Nipashe likiwamo, tamko rasmi la kumuondoa Askofu Mokiwa katika mamlaka ya kuongoza Dayosisi ya Dar es Salaam, lililosomwa na Msajili wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Profesa Kalamagamba Kabudi.

Tuchukue fursa hii, kwanza Nipashe, kusema mgogoro wowote wenye sura ya udini, hata kama ni kwa kiwango cha dhehebu, si hali nzuri kijamii kwa sababu imani ya kidini, tunaona, ni moja ya nguzo muhimu katika ujenzi wa taifa lenye amani.

Hatudhani, Nipashe, kwamba panaweza kuwa na taifa lenye amani ya kweli, kama Tanzania ilivyo, kwa mfano, kwa sababu tu ya uwepo wa nguvu za kutisha za dola, kwa mfano, au kutokana na sheria kali zinazoogopesha watu wote wakati wote.

Kwa sababu imani ya kidini ni muhimu katika kuwa na taifa lenye amani, tuchukue fursa hii Nipashe kumuomba Askofu Mokiwa na Waanglikana wote ambao wapo nyuma yake, wachukue tamko la Msajili wa Kanisa la Anglikana Tanzania la juzi kuwa hitimisho la mgogoro unaohatarisha si tu amani ya nchi, lakini pia kuligawa kanisa lenyewe.

Kama ambavyo Askofu Chimeledya alisema, suala hilo limekwisha na ndivyo tungependa kuwashauri waumini wa kanisa la
Anglikana kwa ujumla kuona kuwa hakuna hatua nyingine tena inayoweza kuchukuliwa na Askofu Mokiwa au wafuasi wake.

Kama ambavyo Dk. Chimeledya alisema baada ya ibada hiyo, Nipashe pia tunasisitiza kuwa malumbano hayana nafasi tena.

Kama ambavyo Dk. Chimeledya alisema baada ya ibada hiyo, Nipashe pia tunasisitiza waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam kusonga mbele katika kazi ya kanisa hilo ya kumtumikia Mwenyezi Mungu. Basi.

Askofu Mokiwa akubali kubaki kama askofu mstaafu asiyekuwa na dayosisi, na bahati nzuri ni kuwa ana ruhusa ya kufanya shughuli za kikanisa kwa idhini ya askofu wa dayosisi husika.

Aidha, tuchukue fursa hii pia, Nipashe, kwanza kumpongeza Venerable Canon Jerome Napella kwa kuteuliwa kuwa Msimamizi wa Dayosisi.

Lakini pia, tuchukue fursa hii, Nipashe, kumshauri Canon Napella kufanya kila awezalo kuunganisha waumini wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam kuwa tena kitu kimoja baada ya uhasama ambao ulitishia kuligawa kanisa.

Moto huu uchunguzwe

Toeo la jana la Nipashe lilikuwa na habari iliyosema nyumba 55 ziliteketea kwa moto mwishoni mwa wiki iliyopita katika kisiwa cha Kasalazi, wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Habari hiyo ilieleza zaidi, hata hivyo, kuwa hilo ni tukio la pili kisiwani humo katika kipindi kisichozidi miezi mitatu.

Aidha, habari hiyo ilisema kuungua kwa nyumba 55 hizo ni tukio la tano kutokea kisiwani humo na kusababisha hasara za mamilioni ya fedha kwa wavuvi.

Tungependa kushauri, Nipashe kufanyika kwa uchunguzi wa kina wa matukio hayo maana si jambo la kawaida.

Habari Kubwa